'Nilipata ujauzito kwa kutumia kidonge cha kuzuia mimba kilichopigwa marufuku'

Mwanamke mjamzito

Chanzo cha picha, Getty Images

Wakati Susan Wamaitha alipoanza kujisikia kuumwa mwaka mmoja uliopita, alidhani ni madhara ya tembe ya kuzuia mimba ambayo alikuwa ameanza kumeza miezi michache mapema - lakini ikawa kwamba alikuwa na ujauzito wa wiki nane.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 32 sasa ni mama wa watoto watatu. Bila kujua, kidonge alichoanza kutumia mnamo Juni 2021 kilipigwa marufuku nchini Kenya.

Jina la dawa hiyo la mtaani nchini Kenya ni "Sofia" lakini inatengenezwa nchini China na maelezo yote kuhusu bidhaa kwenye kifungashio yameandikwa kwa Kichina.

Tafsiri ya mstari wa kwanza inasema ina "Levonorgestrel Fast Tablets".

Kidonge ni "kinga ya uzazi wa mpango ya muda mrefu", kulingana na mstari wa pili.

Kisha kuna habari kuhusu mtengenezaji kwenye tatu: "Zizhu Pharmaceuticals Co Ltd".

Uuzaji wa dawa hiyo ulipigwa marufuku na mamlaka ya Kenya miaka 10 iliyopita kwa sababu ya viwango vya juu vya levonorgestrel - zaidi ya mara 40 ya viwango vilivyopendekezwa.

Levonorgestrel ni dawa ya homoni inayotumiwa katika njia kadhaa za udhibiti wa uzazi.

Watoto ambaio mama zao walipata ujauzito baada ya tembe ya dawa hiyo kushindwa kufanya kazi pia walipatikana kuwa walianza kubalehe mapema, kulingana na wizara ya afya ya Kenya.

Maumivu ya kichwa na kichefuchefu

"Sikujua ilikuwa imepigwa marufuku. Rafiki zangu wengi walikuwa wakiitumia na haikuwa na madhara yoyote," Bi Wamaitha aliambia BBC.

Kama wanawake wengine wengi wa Kenya, alivutiwa na tembe kwa uwezo wake wa kumudu na urahisi wa kumeza mara moja tu kwa mwezi.

dAWA

Chanzo cha picha, PPB

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wanawake huwa wananunua dawa ya Sofia kwa mwezi - wasambazaji wengi hawauzi nyingi kwa pamoja.

Kila kidonge kinagharimu kati ya shilingi 300 ($2.50; £2.20) na 400 za Kenya.

Mbinu nyingine za uzazi wa mpango zinazopatikana nchini ni pamoja na upandikizaji wa homoni ambao huchukua muda wa miezi mitatu, ambao hutolewa katika hospitali za serikali kwa gharama ya dola 5, mbinu nyingine ni kutumia koili, ambavyo hudumu kwa miaka kadhaa na gharama yake ni hadi $9.

Mipira ya Kondomu hutolewa bure katika ofisi za umma na vyoo lakini wakati mwingine huisha, ingawa zinaweza kununuliwa madukani.

“Kwa sababu nilikuwa na koili ya shaba isiyo na umbo la T ambayo ilikuwa ikinipa maumivu ya mgongo, niliamua kuitoa na kutumia kidonge hicho,” Bi Wamaitha aliambia BBC.

Aliitumia pia kwa sababu marafiki zake waliompendekeza Sofia hawakupata uzito wowote - jambo muhimu kwake kwani anasema anatatizika kupunguza uzito.

Hata hivyo, tangu mwanzo hakujisikia vizuri - ingawa alifikiri ingechukua muda tu kwa mwili wake kuzoea dawa mpya. "Nilianza kuumwa na kichwa na kujihisi kichefuchefu. Mwezi wa kwanza nilikosa hedhi," Bi Wamaitha alisema.

Lakini hakuwa na wasiwasi kwani hedhi yake ilikuja kwa mwezi wa pili - ni wakati tu iliporuka tena mwezi wa tatu ndipo alianza kuwa na wasiwasi.

Mume wake alianza kufanya utafiti kuhusu kidonge hicho cha uzazi wa mpango na hapo ndipo alipogundua kilikuwa kimepigwa marufuku.

“Tulianza kuingiwa na hofu kuhusu kutumia kidonge kilichopigwa marufuku na nilipogundua kuwa nimepata ujauzito niliingiwa na wasiwasi kuhusu madhara ambayo huenda yakampata mtoto wangu,” alisema.

Sasa wana mtoto wa kike wa miezi mitatu mwenye afya njema, lakini wenzi hao wamekasirishwa na ukosefu wa habari na athari zinazoweza kumkabili binti yao anapokua.

Dhana zinazogubika uzazi wa mpango

Nchini Kenya, uzazi wa mpango unaelekea kujadiliwa kimya kimya - hasa kwa sababu ya imani za kitamaduni na kidini katika kile ambacho ni jamii ya mfumo dume.

Baadhi ya wanaume hawaruhusu wake zao kutumia vidhibiti mimba huku baadhi ya madhehebu ya kidini yakipinga.

Madhehebu ya Kavonokya mashariki mwa Kenya, kwa mfano, yanakataa dawa zote za kisasa kwani inaamini kwamba Biblia inapendekeza tu maombi kama uingiliaji kati.

Kwa mtaalamu wa idadi ya watu na maendeleo Dk Josephine Kibaru, mbinu ya msingi itakuwa bora zaidi kupata uungwaji mkono wa njia za kisasa za upangaji uzazi.

"Tunahitaji wafanyakazi wa kujitolea wa afya ya jamii wawezeshwe zaidi na habari kwa sababu mwanamke anaweza kumwamini jirani na rafiki zaidi kuliko mfanyakazi wa afya ambaye ametumwa katika zahanati," Dkt Kibaru aliambia BBC.

Anasema kuna pengo la sintofahamu kuhusu njia za uzazi wa mpango zilizopo, huku kukiwa na imani potofu na imani potofu nyingi zinazohitaji kutupiliwa mbali.

Mchanganyiko wa zote mbili pengine ndio unaohitajika kwani daktari wa magonjwa ya wanawake Brigid Monda anasema wanawake wanapaswa kushauriana na watoa huduma za afya ili kuweza kupata njia ya kupanga uzazi ambayo inawafaa. "Ukubwa mmoja haufai zote," aliiambia BBC.

Hata hivyo baadhi ya wanawake pia wamelazimika kuchanganya njia tofauti za uzazi wa mpango kwa sababu ya kukosekana kwa ugavi thabiti katika zahanati zilizopo katika maeneo ya vijijini.

Sofia imeendelea kusambazwa licha ya marufuku yake - ukweli kwamba wanawake hawajui kuwa imepigwa marufuku inategemea ujumbe mbaya wa afya ya umma, kulingana na Dk Kibaru.

"Kutumia vyombo vya habari pekee haitoshi. Kutuma ujumbe kwa umma kimakusudi katika ngazi ya chini ni muhimu ili kuhakikisha raia wanaelewa vyema kwa nini dawa imepigwa marufuku," anasema.

Inauzwa kwa wateja wanaoaminika

Wauzaji dawa wanajua kuwa imepigwa marufuku - onyo lingine lilitolewa na Wizara ya Afya mwezi uliopita - lakini bado wanauza tembe hiyo kwa ajili ya mahitaji.

Haionekani, lakini inauzwa kisiri kwa wateja wanaoaminika wanaokuja kuinunua kila mwezi.

BBC ilitembelea maduka kadhaa ya dawa katika mji mkuu, Nairobi, kufanya uchunguzi kuhusu Sofia - wengi walisema dawa hiyo haiuzwi.

Muuzaji mmoja - ambaye hakutaka jina lake litajwe - alielezea kuwa inapatikana, sio tu kwenye maduka ya dawa bali pia wafamasia waliweza kuinunua kutoka kwa wasambazaji wanaoleta dawa hiyo kwenye mpaka kutoka nchi jirani.

Kwa hakika mapema mwezi huu, afisa wa Bodi ya Famasia na Sumu (PPB) aliliambia gazeti la Standard la Kenya kuwa shehena ilikuwa imenaswa kwenye mpaka wa Uganda.

Bi Wamaitha anasema alinunua tembe zake tatu kutoka kwa rafiki yake ambaye huzipata kwa wingi kutoka kwa mmoja wa wasambazaji hawa.

Anasema rafiki huyu na wengine walijua kidonge kilipigwa marufuku walipompendekeza.

Ujauzito wake haujawashawishi kuacha kuutumia - wala hakuna malalamiko yoyote kwenye makundi mbalimbali ya akina mama wa Kenya kwenye Facebook.

Angalau kwenye vikao vitatu kati ya hivi kumekuwa na mijadala kuhusu Sofia, ambapo wanawake kadhaa walioitumia walisema kuwa wamepata ujauzito.

Hili limemshawishi Bi Wamaitha kuendelea kuwahimiza marafiki zake na wanawake wengine kuzingatia njia tofauti ya kupanga uzazi.

"Najua tu kwamba kutajwa kwa kidonge hicho cha Sofia kunanishtua. Sijui kama nitatumia njia gani ya uzazi wa mpango kuzuia mimba ya nne, lakini nimemaliza, nimemaliza kidonge hicho."