'Kunaswa kuzimu': Mtu aliyenaswa kwenye kifusi cha jengo lililoporomoka alisimulia kilichomsibu

Chanzo cha picha, Delvin Safers
Akiwa amenaswa chini ya vifusi vya jengo la ghorofa tano ambalo liliporomoka katika mji wa pwani wa Afrika Kusini wa George, fundi umeme Delvin Safers alinaswa karibu na mwili wa mwenzake.
Alikuwa amekufa.
Bw. Safers aliogopa sana. Lakini zaidi ya yote, wakati huo, alikuwa na huzuni kwa mtu ambaye alikuwa rafiki baada ya kufanya kazi pamoja kwa muda wa miezi saba katika ujenzi wa ghorofa katika mji kando ya kile kinachojulikana kama scenic Garden Route.
Gorofa zenye mwonekano wa mlima sasa zilikuwa rundo la uchafu, viimarisho vya chuma vilivyosokotwa na kiunzi kilichochongwa, vikiwazika makumi ya wale waliokuwa wakifanya kazi kwenye eneo hilo.
Bw Safers alikumbuka kwamba simu yake ilikuwa mfukoni na kwa mkono wake mmoja alipiga simu yake ya kwanza, kwa ajili ya neno la mwisho na familia yake kwani alikuwa na hakika kwamba hatapona.
"Nilitaka kusema buriani kwa vile nilikuwa nimenaswa na nilifikiri kwamba yameisha kwangu," kijana huyo mwenye umri wa miaka 29 aliiambia BBC kutoka nyumbani kwake huko Mossel Bay, mji ulioko kilomita 40 kusini-magharibi mwa George, alikua akipona lakini alikuwa na sauti iliyochoka.
Dakika chache kabla ya kunasa kwake kwa bahati mbaya Jumatatu iliyopita mchana, alikuwa akijadili tatizo la umeme na mwenzake kwenye ghorofa ya tatu wakati, bila sauti au onyo, sakafu ilianguka chini yao.
"Niliona mgawanyiko huo wa pili tulipoanguka chini kwa sababu bado nakumbuka nikimtazama mwenzangu bado nilipokuwa ninaanguka."

Chanzo cha picha, Delvin Safers
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya mshtuko wa awali, Bw Safers alitumaini zaidi kwamba angenusurika.
“Sikuwa na hofu. Kwa saa 15 au zaidi zilizofuata nilikuwa mtulivu. Nilikuwa nikingoja pale, nikitumaini na kuomba mtu atupate."
Juu ya ardhi oparesheni tata ya uokoaji ilikuwa ikiendelea usiku kucha ikihusisha mashine za kusaga ardhi, visima na uchimbaji.
Makumi ya watu pia walikuwa wakiondoa vifusi kwa mikono polepole. Wengi wa wale ambao waliokolewa kwanza walikuwa wakifanya kazi kwenye orofa za juu.
Lakini baada ya muda ujasiri wa Bw. Safers ulififia na tumaini alilokuwanalo likageuka kukata tamaa. Alikuwa akitetemeka pasipo kujizuia, miguu yake ilikuwa ikitetemeka kwa maumivu, mgongo pia ulikuwa unamuuma na kuanza kuwa na mashaka kwamba asingetoka akiwa hai.
Maelezo ya sauti aliyokuwa akimtumia mpenzi wake na mwanawe, Zyar mwenye umri wa miaka miwili,ni kuwa alizidi kukata tamaa.
Akipumua sana na kulalamika kutokana na maumivu aliwaambia: "Sidhani kama nitafanikiwa."
Alisikia kwamba waokoaji walikuwa karibu lakini kila wakati walionekana kuwa wanakaribia saa zilipita na hakuna kitu kilichotokea, anasema.
"Nilikuwa kwenye nafasi ndogo sana ... nilikuwa nikilala juu ya vipande vya saruji, vipande vya saruji vilivyovunjika kwa saa 28.
"Sikuweza kusogea. Niliweza tu kulala chali au upande wangu mmoja. Hali ilikuwa ya kutisha, ilikuwa hali ngumu, ilikuwa baridi na giza, giza sana, ilikuwa kuzimu."
Kuwaza kuhusu mtoto wake ndiko kulikomfanya aendelee kupigana ili kubaki hai.

Chanzo cha picha, Getty Images
Alizipitia picha alizokuwa nazo Zyar na kukumbuka mara ya mwisho alipomuona. Mamake Bw Safers pia alikuwa amemtumia picha ya hivi karibuni ya mwanawe ili kumtia moyo.
Baada ya saa nane za kufanya kazi karibu naye, waokoaji walifanikiwa kumtoa mwenzake mmoja.
"Sikuweza kupumua wakati huo. Nilijua lazima niwe na nguvu na walikuwa hapa sasa na wangenitoa," anasema.
Lakini pamoja na ahueni, pia kulikuwa na hisia za mara kwa mara za huzuni kwa sababu watu wengi walikuwa bado wamenaswa ndani na wengine walikuwa wamekufa. Idadi ya vifo sasa imefikia 32.
Hatimaye, baada ya zaidi ya saa 28 chini ya vifusi, Bw Safers aliokolewa.
"Sikuwa na kiu wala njaa. Waliponipa maji, nilichukua lakini mwili wangu haukuwa na hamu ya kula wala kunywa. Sijui kwanini."
Alisafirishwa hadi hospitali kupata matibabu ya kuchanika kichwani na kuvunjika mbavu.
Bado haamini jinsi alivyotoka akiwa na majeraha machache na kuruhusiwa kutoka hospitalini baada ya siku mbili tu.
"Inashangaza. Sijui jinsi hilo lilivyotokea... Nimefarijika, sijui ni jinsi gani itawezekana kuondokana na majeraha madogo lakini niliweza."
Ni wazi bado ana kiwewe na ana wasiwasi mwingi kuhusu wale wote aliofanya nao kazi ambao wanabaki wamenaswa baada ya zaidi ya wiki moja. Kuna watu 20 ambao hawajulikani walipo .
Maswali sasa yanageukia chanzo cha ajali hiyo, na mamlaka zinasema uchunguzi unaendelea.
Bw.Safers anasema hakumbuki dalili zozote kwamba kuna kitu kinaweza kuwa kibaya, lakini anafikiria kwamba ikiwa itabainika kuwa njia za mkato zilichukuliwa katika ujenzi huo, basi watu "wawajibike kwa maisha yaliyopotea na watu ambao hawawezi tena kamwe kufanya kazi au kutembea tena”.
End of Maelezo zaidi:
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi












