Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Nato na Ulaya 'hawathamini tunachofanya', - Trump

Rais wa Marekani Donald Trump apuuzilia mbali mapendekezo kwamba kunyakua Greenland kungekuwa pigo kwa Nato.

Muhtasari

Moja kwa moja

Lizzy Masinga & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Shukran kwa kufuatilia na kuwa na usiku mwema

  2. Araqchi aonya kuhusu nia ya kushambulia Iran na Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu

    Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ametoa onyo kuhusu uwezekano wa shambulio la Marekani dhidi ya Iran pamoja na tishio la moja kwa moja kwa Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu.

    Onyo hilo limetolewa kupitia makala mbili tofauti moja iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya Ali Khamenei na nyingine katika gazeti la Marekani The Wall Street Journal.

    Katika makala yake ya lugha ya Kiajemi, Bw. Araqchi alikemea kile alichokitaja kuwa ni “vitisho vya wazi na vinavyojirudia” kutoka kwa Rais wa Marekani dhidi ya Ayatollah Ali Khamenei.

    Alisisitiza kuwa vitisho vinavyomlenga “kiongozi mkuu wa nchi huru” ni kitendo kisichokubalika na kinachokiuka misingi ya mahusiano ya kimataifa.

    Akiendelea kuandika kwenye tovuti ya Ali Khamenei, Araqchi alieleza kuwa Marekani inapaswa kuwajibishwa kwa matendo yake dhidi ya Iran.

    Katika makala nyingine iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza na kuchapishwa katika The Wall Street Journal, Waziri huyo wa Mambo ya Nje alimuelezea Rais wa Marekani, Donald Trump, kama mtu anayejiona kuwa mpatanishi wa mikataba, lakini akabainisha kuwa hatua zake katika eneo la Mashariki ya Kati zimezalisha migogoro na vita pekee.

    Soma Pia:

  3. Trump asema atakutana na Rais wa Ukraine Zelensky

    Rais Donald Trump alisema kuwa atakutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kando ya Kongamano la Kiuchumi la Dunia huko Davos.

    Hata hivyo haijulikani ni lini hii itatokea.

    "Rais yuko Kyiv," mshauri wa Zelensky, Dmytro Lytvyn aliwaambia waandishi wa habari, muda mfupi tu baada ya Trump kuliambia jukwaa kwamba viongozi hao wawili wanaweza kukutana baadaye leo na kwamba Zelensky anaweza kuwa "katika hadhira".

    Trump alitoa wito kwa Zelensky na Rais wa Urusi Vladimir Putin kumaliza vita nchini Ukraine, akisema kuwa nchi hizo ziko katika nafasi ya kufanya makubaliano.

    "Lazima ufanye mpango huu. Watu wengi sana wanakufa. Haifai," Trump alisema katika kipindi cha maswali na majibu baada ya matamshi yake rasmi kwenye kongamano la Davos.

    "Ikiwa hawatafanya hivi ni wajinga," Trump alisema kuhusu Zelensky na Putin.

    Soma pia:

  4. Je, kuna ushahidi wowote kwamba Trump amemaliza vita 8?

    Rais Trump kwa mara nyingine tena amerudia madai yake maarufu ya kutia shaka kwamba "amemaliza vita nane.

    BBC Verify hapo awali ilichunguza dai hili kwa kina.

    Vita vinane, kulingana na Ikulu ya White, ni vile kati ya:

    Israel na Hamas

    Israel na Iran

    Pakistan na India

    Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)

    Thailand na Kambodia

    Armenia na Azerbaijan

    Misri na Ethiopia

    Serbia na Kosovo

    Baadhi ya "vita" hivi vilidumu kwa siku chache tu, licha ya kuwa ni matokeo ya mivutano ya muda mrefu.

    Katika kisa kimoja, "vita" kati ya Misri na Ethiopia vilikuwa mzozo juu ya ujenzi wa bwawa, na hakuna vita halisi vilivyosimamishwa.

    Kulikuwa pia na vita kati ya Rwanda na DRC, ingawa pande zote mbili zilitia saini makubaliano ya amani huko Washington.

    Soma Pia:

  5. Trump anataka 'mazungumzo ya haraka' kupata Greenland lakini anasisitiza 'hatatumia nguvu'

    Rais Trump amesema kuwa viongozi wa Marekani wamekuwa wakitafuta kununua Greenland kwa karne nyingi.

    Trump amesema "hakuna dalili" kwamba Denmark inamiliki kisiwa hicho, na kwamba Denmark ilikuwa ikitumia pesa kidogo kwa Greenland kuliko ilivyoahidi.

    "Marekani pekee ndiyo inaweza kulinda ardhi hii kubwa, eneo hili kubwa la barafu, na kuliendeleza," alisema.

    Hii, anasema, ndiyo sababu anataka "mazungumzo ya haraka" kupata kisiwa hicho.

    Aliongeza: "Hatutafanikiwa chochote isipokuwa tukiamua kutumia nguvu kupita kiasi. Hatuwezi kuzuiwa, lakini hatutafanya hivyo." Kitu pekee ambacho Marekani inadai, anasema, ni "mahali panapoitwa Greenland".

    Soma pia:

  6. Trump asema 'Ulaya haielekei katika mwelekeo sahihi'

    Rais wa Marekani Donald Trump akiwahutubia viongozi wa dunia huko Davos, ameanza kwa kusema Ulaya "haielekei katika mwelekeo sahihi''.

    Trump anasema "haitambui Ulaya", na kuongeza: "Naipenda Ulaya, nataka kuiona ikifanya vyema lakini haiendi katika mwelekeo sahihi."

    "Sitaki kumtukana mtu yeyote", Trump anaendelea, lakini anaongeza kuwa marafiki wanarudi kutoka sehemu za Ulaya na wanamwambia hawatambui Ulaya.

    Anataja "uhamiaji wa watu wengi ambao haujadhibitiwa", na rekodi ya bajeti na nakisi za biashara.

    ''Sehemu za ulimwengu wetu zinaharibiwa mbele ya macho yetu na viongozi hawafanyi chochote juu yake'', Trump anasema, lakini haifafanui hili.

    Trump anadai kuwa katika mwaka mmoja alipunguza nakisi ya biashara ya kila mwezi ya Marekani kwa 77% bila mfumuko wa bei - jambo ambalo anasema kila mtu alisema haliwezi kufanywa.

    ''Wataalamu walidai mipango yangu ingesababisha kushuka kwa uchumi na mfumuko mkubwa wa bei lakini tumethibitisha kuwa sio sawa'', anasema huku viongozi wa Ulaya wakiendelea kumsikiza.

  7. Nato na Ulaya 'hawathamini tunachofanya', anadai Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amepuuzilia mbali mapendekezo kwamba kunyakua Greenland kungekuwa pigo kwa Nato.

    Marekani inatendewa isivyo haki na Nato, anasema, na kuongeza: "Tunatoa sana na tunapata malipo kidogo." "Hungekuwa na Nato ikiwa singehusika," anasema. "Hawathamini tunachofanya. Nazungumzia Nato na Ulaya."

    Hata hivyo wachambuzi wameeleza kuwa madai ya Trump kwamba Marekani haijapata "chochote" kutoka kwa Nato mbali na jukumu lake wakati wa Vita Baridi ni ya kupotosha.

    Baada ya Marekani kushambuliwa tarehe 11 Septemba, Nato ilitumia Kifungu cha 5 - ikimaanisha kuwa shambulio dhidi ya mwanachama mmoja linachukuliwa kuwa ni shambulio dhidi ya mwingine ambalo lilisababisha uungwaji mkono mkubwa, ikiwa ni pamoja na onyo la anga na doria za uchunguzi juu ya Marekani.

    Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mali za kijeshi za Nato kutumika kufuatia maombi ya Kifungu cha 5.

    Zaidi ya hayo, nchi nyingi za Nato - ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Ufaransa, Italia na Uingereza zilituma askari katika Kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi na Utulivu kinachoendeshwa na Nato, au ISAF, nchini Afghanistan.

    Soma pia:

  8. Venezuela itanufaika kifedha kwa kiwango kikubwa chini ya Marekani - Trump

    Rais wa Marekani, Donald Trump ameeleza gharama za mafuta chini ya mtangulizi wake, Rais wa zamani Joe Biden, akikosoa kile anachodai kuwa bei zilipanda kutokana na sera za kijani.

    Chini ya urais wake, uzalishaji wa mafuta na gesi uko juu, alisema.

    Akigusia kuhusu mapipa milioni 50 ya mafuta anayodai yalikamatwa kutoka Venezuela na kuletwa Marekani.

    Anasema "mara baada ya shambulio kumalizika, walisema, 'tufanye makubaliano'. Watu zaidi wanapaswa kufanya hivyo".

    Marekani ilimkamata Rais wa Venezuela Nicolás Maduro kutoka kwa boma yake huko Caracas mapema mwezi huu.

    Tangu wakati huo Trump amemsifu aliyechukua nafasi ya Maduro, kaimu Rais Delcy Rodríguez.

    "Venezuela itatengeneza pesa nyingi zaidi katika miezi sita ijayo kuliko walivyopata katika miaka 20 iliyopita," anadai.

    Soma Pia:

  9. Al-Shabaab wadhibiti kambi ya kijeshi ya Jubaland huko Kudhaa

    Ripoti kutoka wilaya ya Kudhaa ya utawala wa Jubaland zinaonyesha kuwa kundi la al-Shabaab lilishambulia kambi ya jeshi ya Jubaland hapo mwendo wa saa tatu asubuhi ya leo.

    Wenyeji pia wanasema kuwa kundi hilo limeteka kijiji cha Kudhaa na sasa linadhibiti.

    Wakati huo huo, kuna ripoti za raia kupigwa risasi majumbani mwao. Vifo vinaripotiwa.

    Bado hatujapokea taarifa rasmi kutoka kwa Jubaland kuhusiana na majeruhi waliokumbana na vikosi vyao.

    Kambi hiyo ambayo sasa inakaliwa na Al-Shabaab hapo awali ilikuwa inakaliwa na wanajeshi wa Kenya.

    Soma pia:

  10. Japan yaanzisha tena mtambo mkubwa zaidi wa nyuklia duniani

    Japan imeanza tena uendeshaji wa kinu kimoja katika mtambo mkubwa zaidi wa nyuklia duniani, takriban miaka 15 baada ya janga la kituo cha nyuklia cha Fukushima kulazimisha kusitishwa kwa mitambo yote ya nyuklia nchini humo.

    Kinu namba sita katika mtambo wa Kashiwazaki–Kariwa, ulioko kaskazini-magharibi mwa mji wa Tokyo, kilianzishwa tena Jumatano baada ya kucheleweshwa kwa siku moja kutokana na hitilafu ya mfumo wa tahadhari.

    Kinu hicho kinatarajiwa kuanza uzalishaji wa kibiashara mwezi ujao.

    Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Japani wa kurejesha hatua kwa hatua matumizi ya nishati ya nyuklia, ingawa mchakato huo bado una changamoto nyingi.

    Kinu cha saba hakitarajiwi kurejeshwa hadi mwaka 2030, huku mitambo mingine mitano ikikabiliwa na uwezekano wa kuondolewa kabisa.

    Hali hii imepunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uzalishaji wa mtambo huo ikilinganishwa na uwezo wake wa awali wa gigawati 8.2, wakati mitambo yote saba ilikuwa ikifanya kazi.

    Kwa muda mrefu Japan imekuwa ikitegemea kwa kiwango kikubwa uagizaji wa nishati kutoka nje, hali iliyoiweka miongoni mwa nchi za mwanzo kuwekeza katika nishati ya nyuklia.

    Hata hivyo, matarajio hayo yalivunjika mwaka 2011 kufuatia tukio linalokumbukwa kama mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya nyuklia katika historia ya dunia.

    Janga hilo lilisababishwa na tetemeko la ardhi lenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Japani, na kusababisha kuyeyuka kwa mitambo ya nyuklia katika kituo cha Fukushima Daiichi pamoja na kuvuja kwa mionzi hatari.

    Tukio hilo liliacha athari kubwa za kijamii na kisaikolojia, hususan kwa jamii zilizohamishwa, ambazo nyingi bado hazijarejea makwao licha ya uhakikisho wa serikali kuhusu usalama wa maeneo hayo.

    Wakosoaji wanadai kuwa mmiliki wa kituo hicho, Kampuni ya Umeme ya Tokyo (Tepco), haukuwa umejiandaa ipasavyo kukabiliana na janga hilo, huku uratibu kati ya kampuni na serikali ukitajwa kuwa dhaifu.

    Ripoti huru ya serikali ililitaja tukio hilo kuwa “janga lililosababishwa na binadamu” na kuilaumu Tepco, ingawa baadaye mahakama iliondoa mashtaka ya uzembe dhidi ya watendaji watatu wa zamani wa kampuni hiyo.

    Hata hivyo, hofu ya umma na mmomonyoko wa imani kwa sekta ya nyuklia uliibua upinzani mkubwa dhidi ya matumizi ya nishati hiyo, hali iliyosababisha Japan kusimamisha mitambo yake yote 54 ya nyuklia muda mfupi baada ya janga la Fukushima.

    Soma zaidi:

  11. Mke wa Besigye aeleza sababu za mumewe kufungwa gerezani licha ya kuwa mgonjwa

    Winnie Byanyima, mke wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda aliyefungwa jela Kizza Besigye amewalaumu Rais mteule Yoweri Museveni na mtoto wake wa kiume Jenerali Muhoozi Kainerugaba kwa kile alichokitaja kama kumuweka kizuizini kiharamu na kumyanyasa mumewe kwa kupinga mpango wa urithi wa urais.

    Akizungumza akiwa nyumbani kwake eneo la Kasangati, Uganda amesema Besigye amezuiliwa kimakusudi kwa kupinga nia ya kumrithisha Jenerali Muhoozi kama rais ajaye.

    Kulingana naye, anasema Besigye amezuiliwa chini ya udhibiti wa kijeshi katika gereza la luziro.

    Soma Pia:

  12. Kizza Besigye yuko hali mahututi - Chama chake

    Afya ya mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye "imefikia hali mbaya na mbaya", chama chake kinasema, baada ya kupelekwa kwenye kituo cha matibabu katika mji mkuu, Kampala.

    Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 69 alikimbizwa katika kituo cha matibabu cha kibinafsi chini ya "ulinzi mkali", chama cha People's Front for Freedom (PFF) kilisema, bila kutaja anasumbuliwa na nini.

    Hata hivyo, wakuu wa magereza walikanusha kuwa afya ya Besigye ilikuwa mbaya, na kuelezea ziara yake ya usiku kwa daktari kama "uchunguzi wa jumla".

    Besigye, daktari wa zamani wa Rais Yoweri Museveni na mmoja wa wapinzani wake wa muda mrefu wa kisiasa, amekuwa kizuizini tangu Novemba 2024.

    Kiongozi huyo wa PFF alishtakiwa katika mahakama ya kijeshi kwa kosa la uhaini, ambalo lina hukumu ya kifo, pamoja na kumiliki bunduki kinyume cha sheria na kutishia usalama wa taifa.

    Amekanusha tuhuma hizo.

    Besigye, ambaye amewania urais dhidi ya Museveni mara nne, amekuwa kizuizini na mshirika wake Obeid Lutale tangu wote wawili walikamatwa nchini Kenya na kurudishwa Uganda.

    Soma zaidi:

  13. Mafuriko ya Msumbiji yawalazimu maelfu kukimbia huku maji yakijaa pomoni

    Afrika Kusini imetuma timu kusaidia juhudi za uokoaji baada ya mwanasiasa wa eneo hilo kusombwa na mafuriko alipokuwa akizuru nchi jirani ya Msumbiji.

    Andile Mngwevu, diwani katika manispaa ya Ekurhuleni, mashariki mwa Johannesburg, na wengine wanne walikuwa katika jimbo la Gaza nchini Msumbiji wakati gari lao lilipokumbwa na mafuriko, maafisa wanasema.

    Ni mmoja tu wa abiria ambaye amegunduliwa "hadhi na mahali walipo abiria wengine bado haijathibitishwa", manispaa ilisema katika taarifa.

    Mafuriko yameharibu sehemu za nchi zote mbili na kusababisha Rais wa Msumbiji Daniel Chapo kufuta safari yake ya Mkutano wa Kiuchumi wa Dunia huko Davos.

    Msumbiji imetangaza tahadhari ya hali ya ta dharura kutokana na mafuriko makubwa huku Afrika Kusini ikitangaza janga la kitaifa.

    Msimu wa mvua umeanza katikati na kaskazini mwa Msumbiji, na utabiri wa mvua kubwa zaidi katika sehemu kubwa za nchi, ambayo inaingia msimu wake wa kila mwaka wa vimbunga.

    Soma pia:

  14. Ulaya 'imejiandaa kuchukua hatua kwa dharura' kuhusu Greenland - mkuu wa EU

    Mkuu waTume ya Ulaya, Ursula von der Leyen anasema akiwa Davos kuwa Ulaya imejipanga kukabiliana na Trump kuhusu azimio la Trump kudhibiti Greenland.

    Siku ya Jumanne, Rais wa Ufaransa Macron alisema EU inaweza kuzingatia chaguzi kadhaa za kulipiza kisasi ikiwa ni pamoja na "kutunisha misuli ya biashara".

    Wakati huo huo, Rais wa Marekani yuko njiani kukutana na viongozi wa dunia katika mkutano huo lakini anachelewa baada ya Air Force One kulazimika kugeuka kutokana na "suala dogo la umeme".

    Trump anatishia kuongeza ushuru wa asilimia10% kwa "bidhaa zozote na zote" zinazoagizwa kutoka nchi nane za Ulaya kuanzia tarehe 1 Februari ikiwa watapinga pendekezo lake la kutwaa Greenland.

    Unaweza kusoma;

  15. Mambo yaenda mrama Man City, Guardiola akerwa na kipigo cha Klabu Bingwa

    Bodo /Glimt kutoka Norway iliwafedhehesha miamba wa soka wa Uingereza Manchester City kwa kuwachabanga mabao 3-1 katika mechi ya klabu bingwa ulaya jana usiku.

    Huu ni ushindi wa kwanza wa Bodo katika historia ya michuano ya Klabu Bingwa. Kwa kipigo hicho,Manchester City ni sharti washinde mechi yao ya mwisho dhidi ya Galatasaray ya Uturuki la sivyo watalazimika kuingia katika mchujo wa kufuzu raundi ya 16.

    Usiku huo ulikuwa wa aibu kwa Man City katika michuano hiyo na hakika ni muendelezo wa matokeo yao mabovu wakiwa hawajashinda hata mechi moja mwaka huu wa 2026.

    Sasa je, hii ni ajali ya kuteleza tu kazini tu kwa Pep Guardiola ama ni kweli kuna majanga City?

    Kulinganisha thamani ya timu hizi mbili Bodo na City ni kama mfano wa maji na damu.

    Miaka kumi iliyopita Bodo walikuwa wanacheza katika Ligi ya Daraja la Pili huko Norway.

    Ni klabu ndogo sana ikilinganishwa na Man City iliyotumia zaidi ya pauni milioni 200 kuboresha kikosi chao msimu huu.

    Mambo yanakwenda mrama..Baada ya kumaliza mwaka jana vizuri kwa kushinda mechi nane mtawalia. Man City wameufungua mwaka huu wakiwa shaghla baghla.

    Wameshinda mechi mbili tu katika saba walizocheza ikiwemo kutitigwa vibaya na Manchester United wikendi iliyopita katika Ligi Kuu ya Premia.

    Guardiola alikiri kuwa mambo hayaendi sawa, huku wasiwasi ukiongezeka kuhusu ongezeko la majeruhi, kusimamishwa kwa Rodri akitumikia, na ukame wa mabao wa Erling Haaland.

    Upande mwingine, Bodo/Glimt walisifiwa kwa nidhamu ya kiufundi, kasi, matokeo ambayo yanahesabika kuwa moja ya ushindi mkubwa zaidi katika historia ya soka la Norway.

    Maelezo zaidi:

  16. Trump kuhutubia viongozi wa dunia Davos baada ya kusisitiza mpango wake kuhusu Greenland

    Rais wa Marekani Donald Trump leo anatarajiwa kutoa hotuba kwa viongozi wa dunia huko Davos, Uswisi, baada ya kusisitiza tena vitisho vyake vya kuchukua udhibiti wa Greenland.

    Anatarajiwa kuzungumza katika Jukwaa la Uchumi Duniani, ambapo jana Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alionya kuhusu “mabadiliko kuelekea dunia isiyo na sheria”. Trump amesema kuna “mikutano mingi iliyopangwa kuhusu Greenland”.

    Haya yanajiri baada ya kuulizwa katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne ni kwa kiwango gani yuko tayari kwenda ili kuipata Greenland, naye akajibu: “Mtajua.”

    Kuwasili kwake Davos kunatarajiwa kuchelewa kutokana na “hitilafu ndogo ya umeme” kwenye ndege ya Air Force One.

    Wakati huo huo, Waziri wa Viwanda na Rasilimali Asilia wa Greenland, Naaja Nathanielsen, aliiambia BBC: “Hatutaki kuwa Wamarekani, na tumekuwa wazi kabisa kuhusu hilo.”

    Unaweza kusoma;

  17. Maambukizi ya surua yaongezeka South Carolina nchini Marekani

    Takribani kesi 88 mpya za surua zimeripotiwa huko South Carolina, huku mlipuko ukiendelea kuongezeka, na maambukizi 646 yameripotiwa katika jimbo hilo tangu Oktoba, kulingana na maafisa.

    Maafisa wa afya wa jimbo wanasema zaidi ya watu 500 na wanafunzi katika shule 15 wako karantini baada ya kuathiriwa na virusi.

    Mlipuko huu, mbaya zaidi tangu Texas kuripoti kesi zaidi ya 700 za surua mwaka 2025, unaiweka Marekani katika hatari ya kupoteza hadhi yake ya katika jitihada za kuondoa surua.

    Surua ni mojawapo ya magonjwa yenye kuambukiza sana duniani, ikienea kwa njia ya hewa, kupitia kukohoa na kupiga chafya, huku hadi 90% ya watu wasiochanjwa walio karibu wakikutana na virusi wanaweza kuambukizwa.

    Miezi 12 iliyopita imeashiria mlipuko mbaya zaidi wa surua Marekani katika miongo kadhaa, ukiwemo maambukizi zaidi ya 2,000.

    Watu watatu walifariki Texas, na katika miezi ya hivi karibuni Utah na Arizona pia zimeripoti mamia ya kesi za surua.

  18. Dereva afariki katika ajali ya treni Hispania siku chache baada ya ajali ya treni ya mwendokasi

    Dereva wa treni amepoteza maisha na takribani watu 37 kujeruhiwa, watano vibaya, baada ya treni ya abiria kutoka njia kuu kugonga na karibu na jiji la Barcelona, siku chache tu baada ya ajali ya treni mbili iliyogharimu maisha kusini mwa Uhispania Jumapili.

    Kulingana na maafisa wa eneo hilo, Jumanne jioni treni ya Rodalies iligonga ukuta wa kizuizi uliopinduka na kuanguka kwenye reli kati ya Gelida na Sant Sadurní.

    Mkaguzi wa ajali za moto wa mkoa wa Catalonia, Claudi Gallardo, alisema abiria wote waliondolewa kutoka kwenye treni.

    Tukio hili lilitokea wakati dhoruba kubwa zikipiga kaskazini-mashariki mwa Hispania, huku maeneo ya pwani mashariki na kaskazini-magharibi mwa Hispania yakiwa katika tahadhari kubwa kutokana na hali ya hewa.

  19. Polisi wa Nigeria wathibitisha kutekwa kwa waumini kutoka makanisani baada ya awali kukana

    Polisi wa Nigeria wamebadili msimamo wao wa awali, wakithibitisha kwamba waumini kweli walitekwa nyara huko Kurmin Wali.

    Karibu saa 48 baada ya tukio, polisi walisema usiku wa Jumanne kuwa taarifa ya awali iliyokanusha shambulio hilo “ilieleweka vibaya kwa kiasi kikubwa.” Walisema ilikuwa “siyo kukana tukio hilo bali ni jibu la tahadhari hadi kuthibitisha maelezo kutoka eneo lilipotokea tukio, ikiwa ni pamoja na utambulisho na idadi ya walioathirika.”

    Msemaji wa polisi, Benjamin Hundeyin, alisema ukaguzi uliofanywa baadaye na vitengo vya operesheni na vyanzo vya kijasusi umethibitisha kwamba utekaji nyara kweli ulifanyika.

    Hatujapewa idadi kamili ya waliochukuliwa au waliokimbia, lakini alisema nguvu za usalama zimetumwa kikamilifu Kajuru na jamii zinazozunguka. Aliongeza kuwa operesheni za utafutaji na kuokoa pamoja na doria zinaendelea.

    Amnesty International imeikosoa serikali ya Nigeria kutokana na kile ilichokielezea kama “kukana wa kukatisha tamaa” kuhusu tukio hilo.

    Kikundi hicho cha haki za binadamu kiliongeza kuwa, “Mamlaka pia lazima ianze kuchukua hatua za haraka na za wazi ili kuzuia utekaji wa nyara unaoenea kwa kasi ambao unazidi kuwa jambo la kawaida Nigeria.”

    Awali, wanajamii waliwaambia BBC kwamba waumini 177 walitekwa nyara kutoka makanisa matatu huko Kurmin Wali. Walisema watu 11 walitoroka baadaye, na kuacha zaidi ya watu 160 bado wakiwa mateka. Orodha iliyopatikana na BBC siku ya Jumanne ina zaidi ya majina 160, ingawa haya bado hayajathibitishwa kwa uhuru.

    Shuhuda mmoja alisema shambulio hilo lilitokea takriban saa 4 asubuhi kwa muda wa eneo hilo Jumapili.

    “Baadhi ya watu walijaribu kukimbia, lakini hawakuweza kwa sababu wanaume wenye silaha walizunguka kijiji,” alisema. “Walikusanya watu pamoja na baadaye kuwalazimisha kutembea kwenda msituni.”

  20. Rais wa zamani atuhumiwa kwa njama ya mauaji afukuzwa Togo, arejeshwa Burkina Faso

    Togo imemkamata na kumrudisha nchini Burkina Faso aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, baada ya mamlaka mjini Ouagadougou kumtuhumu kupanga njama ya kumuua mrithi wake.

    Paul-Henri Sandaogo Damiba, aliyepata madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2022 kabla ya kuondolewa madarakani na Ibrahim Traoré miezi minane baadaye, anatuhumiwa na utawala wa sasa kuwa ndiye aliyepanga jaribio la kumuua Traoré.

    Kwa mujibu wa wizara ya sheria ya Togo, Damiba alikabidhiwa kwa mamlaka ya Burkina Faso siku ya Jumamosi.

    Wizara hiyo ilisema kuwa kama sehemu ya makubaliano hayo, Burkina Faso iliahidi kuhakikisha “usalama, heshima na kesi ya haki kwa Bw. Paul-Henri Sandaogo Damiba, pamoja na kutotumika kwa adhabu ya kifo.”

    Kati ya mashtaka yaliyowekwa dhidi ya Damiba na serikali ya kijeshi ya Burkina Faso ni pamoja na “kuiba fedha za umma, kupata utajiri kinyemela, ufisadi, kupokea mali zilizoporwa kwa hali ya hatari na utakatishaji wa fedha,” kulingana na taarifa ya wizara ya sheria ya Togo.

    Hakuna maoni yoyote kutoka kwa Damiba kuhusu mashtaka hayo yaliyoripotiwa, na wala simu za BBC hazijapokelewa.

    Yaliyozidi kuwa makubwa ni mashtaka ya njama za mauaji.

    Mapema mwezi huu, Waziri wa Usalama wa Burkina Faso, Mahamadou Sana, alitangaza kwenye televisheni ya serikali kwamba vikosi vya usalama vilizuia mpango wa mfululizo wa mauaji yaliyozingatia kulenga watu binafsi kwa lengo la kutuliza serikali.

    Maafisa mjini Ouagadougou mara kwa mara wamemshutumu Damiba kwa kupanga njama kutoka uhamishoni. Mwishoni mwa mwaka 2024, alitajwa tena hadharani kama kiongozi wa kile mamlaka yalichokiita “tawi la kijeshi” la njama kubwa zaidi.

    Damiba aliibuka madarakani kwa mara ya kwanza Januari 2022, baada ya kuangusha serikali iliyochaguliwa ya Roch Marc Christian Kaboré kutokana na kutoaminika kwa serikali kushughulikia vurugu za kiislamu.

    Lakini baada ya miezi minane tu, yeye mwenyewe aliondolewa madarakani na Traoré, afisa wa makombora wa umri wa miaka 34 ambaye alimdai kushindwa kuboresha usalama.

    Tangu wakati huo, junta inayosimamiwa na Traoré imeimarisha udhibiti wake nchini, ikituma walowezi wa Kifaransa, ikichukua msimamo mkali wa kitaifa na hivi karibuni kurejesha adhabu ya kifo, ikiwemo kwa makosa ya uhaini ya hali ya juu.

    Licha ya ahadi za kurejesha utulivu, Burkina Faso bado inakabiliwa na moja ya migogoro mikali ya usalama duniani, huku mashambulizi ya kigaidi ya kiislamu yakiendelea katika sehemu kubwa za nchi.

    Unaweza kusoma;