India na Pakistani: Nani mbabe wa kijeshi kati ya mataifa haya yanayozozana?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Pakistan inasema ilizidungua droni 25 za India zenye silaha (SiHAs) kote nchini kufuatia mashambulizi ya eneo la Kashmir linalotawaliwa na Pakistan .

Msemaji wa jeshi la Pakistan Ahmed Sharif alielezea matukio hayo kama "kitendo kingine cha wazi cha uvamizi wa kijeshi wa India".

Kwa upande wake, India inasema ilidungua ndege zisizo na rubani za Pakistan pamoja na makombora yake yaliyorushwa na Pakistan. "

Tunalinganisha uwezo wa kijeshi wa nchi hizo mbili.

Pia unaweza kusoma

Droni

Nchi zote mbili zinapanua ndege zao zisizo na rubani UAV kwa kuagiza na kuendeleza teknolojia asilia, lakini India iko mbele kwa idadi.

Akiongea na BBC, mchambuzi wa masuala ya ulinzi Rahul Bedi amesema nchi hiyo yenye watu wengi zaidi duniani itadhibiti takriban ndege zisizo na rubani 5,000 katika miaka miwili hadi minne ijayo.

India imetia saini makubaliano na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kununua ndege 31 zisizo na rubani aina ya MQ-9B SkyGuardian na za bhadrini kwa jina la SeaGuardian UAV mwaka wa 2024.

Ingawa Pakistan ina UAV chache kuliko India, wana uwezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji, upelelezi na mashambulizi yenye usahihi.

Nguvu kubwa ya UAV za Pakistani ziko katika uzoefu wao wa mapigano. Kwa mfano, UAV ya kiasili, Burak, imetumika katika shughuli za kukabiliana na ugaidi tangu 2015. Pia inanunua droni za hali ya juu kutoka Uturuki na Uchina.

Bajeti ya ulinzi na ukubwa wa jeshi

Kuna wasiwasi mpya kwamba nchi hizo mbili zitatumbukia tena katika vita vya pande zote, kama ilivyokuwa mwaka 1999.

India ina jeshi la nne kwa nguvu zaidi, kulingana na Kielelezo huru cha Global Firepower Index (GFI), ambacho kinaorodhesha nguvu za kijeshi duniani, na wanajeshi wanaofanya kazi zaidi ya milioni 1.4, wakati Pakistan ina wanajeshi 654,000.

Kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), India ilitumia mara tisa zaidi katika ulinzi kuliko Pakistan mnamo 2024.

Kwa upande wa vikosi vya ardhini, India ina zaidi ya vifaru 4,200 na magari ya kivita 150,000.

Pakistan ina zaidi ya Vifaru 2,600 na chini ya magari 18,000 ya kivita.

Jeshi la angani la India lina ndege 2,229, zikiwemo ndege 513 za kivita na 130 za kulipua mabomu.

Kulingana na GFI, jeshi la anga la Pakistan lina karibu ndege 1,400.

Idadi ya meli za wanamaji za India ni mara mbili za Pakistan ikiwa na meli 293.

Makombora na silaha za nyuklia

Programu ya makombora ya Pakistani ina makombora ya masafa marefu (yaliyoundwa kwa uwanja wa vita), pamoja na makombora ya masafa mafupi na ya kati.

Makombora ya India ni tofauti zaidi, yakiwemo makombora ya Prithvi yanayoweza kuruka umbali wa kilomita 250 hadi 600; makombora ya mfululizo ya Agni yanayoweza kuruka umbali wa kilomita 1,200 hadi 8,000; mbali na makombora ya cruise ya Nirbhaya na Brahmos.

Idadi kubwa ya makombora ya India pia inakusudiwa kutishia Uchina, jirani mwingine ambaye nchi hiyo ina mizozo ya kieneo naye.

Hatahivyo, hii haimaanishi kuwa Pakistan inaweza kushindwa kwa urahisi kwa sababu nchi zote mbili zina silaha za nyuklia zenye nguvu sawa.

Kulingana na makadirio ya SIPRI, India ina vichwa 172 vya nyuklia na Pakistan ina vichwa 170 vya nyuklia.

Lakini haijulikani ni vingapi kati ya vichwa hivi vya vita ambavyo nchi hizo mbili ziko tayari kutumia. Pakistan inaunda silaha za nyuklia ili kushindana na India, wakati India inazingatia silaha za masafa marefu ambazo zinaweza kulenga Uchina.

China, jirani ya India na Pakistani, imepanua silaha zake za nyuklia kwa 22%, na kuongeza idadi ya vichwa vya nyuklia kutoka 410 hadi 500. Matokeo yake yanaweza kuwa janga.

Hatari ni kubwa sana, ndiyo maana jumuiya ya kimataifa inatoa wito kwa nchi zote mbili kujizuia.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla