Zelensky yuko tayari kufanya kazi na Trump

Hatua hiyo inafuatia majibizano yao ya ijumaa iliyopita ambayo Zelensky anayataja kama ya kujutia na hayakufanyika kama ilivyopangwa

Muhtasari

Moja kwa moja

Rashid Abdallah

  1. Mwisho wa habari zetu za moja kwa moja, Asante.

  2. Kauli ya Vance yakosolewa kudhoofisha juhudi za ulinzi wa amani

    xyz

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Makamu wa rais wa Marekani amekosolewa na watu, mashirika, na nchi mbalimba kufuatia maoni aliyoyatoa kuhusu uwezekano wa kushirikishwa kwa vikosi vya kimataifa kusimamia makubaliano ya amani nchini Ukraine.

    Wanasiasa wa upinzani nchini Uingereza walimshutumu JD Vance kwa kudhalilisha vikosi vya Uingereza, baada ya kusema kwenye kituo cha Fox News kwamba mchango wa Marekani katika uchumi wa Ukraine ilikuwa "dhamana bora ya usalama kuliko askari 20,000 kutoka kwenye nchi yoyote dhaifu ambayo haijapigana vita kwa miaka 30 au 40."

    Uingereza na Ufaransa zimesema zingeweza kutuma vikosi nchini Ukraine kama sehemu ya makubaliano ya amani.

    Vance tangu wakati huo amesisitiza kwamba hakuzitaja "Uingereza wala Ufaransa," na kuongeza kwamba zote mbili "zimepigana kwa ujasiri sambamba na Marekani katika miaka 20 iliyopita, na zaidi."

    Hata hivyo, hakuelezea ni nchi gani alikuwa akizilenga.

    Katika chapisho la mitandao ya kijamii, aliongeza: "Lakini tuwe wa wazi: kuna nchi nyingi zinazojitolea (kwa siri au hadharani) kusaidia, ambazo hazina uzoefu wa vita wala vifaa vya kijeshi katika kufanya chochote cha maana."

    Hadi sasa, ni Uingereza na Ufaransa pekee ndizo zilizojitolea hadharani kupeleka vikosi kwa ajili ya kulinda makubaliano ya amani nchini Ukraine, ingawa Waziri Mkuu Sir Keir Starmer alisema awali kuwa "nchi kadhaa" zimekubali kutuma vikosi.

    Awali, maoni ya Vance yalikosolewa na wanasiasa wa upinzani wa Uingereza.

    Soma pia;

  3. Gaza kujengwa upya kwa dola 20b

    xyz

    Viongozi wa nchi za Kiarabu wanaokutana Cairo,Misri kujadili jinsi ya kujenga upya Gaza wameidhinisha mipango ya kujenga makaazi mapya laki mbili kwa gharama ya dola bilioni ishirini.

    Mpango huo hautawaondoa Wapalestina katika makazi yao.

    Mpango huo pia unataka uchaguzi ufanyike katika maeneo yote ya Palestina katika kipindi cha mwaka mmoja.

    Viongozi hao wameiomba jumuiya ya kimataifa na asasi za kifedha kujitolea kufadhili mpango huo. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa gharama ya kuujenga upya ukanda wa Gaza ni zaidi ya dola bilioni hamsini.

    Nchi za kiarabu zimekuwa zikikabiliwa na shinikizo la kuja na mapendekezo mbadala na yale yaliyotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump ya kutaka kudhibiti Gaza na kuhamisha Wapalestina wa Gaza hadi nchi jirani,pendekezo ambalo limepingwa vikali na nchi hizo za kiarabu na jumuiya ya kimataifa.

    Kundi la wanamgambo la Hamas limetaka viongozi hao wanaohudhuria mkutano huo wa kilele kuepusha kuondolewa kwa wapalestina wa Gaza.

    Hamas inasema inatumai kuwa viongozi wa kiarabu watakuwa na wajibu muhimu na utakaokomesha janga la kibinadamu lililosababishwa na kukaliwa kimabavu kwa ukanda wa Gaza.

    Marekani ilikuwa imependekeza Wagaza wahamishiwe nchi jirani za Misri na Jordan.

    Mkutano huo unajiri huku kukiwa na mkwamo kati ya Hamas na Israel kuhusu hatua inayofuata juu ya hatma ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili tarehe 19 Januari.

    Baada ya awamu ya kwanza ya makubaliano hayo kuisha mwishoni mwa juma lililopita bila ya muafaka ya namna gani yataendelezwa,Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza misaada ya kiutu izuiwe kuingia ukanda wa Gaza.

    Soma pia;

  4. EU yaikingia kifua Ukraine,baada ya Marekani kusitisha misaada

    XYZ

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Tume ya umoja wa ulaya EU imeweka wazi msimamo wake wa kuongeza matumizi katika sekta ya ulinzi hatua inayokuja wakati huu rais wa Marekani Donald Trump akisitisha misaada yote ya kijeshi kwa Ukraine kufuatia mzozo wake na rais Zelensky wiki iliyopita.

    Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen, alieleza mapema msimamo wa EU.

    "Tuko katika zama za kujiimarisha kiulinzi tena," aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kabla ya kuelezea mipango hiyo.

    Hotuba yake fupi inakuja kabla ya mkutano wa kilele na viongozi siku ya alhamisi ambapo mapendekezo hayo yatajadiliwa.

    Mpango huo unajumuisha mapendekezo matatu:

    Mosi kuruhusu nchi kuongeza matumizi ya ulinzi bila kuamsha mifumo ya Umoja wa Ulaya dhidi ya upungufu wa bajeti.

    Pili, €150bn katika mikopo kwa ajili ya uwekezaji wa ulinzi katika maeneo ambayo yanaweza kusaidia ulinzi wa EU kwa ujumla - kwa mfano, ulinzi wa anga na makombora, mifumo ya kupambana na ndege zisizokuwa na rubani, na uhamaji wa kijeshi. Chombo hiki kitasaidia kuunganisha mahitaji, na manunuzi ya pamoja yatapunguza gharama.

    Na tatu,kuruhusu nchi kuelekeza fedha zilizopangwa kwa ajili ya propramu ya sera zinazolenga kupunguza tofauti kati ya maeneo maskini na tajiri kwa matumizi ya ulinzi.

    Aidha Von der Leyen alisema mpango wake unaweza kukusanya jumla ya euro 800bn matumizi ya sekta ya ulinzi "kwa ajili ya Ulaya salama na thabiti".

    Mipango hiyo inaendelea wakati huu Urusi ikipongeza uamuzi wa Marekani kwa kile ilichodai kusitisha msaada wa silaha kwa Ukraine kunaweza kuwa mchango bora wa amani.

    Soma pia;

  5. Ugonjwa usiojulikana waua 53 DRC

    XYZ

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Takriban watu 53 wanaripotiwa kufariki kutokana na ugonjwa usiojulikana ndani ya siku moja tangu kugundulika kwa dalili za ugonjwa kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya demokrasi ya Congo.

    Shirika la afya duniani WHO linasema hatari ya ugonjwa huo kuenea kimataifa ni ndogo na linachunguza kwa kina kuhusu ugonjwa huo wa ajabu,na chanzo chake.

    Vifo hivyo vinajulikana kutokea kwa muda wa wiki mbili mwezi Februari, katika kijiji kimoja huko Basankusu, jimbo la Equateur.

    Hakuna uhusiano na virusi vya Ebola na Marburg.kwa mujibu wa matokeo ya vipimo vya maabara.

    Nusu ya wagonjwa walikuwa na malaria.

    Wataalam sasa wanachunguza ikiwa ni viashiria vya homa ya uti wa mgongo miongoni mwa watu ambao tayari walikuwa na maambukizi mengine kama vile malaria.

    Pia wamekusanya maji na sampuli nyingine za mazingira ili kuchunguza zaidi.

    Kifo cha mwisho kiliripotiwa tarehe 22 mwezi uliopita na hakuna ushahidi wa maambukizi zaidi katika kijiji hicho kilichoathiriwa.

    Awali vifo vilitokea miongoni mwa makundi yote ya umri lakini viliathiri zaidi wavulana na wanaume vijana.

    Zaidi ya watu elfu moja mia tatu wenye dalili za ugonjwa huo walitambuliwa.

    Soma pia;

  6. Rwanda yaishutumu Uingereza kwa kuvunja uaminifu

    fc

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza wakati huo Priti Patel (kushoto), na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Rwanda Vincent Biruta wakitia saini makubaliano katika Kituo cha Mikutano cha Kigali, Rwanda, Aprili 14, 2022.

    Serikali ya Rwanda imeishutumu Uingereza kwa kuvunja uaminifu na kuchukua hatua zisizo na msingi dhidi ya Kigali, na imeitaka serikali ya Uingereza iilipe Rwanda kiasi cha pauni milioni 50 chini ya mpango wa Ushirikiano juu ya Wahamiaji na Maendeleo ya Kiuchumi ambao haupo kwa sasa.

    Yolande Makolo, msemaji wa serikali ya Rwanda, ameikosoa Uingereza kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake, akisema Rwanda ilikubali kutochukua malipo hayo kwa kuzingatia uaminifu na imani iliyokuwepo kati ya mataifa hayo mawili.

    Hata hivyo, Makolo anasema imani hii imekiukwa kupitia hatua za hivi karibuni za Uingereza, ikiwa ni pamoja na kusimamisha misaada kwa Rwanda na kutoa matamshi mabaya Bungeni.

    "Uingereza iliitaka Rwanda kutodai malipo kwa kuzingatia uaminifu na nia njema iliyopo kati ya mataifa yetu mawili," Makolo alichapisha taarifa kwenye X siku ya Jumatatu, Machi 3.

    "Hata hivyo, Uingereza imevunja imani hii kupitia hatua zisizo na msingi za kuilazimisha Rwanda kuhatarisha usalama wa "taifa letu". Rwanda pia imelaani kile ilichosema ni maoni mabaya yaliyotolewa Bungeni na Lord Collins, Waziri wa Uingereza wa maswala ya Afrika.

    ’’Kwa hiyo tunafwatilia fedha hizi kwa mjibu wa sheria na makubaliano yaliyopo,’’ Makolo amesema.

    Mzozo kati ya nchi hizo mbili umeibuka baada ya Waziri wa Mambo ya Nje David Lammy kusitisha msaada wa Uingereza kwa Rwanda wiki iliyopita, akisema ni kutokana na Rwanda kuunga mkono kundi la waasi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Rwanda imekanusha vikali madai hayo, ikiishutumu Uingereza kwa kuendeleza hadithi za uongo na kudhoofisha juhudi za amani za kikanda.

    Malipo ya pauni milioni 50 yalikuwa sehemu ya makubaliano ya mpango wa wahamiaji, ambapo Uingereza ilipanga kutuma waomba hifadhi nchini Rwanda. Hata hivyo, serikali ya chama cha Labour, imeachana na mpango huo muda mfupi baada ya kuchukua madaraka.

    Pamoja na hayo, Rwanda inasema Uingereza haijakatisha rasmi mkataba huo, kumaanisha malipo hayo bado yanadaiwa kisheria.

    "Uingereza iliitaka Rwanda kutodai malipo hayo wakati inashughulikia kusitisha rasmi mpango huo," Makolo aliongeza. "Lakini wameshindwa kufanya hivyo, na kwa hatua zao za hivi majuzi, hatuna sababu ya kuendelea kusubiri."

    Pia unaweza kusoma:

  7. China yajibu mapigo ushuru mpya wa Trump

    fc

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mwonekano wa makontena na meli za mizigo kwenye bandari ya Wuhu, katika mkoa wa Anhui, China tarehe 4 Februari 2025

    Siku ya Jumanne China imelipiza kisasi ushuru mpya wa Marekani, kwa kutangaza ongezeko la 10% -15% la ushuru kwa bidhaa mbalimbali za kilimo na chakula za Marekani.

    Beijing pia imeyawekea makampuni ishirini na tano ya Marekani vikwazo kwa uuzaji wa nje na uwekezaji kwa misingi ya usalama wa taifa.

    Kumi kati ya makampuni haya 25 ya Marekani yamelengwa na China kwa kuiuzia silaha Taiwan, ambayo China inadai kuwa ni eneo lake.

    Ushuru huu wa kulipiza kisasi wa China umekuja wakati ambao ushuru wa 10% wa Rais wa Marekani Donald Trump umewekwa na utaanza kufanya kazi Machi 4 kwa bidhaa kutoka China. Hilo linafanya ushuru jumla kufikia 20%.

    Trump anasema ni kwa sababu China haichukui hatua za kuzuia mtiririko wa dawa za kulevya kutoka China zinazoingia Marekani.

    Wachambuzi wamesema Beijing bado ina matumaini ya kufikia makubaliano na utawala wa Trump, lakini ushuru wa kulipiza kisasi unatishia kuenea vita vya kibiashara kati ya mataifa hayo makubwa ya kiuchumi.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Waislamu wanaokula hadharani wakati wa Ramadhan watiwa mbaroni Nigeria

    Polisi wa Kiislamu, au Hisbah, wanasema kukamatwa kwa watu hao kutaendelea katika kipindi chote cha Ramadhani

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Polisi wa Kiislamu, au Hisbah, wanasema kukamatwa kwa watu hao kutaendelea katika kipindi chote cha Ramadhani

    Maafisa wa usalama wa Kiislamu kaskazini mwa Nigeria katika jimbo la Kano wamewatia nguvuni Waislamu wanaonekana wakila na kunywa hadharani, pamoja na wale wanaouza chakula mchana ilhali wanapaswa kufunga kuanzia machweo hadi jioni.

    Naibu Kamanda wa kikosi cha Hisbah, Mujahid Aminudeen ameiambia BBC kuwa takriban watu 20 wamekamatwa kwa kutofunga na watano kwa kuuza chakula mchana na operesheni hiyo itaendelea hadi Ramadhan ikamilike.

    ‘’Ni muhimu ijulikane kuwa hatulengi wasio Waislamu,’’ anasema.

    "Ni jambo la kuvunja moyo wakati mwezi mtukufu unaohitaji watu wafunge, watu wanaonekana wakibugia na kula mbele za umma. Hilo hatutakubaliana nalo ndio maana tumekwenda kuwakamata wote,’’ anasema.

    Mujahid pia ameweka wazi kuwa watu hao waliokamatwa watasomewa mashtaka katika mahakama ya sharia na wataadhibiwa vilivyo.

    Afisa huyo pia anasema mara nyingi hupatiwa fununu kuhusu wasiofunga.

    Pia amethibitisha kukamatwa kwa wale wanaokutwa wamenyoa ‘’mtindo usiofaa,’’ waliovaa kaptula zinazoonyesha magoti yao na magari yanayochanganya jinsia ya kiume na kike.

    Mwaka jana wakati wa Ramadhan waliokamatwa waliachiliwa baada ya kuahidi kufunga funga walizoziacha na familia zao kutoa hakikisho kuwa watawafuatilia utekelezwaji wa ahadi zao.

    Miongo miwili iliyopita sheria ya Kiislamu ilibuniwa na kuanza kutumika katika majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria ambayo wakaazi wengi ni waumini wa dini ya Kiislamu.

    Wakati wa Ramadhan, Waislamu wanatakiwa kufunga kula na kunywa na kujikurubisha kwa Allah kuanzia asubuhi hadi jioni.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Canada yaiwekea Rwanda vikwazo vya kiuchumi na kisiasa

    vc

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Canada imetangaza vikwazo vya kiuchumi na kisiasa dhidi ya Rwanda, ikisema vikosi vyake vinalisaidia kundi la M23 nchini DR Congo, na hivyo kukandamiza "uhuru" wa nchi nyingine.

    Serikali ya Canada inasema inalaani "mauaji makubwa mashariki mwa DRC," na mashambulizi dhidi ya raia, wakimbizi, vikosi vya Umoja wa Mataifa na kikanda, pamoja na "mauaji ya watu wengi na utekaji nyara."

    Canada inasema "kutokana na kuhusika kwa Rwanda" Mashariki mwa Congo, imechukua maamuzi ya; kuacha kutoa leseni za kuuza huduma za teknolojia nchini Rwanda, kusitisha ushirikiano kati ya serikali ya Canada na Rwanda katika masuala ya biashara, na sekta binafsi. Vilevile Canada itaacha kushiriki katika shughuli za kimataifa zinazoandaliwa na Rwanda.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda imesema matamshi ya Canada ikiwa ni pamoja na "tuhuma za mauaji, Rwanda itaitaka Canada kutoa maelezo na hilo.

    Rwanda inasema Canada haiwezi kusema inaunga mkono juhudi za kikanda za kufikia amani "huku ikitoa kila aina ya shutuma dhidi ya Rwanda, na inashindwa kuiwajibisha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa mashambulizi dhidi ya raia wake wa kabila la Banyamulenge huko Kivu Kusini na kuongeza kuwa hatua za Canada dhidi ya Rwanda "hazitasuluhisha mzozo."

    Canada ilitangaza vikwazo dhidi ya Rwanda baada ya Ubelgiji, Uingereza na Marekani kumuwekea vikwazo Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mahusiano ya Kikanda, Jenerali Mstaafu James Kabarebe.

    Nchi za Magharibi, Umoja wa Mataifa na serikali ya Kinshasa zinaishutumu Rwanda kwa kutuma wanajeshi wake nchini Congo kusaidia kundi la M23 ambalo sasa linadhibiti miji ya Goma na Bukavu baada ya mapigano makali mwishoni mwa mwezi wa kwanza na wa pili.

    Rwanda imekanusha kutuma wanajeshi wake DR Congo, ikisema Rwanda imechukua hatua za kulinda mipaka yake kwa sababu usalama wa nchi hiyo unatishiwa na ushirikiano wa kundi la waasi la Wahutu la FDLR na vikosi vya serikali ya Congo.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Wanajeshi wa Congo wafikishwa kizimbani kwa tuhuma za ubakaji na mauaji

    j

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (FARDC) waliotumwa kupambana na waasi wa M23 wakiwa katika ya kukimbia vita na kufanya uhalifu dhidi ya raia

    Wanajeshi wa Congo wakiwa na mchanganyiko wa nguo za kijeshi na za kawaida, walijaa kwenye kanisa wiki iliyopita kujibu mashtaka ya uhalifu ikiwa ni pamoja na ubakaji na mauaji yanayodaiwa kufanywa walipokuwa wakikimbia waasi wa M23.

    Kauli zao wakati wa kesi hiyo katika mahakama ya kijeshi zinaonyesha kushindwa kwa jeshi ambalo sasa limepoteza maeneo mengi mashariki mwa Congo kutokana na wapiganaji wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kusonga mbele.

    Machafuko ya wiki chache zilizopita yamezidi kuzorotesha jeshi dhaifu la Congo, na kuongeza hatari za vitendo vya dhuluma dhidi ya raia, inasema hati ya siri ya Umoja wa Mataifa iliyoonekana na Reuters.

    Wakati serikali ya Rais Felix Tshisekedi akipongeza juhudi za kuajiri wanajeshi wapya na kupata silaha mpya, ushuhuda kutoka kwa maafisa wakuu wanasema, hilo halina maana kwa askari walio mstari wa mbele, ambao wanalipwa ujira mdogo na wasio na vifaa vya kutosha.

    "Tunakosolewa lakini tunateseka kama watu wengine," alisema kanali mmoja ambaye wanajeshi wake wamepigana katika jimbo la Kivu Kusini.

    Katika kesi za Musienene wiki iliyopita na katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, Bukavu mapema mwezi Februari, waendesha mashtaka wa kijeshi walisikiliza mashtaka yakiwemo wizi, uporaji, unyang'anyi na kupoteza silaha.

    Wengi wa washtakiwa walikiri kuwa baadhi ya askari walifanya uhalifu huo lakini wao wenyewe wakakanusha kuhusika.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Wabunge wa Ghana wawasilisha mswada wa kuongeza adhabu kwa LGBTQ

    k

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo akihutubia bunge mjini Accra, Ghana, Machi 30, 2022.

    Wabunge watatu wameliambia shirika la habari la Reuters, kuwa Wabunge wa Ghana wamewasilisha tena mswada dhidi ya LGBTQ, baada ya jaribio la awali la kushindikana kwa sababu ya changamoto za kisheria.

    Vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kwa sasa vinaadhibiwa hadi miaka mitatu jela nchini Ghana. Mswada huo utaongeza adhabu hadi miaka mitano na pia kuweka kifungo cha jela kwa "kuhamasisha kwa makusudi, ufadhili au usaidizi wa shughuli za LGBTQ+."

    Bunge la Ghana liliidhinisha mswada huo Februari 2024 lakini Rais wa wakati huo Nana Akufo-Addo hakuutia saini kabla ya muhula wake kumalizika na John Dramani Mahama kuingia madarakani Januari.

    Mswada wowote uliopitishwa na bunge lazima uende kwa rais ili kutiwa saini na kuwa sheria.

    Wabunge wa chama tawala Samuel Nartey George na Emmanuel Kwasi Bedzrah na mbunge wa upinzani John Ntim Fordjour wameiambia Reuters, mswada huo huo umewasilishwa tena bungeni Februari 25, na wabunge 10.

    Va-Bene Elikem Fiatsi, mwanaharakati wa Ghana wa LGBTQ, ameiambia Reuters, kuletwa upya kwa muswada huo "kunavunja moyo " lakini harakati za kuunga mkono LGBTQ zitaendelea.

    Mwaka jana wizara ya fedha ya Ghana ilionya kwamba mswada huo, ikiwa utatiwa saini kuwa sheria, unaweza kuhatarisha dola bilioni 3.8 katika ufadhili wa Benki ya Dunia na kukwamisha mkopo wa dola bilioni 3 kutoka Monetary Fund.

  12. Trump kuzitoza ushuru bidhaa za Mexico na Canada kuanzia Jumanne

    Trump anasema Mexico na Canada zitalazimika kujenga viwanda vyao nchini Marekani.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Trump anasema Mexico na Canada zitalazimika kujenga viwanda vyao nchini Marekani.

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuendelea na mpango wake kutoza ushuru wa asilimia 25% kwa bidhaa zinazotoka Canada na Mexico zinazoingizwa Marekani baada ya muda wa makubaliano kumalizika.

    "Muda wa kuelewana haupo tena, hakuna kitakachowasaidia Mexico na Canada,’’ Trump amesema akiwa White House siku ya Jumatatu. "Ushuru bado upo. Na utaanza kutekelezwa kuanzia Jumanne.’’

    Kwa upande wa Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau amejibu hatua ya Trump kwa kutangaza kutoza ushuru wa asilimia 25% kwa bidhaa za gharama ya dola bilioni 30 zinazotoka Marekani.

    Huko Mexico, Rais Claudia Sheinbaum amesema kuwa taifa lake linapaswa ‘’kuheshimiwa."

    Washington pia inatarajiwa kuongeza ushuru mwingine wa asilimia 10% kwa bidhaa zinazotoka China na kuzifanya nchi hizo washirika watatu wakuu wa biashara wa Marekani kuwa na ushuru wa juu zaidi.

    Rais wa Marekani alieleza ataweka ushuru kwa nchi zote tatu mapema mwaka huu kujibu kile anachoelezea kama "mtiririko usiokubalika" wa dawa haramu na wahamiaji wasio na vibali nchini Marekani.

    Mataifa ambayo yameongezewa ushuru kwa bidhaa zao yameapa kuungana dhidi ya Marekani na kuibua wasiwasi wa vita vya kiuchumi ambavyo huenda vikaathiri masoko ulimwenguni.

    Soko la hisa la Marekani liliporomoka baada ya kuthibitishwa kwa hatua ambazo Trump amekuwa akitishia tangu aingie madarakani kama Rais mwezi Januari.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Watoto wenye umri wa mwaka mmoja ni miongoni mwa waliobakwa katika vita vya Sudan - UN

    fc

    Chanzo cha picha, UNICEF

    Maelezo ya picha, Hala (sio jina lake halisi) ni mmoja wa wasichana wengi waliobakwa tangu vita vianze

    Watu wenye silaha wanabaka na kuwanyanyasa kingono watoto wenye umri hadi mwaka mmoja katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, linasema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef.

    Unyanyasaji mkubwa wa kingono wa watu wengi umerekodiwa na kutumiwa kama silaha ya vita katika mzozo huo wa karibu miaka miwili.

    Theluthi moja ya waathiriwa ni wavulana, ambao kwa kawaida wanakabiliwa na "changamoto” katika kuripoti uhalifu kama huo na kutafuta msaada wanaohitaji.

    Unicef ​​i nasema, ingawa kesi 221 za ubakaji dhidi ya watoto zimeripotiwa rasmi tangu kuanza kwa 2024, idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi.

    Sudan ni nchi yenye uhafidhina katika jamii na hilo huzuia waathirika na familia zao kuzungumza juu ya ubakaji, kwa hofu ya kuadhibiwa na makundi yenye silaha.

    Unicef inasema waathiriwa 16 wa unyanyasaji wa kingono walikuwa na umri wa chini ya miaka mitano, wakiwemo watoto wachanga wanne.

    Unicef ​​haisemi ni nani anahusika, lakini uchunguzi mwingine wa Umoja wa Mataifa umewanyooshea kidole wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), inasema wapiganaji wa RSF walikuwa na mtindo wa kutumia unyanyasaji wa kijinsia kuwatisha raia na kukandamiza upinzani dhidi ya harakati zao.

    RSF, ambayo inapigana vita dhidi ya washirika wake wa zamani, vikosi vya Wanajeshi wa Sudan, imekanusha kufanya makosa yoyote.

    Kulingana na ushahidi uliowasilishwa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu, wahanga katika ngome za RSF huko Darfur mara nyingi walilengwa kwa sababu walikuwa Waafrika weusi na si Waarabu, kwa lengo la kuwafukuza kutoka Sudan.

    Kuna maelezo ya kutisha katika ripoti ya Unicef kama yale ya Omnia.

    "Baada ya saa tisa usiku, mtu alifungua mlango, akiwa amebeba kiboko, akachagua msichana mmoja, na kumpeleka kwenye chumba kingine. Nilisikia msichana mdogo akilia na kupiga mayowe. Walikuwa wakimbaka," ameeleza Omnia (si jina lake halisi), mwanamke mtu mzima aliyenusurika baada ya kushikiliwa na wanaume wenye silaha katika chumba na wanawake wengine na wasichana.

    "Kila mara walipombaka msichana huyu alikuwa akirudi akiwa ametapakaa damu. Ni mtoto mdogo tu. Wanawaachilia wasichana hawa alfajiri, na wanarudi wakiwa hawajitambui. Kila mmoja wao analia na kuongea ovyo. Katika siku 19 nilizokaa huko, nilifikia hatua ambayo nilitaka kukatisha maisha yangu."

    Idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita imewafanya wanawake na watoto kuwa katika hatari zaidi ya kushambuliwa – Umoja wa Mataifa unasema, wasichana watatu kati ya wanne wa umri wa kwenda shule hawaendi shule.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Papa Francis akumbwa na tatizo la kushindwa kupumua mara mbili

    efd

    Chanzo cha picha, Reuters

    Papa Francis yuko macho baada ya kukumbwa na matukio mawili ya "kushindwa kupumua" siku ya Jumatatu alasiri, imesema Vatican.

    Madaktari walilazimika kuingilia kati ili kuondoa kamasi kwenye mapafu ya Papa, imesema taarifa kutoka serikali kuu ya Vatican ya Holy See, ingawa wanasema alikuwa anajitambua wakati wote.

    Papa mwenye umri wa miaka 88 ameanza tena matumizi ya mashine ya kupumulia ili kumsaidia kupumua, lakini bado yuko "macho, anajitambua na anatoa ushirikiano," imesema Vatican.

    Hii ni mara ya tatu hali ya Papa kubadilika ghafla tangu alipolazwa hospitalini siku 18 zilizopita kutokana na nimonia. Siku ya Ijumaa, Papa Francis alipata shida ya kupumua iliyohusisha kutapika, ilisema Vatican.

    Mamia ya Wakatoliki walikusanyika nje katika uwanja wa St Peter's Square Jumatatu jioni kumwombea Papa, wengi wao wakiwa wamebeba rozari.

    Papa alilazwa hospitalini tarehe 14 Februari baada ya kupata matatizo ya kupumua kwa siku kadhaa. Alitibiwa mara ya kwanza kikohozi kabla ya kugunduliwa na nimonia katika mapafu yote mawili.

    Vyanzo kutoka Vatikan vinasisitiza kwamba hali ya Papa bado ni ngumu na madaktari wake wako kwenye uangalifu.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Waasi wa M23 wawateka nyara wagonjwa 130 kutoka hospitalini - UN

    c

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Waasi wa M23 wakiwa katika gari wakati wa kuwasindikiza waasi wa FDLR waliotekwa (hawapo pichani) kuelekea Rwanda kupitia kivuko cha mpaka wa Goma-Gisenyi Grande Barrier, Machi 1, 2025.

    Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wamefanya mashambulizi Mashariki mwa DR Congo na kuwateka nyara takribani wagonjwa na waliojeruhiwa 130 kutoka katika hospitali mbili za mji wa Goma wiki iliyopita, umesema Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu.

    Wapiganaji wa M23 walivamia Hospitali ya CBCA Ndosho na Hospitali ya Heal Africa usiku wa Februari 28, na kuchukua wagonjwa 116 na 15, amesema msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani.

    Watu hao waliotekwa nyara wanashukiwa kuwa ni wanajeshi wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo au wanamgambo wanaoiunga mkono serikali wanaojulikana kwa jina la Wazalendo.

    "Inasikitisha sana kwamba M23 inawanyakua wagonjwa katika vitanda vya hospitali kupitia uvamizi ulioratibiwa na kuwaweka katika maeneo yasiyojulikana," amesema Shamdasani, akitaka waachiliwe mara moja.

    Wasemaji wa M23, Willy Ngoma na Lawrence Kanyuka Kingston hawakujibu maswali ya Reuters kuhusu tukio hilo.

    Waasi wa M23 wanaoongozwa na Watutsi waliingia katika mji wa Goma mwishoni mwa Januari na tangu wakati huo wamepiga hatua kubwa kuelekea mashariki mwa Congo, wakiteka maeneo na kushikilia maeneo ya madini ya thamani.

    Takriban watu 7,000 wameuawa mashariki mwa Congo tangu Januari na karibu watu nusu milioni wameachwa bila makazi baada ya kambi 90 za wakimbizi kuharibiwa katika mapigano hayo, kulingana na serikali.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Trump asitisha misaada yote ya kijeshi ya Marekani kwa Ukraine

    fdc

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amesitisha misaada yote ya kijeshi kwa Ukraine kufuatia mzozo wake na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy wiki iliyopita, amesema afisa wa Ikulu ya White House.

    "Rais Trump amekuwa wazi kuwa anataka amani. Tunataka pia washirika wetu wajitolee kwa lengo hilo. Tunasitisha misaada yetu na kuikagua ili kuhakikisha inachangia katika suluhu," alisema afisa huyo siku ya Jumatatu, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Ikulu ya White House haijaeleza aina na kiasi cha misaada itakayo sitishwa au muda wa kusitisha utadumu kwa kipindi gani.

    Pentagon pia haijatoa maelezo zaidi.

    Ofisi ya Zelenskiy haijatoa majibu kwa maswali ya Reuters kupitia Ubalozi wa Ukraine huko Washington.

    Hatua hiyo imekuja baada ya Trump kupindua sera za Marekani kuhusu Ukraine na Urusi alipoingia madarakani mwezi Januari, na kuchukua msimamo wa urafiki zaidi kwa Moscow.

    Haya yanakuja baada ya mabishano makali kati ya Trump na Zelenskiy katika Ikulu ya White House siku ya Ijumaa ambapo Trump alimtuhumu kwa kutoshukuru vya kutosha kwa uungaji mkono wa Washington katika vita na Urusi.

    Pia unaweza kusoma:

  17. Hujambo na karibu

    Nikukaribishe katika taarifa zetu za moja kwa moja, leo Jumanne tarehe 4 Machi 2025