Kwa nini Waislamu wa Marekani walikataa kufuturu na Rais Biden?

Chanzo cha picha, Reuters
Mwaka jana, Rais Joe Biden hakuweza kusoma na kumaliza hotuba yake kusherehekea Ramadhani Ikulu ya White House kabla ya mtu kusema "tunakupenda." Mamia ya Waislamu walikuwepo kusherehekea kukamilika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hakuna matukio ya furaha kama hayo katika sherehe za kuuaga mwei wa Ramadhani mwaka huu.
Waislamu wa Marekani mwaka huu wamekasirishwa na hatua ya Rais Joe Biden kuiunga mkono Israel tangu kuanza kwa vita vya Gaza mnamo Oktoba 7 mwaka jana.
Kwa mujibu wa BBC Somalia Ikulu ya White House ilichagua kuandaa karamu ndogo ya iftar Jumanne jioni lakini watu pekee waliohudhuria walikuwa watu wanaofanya kazi katika utawala wake.
"Tunaishi katika ulimwengu tofauti, kwa kweli ni ndoto, na ni jambo la kusikitisha," alisema Wa'el AlZayat, kiongozi wa Emgage, shirika linalotetea Waislamu.
Alzayat alihudhuria hafla kama hiyo mwaka jana, lakini alikataa mwaliko wa futari ya Biden mwaka huu, akisema "haifai kuwa na sherehe kama hiyo wakati kuna njaa huko Gaza."
Alinukuliwa na BBC Somali akisema kuwa Ikulu ya White House inahitajika kurekebisha mipango yake. Alzayat alisema anaamini siku moja haitoshi kujiandaa kwa fursa ya kugeuza mawazo ya Biden kutoka kwenye mzozo huo.
"Sidhani kama mtindo huo utajitolea kwa mjadala halisi wa kisiasa," aliongeza.
Kukataa kufuturu au hata kukusanyika pamoja ni ushahidi mpya wa kuvunjika kwa uhusiano kati ya utawala wa Biden na jamii ya Waislamu miezi sita baada ya kuzuka kwa mzozo kati ya Israel na Hamas.

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa mujibu wa BBC Somali ,Rais huyo wa chama cha Democratic alipoingia madarakani miaka mitatu iliyopita, viongozi wengi wa Kiislamu walitaka kumuunga mkono kwani walikuwa wakitaka kuondolewa kwa Trump.
Lakini Wanademokrasia wanahofia kwamba hatua ya Waislamu kutomuunga mkono Biden kunaweza kumzuia kurudi Ikulu.
Uchaguzi wa mwaka huu unaweza kutegemea idadi ndogo ya majimbo yenye Waislamu wengi kama vile Michigan.
Alzayat, anafikiri kwamba hakuna tofauti kubwa kati ya watu hao wawili, akimaanisha Biden na Trump.
Aliongeza, "Si vizuri kuwaambia watu kwamba Donald Trump atakuwa mbaya zaidi."
Viongozi kadhaa wa Kiislamu walihudhuria mkutano wa Jumanne na Biden, Makamu wa Rais Kamala Harris, maafisa wa serikali ya Kiislamu na viongozi wa usalama wa kitaifa.

Chanzo cha picha, social
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya Iftar, msemaji wa White House Jean-Pierre alisema "rais ataendeleza utamaduni wake wa kuheshimu jamii ya Waislamu wakati wa Ramadhani."
Mkutano wa Iftar katika Ikulu ya White House haukuwa wazi hata kwa waandishi wa habari kama ilivyokuwa mwaka jana.
Nihad Awad, mkurugenzi mtendaji wa Baraza la Uhusiano wa Marekani na Kiislamu, alisema aliwahimiza viongozi wengine wa Kiislamu kukataa mialiko ya Ikulu ya Marekani iwapo wataipokea.
Ujumbe ulioshirikiwa ulikuwa "hadi atakapotoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, hakutakuwa na mkutano naye au wawakilishi wake."
“Ninaamini kuwa rais ndiye mtu pekee duniani anayeweza kuzuia hili, anaweza kuchukua simu na kumwambia Benjamin Netanyahu kwa umakini, hakuna silaha tena, acha tu, Benjamin Netanyahu hatakuwa na la kufanya zaidi ya kufanya hivyo’’, alisema Nihad Awad.
Vita hivyo vilianza Oktoba 7 wakati Hamas ilipofanya shambulizi la kushtukiza lililoua Waisraeli 1,200.
Katika kujibu, Israel imeua takriban Wapalestina 33,000.
Utawala wa Biden umeendelea kuidhinisha uuzaji wa silaha kwa Israeli licha ya rais huyo kuwataka viongozi wa Israeli kuwa waangalifu zaidi dhidi ya vifo vya raia na kuwahimiza kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu kuingia Gaza.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












