Msemaji wa jeshi Hamas Abu Obeida auawa

Chanzo cha picha, Getty Images
Kundi la Kipalestina la Hamas limethibitisha kuwa msemaji wake wa kijeshi, Abu Obeida, pamoja na kiongozi wa zamani wa Gaza, Mohammed Sinwar, waliuawa na jeshi la Israel.
Kundi hilo kupitia brigedi ya Qassam ilitangaza taarifa hiyo ya kuthibitisha hilo Jumatatu. Pia zilithibitisha vifo vya Mohammed Shabanah, kiongozi wa tawi la Rafah, pamoja na viongozi wengine wawili, Hakam al-Issi na Raed Saad.
Jeshi la Israeli lilisema mwezi Mei kwamba liliwaua Sinwar, kaka mdogo wa kiongozi wa zamani wa Hamas, Yahya Sinwar. Miezi mitatu baadaye, lilidai pia kwamba lilimuua Abu Obeida.
Hamas imethibitisha kuwa jina halisi la Abu Obeida lilikuwa Huthaifa al-Kahlout.
Taarifa ya mwisho ya Abu Obeida ilikuwa mwanzoni mwa Septemba wakati Israel ilipoanza hatua za awali za shambulio jipya la kijeshi kwenye Jiji la Gaza, ikitangaza eneo hilo kama kizuizi cha mapambano huku ikiharibu mamia ya majengo ya makazi na mamilioni ya Wapalestina walikimbia makazi yao.
Abu Obeida alikuwa sauti muhimu ya Hamas huko Gaza, akitoa taarifa kuhusu hali ya mapambano, ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano, na makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya Wapalestina na Israel mwanzoni mwa mwaka huu wakati wa mapumziko ya muda mfupi ya amani, ambayo Israel iliyavunja.
Sinwar na Abu Obeida ni wawakilishi wa hivi karibuni wa Hamas waliothibitishwa kuuawa na Israel katika miaka miwili iliyopita, ikiwa ni pamoja na viongozi wengi wa ngazi ya juu wa kijeshi na kisiasa wa Hamas, kama vile kiongozi wa kisiasa Yahya Sinwar; kamanda wa kijeshi Mohammed Deif, mmoja wa waanzilishi wa Brigedi za Qassam miaka ya 1990; na kiongozi wa kisiasa Ismail Haniyeh, aliyeuawa katika mji mkuu wa Iran, Tehran.














