Watu 12 wameuawa kwa kupigwa risasi, shambulio lililolenga jamii ya Wayahudi Australia

Kamishna wa Polisi Mal Lanyon alitangaza rasmi kuwa ni "tukio la kigaidi", akiongeza kuwa kulikuwa na zaidi ya watu 1,000 kwenye eneo hilo, wengi wakisherehekea sikukuu ya Kiyahudi ya Hanukkah.

Muhtasari

  • Israel yamlenga afisa mkuu wa Hamas katika shambulio baya la Gaza

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Rais wa Israel asema ufyatuaji risasi ni “shambulio la kikatili dhidi ya Wayahudi”

    Isaac Herzog

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Israel, Isaac Herzog, ametoa tamko kufuatia tukio la ufyatuaji risasi lililotokea Bondi Australia , akilieleza kuwa ni “shambulio la kikatili sana dhidi ya Wayahudi.”

    Inafahamika kuwa wakati tukio hilo linatokea, kulikuwa na hafla ya kuadhimisha siku ya kwanza ya sikukuu ya Kiyahudi ya Hanukkah katika ufukwe wa Bondi.

    Hadi sasa, haijabainika wazi nia ya washambuliaji.

    “Dada na kaka zetu huko Sydney wameshambuliwa na magaidi waovu katika shambulio la kikatili sana dhidi ya Wayahudi waliokuwa wamekusanyika kuwasha mshumaa wa kwanza wa Hanukkah katika ufukwe wa Bondi,” amesema Herzog.

  2. Tunachokifahamu kufikia sasa kuhusu shambulizi la kigaidi kwenye ufukwe wa Bondi Australia

    Waziri Mkuu wa New South Wales Chris Minns (kushoto) na Kamishna wa Polisi Mal Lanyon walitoa taarifa katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo.

    Chanzo cha picha, DEAN LEWINS/EPA/Shutterstock

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa New South Wales Chris Minns (kushoto) na Kamishna wa Polisi Mal Lanyon walitoa taarifa katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo.

    Idadi ya vifo imeongezeka na kufikia 12, kwa mujibu wa Waziri Mkuu Chris Minns, ambaye amesema shambulio hilo lililenga moja kwa moja jamii ya Wayahudi wa Sydney.

    Kamishna wa Polisi, Mal Lanyon, ametangaza rasmi tukio hilo kuwa shambulio la kigaidi, akisema kulikuwa na zaidi ya watu 1,000 eneo la tukio, wengi wao wakisherehekea sikukuu ya Kiyahudi ya Hanukkah.

    Watu 29 wamepelekwa hospitalini, akiwemo mtoto mmoja.

    Miongoni mwa waliojeruhiwa ni maafisa wawili wa polisi, ambao hali zao ni mahututi, na walifanyiwa upasuaji wa dharura.

    Kuhusu washambuliaji wawili waliotajwa, mmoja amefariki dunia, na mwingine yuko hospitalini akiwa katika hali mbaya, amesema Lanyon.

    Polisi hawajatoa taarifa za kina kuhusu washambuliaji kwa sasa, lakini wamesema wanachunguza uwezekano wa kuwepo kwa mshambuliaji wa tatu.

    Polisi wamegundua bomu la kujitengenezea ndani ya gari linalohusishwa na mshambuliaji aliyefariki.

    Kikosi cha kitaalamu cha kutegua mabomu kiko eneo la Campbell Parade, Bondi.

    Chris Minns amempongeza mwanaume aliyerekodiwa kwenye video akimkabili mshambuliaji mmoja, kumuangusha na kumnyang’anya silaha yake, hatua iliyosaidia kuzuia maaafa zaidi.

  3. Mkuu wa Umoja wa Mataifa ashtushwa na “shambulio la kikatili dhidi ya familia za Kiyahudi”

    Antonio Guterres

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema ameshtushwa sana na tukio la ufyatuaji risasi lililotokea Bondi Beach.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, amesema: “Nimeshtushwa sana na ninalaani shambulio hili la kikatili lililosababisha vifo dhidi ya familia za Kiyahudi zilizokuwa zimekusanyika mjini Sydney kusherehekea sikukuu ya Hannukah.”

    Ameongeza kuwa: “Moyo wangu uko pamoja na Wayahudi kote duniani katika siku hii ya kwanza ya Hannukah, sikukuu inayoadhimisha muujiza wa amani na mwanga unaoshinda giza.”

  4. Msako waendelea baada ya watu wawili kuuawa kwa kupigwa risasi katika Chuo Kikuu cha Brown

    Mshambuliaji huyo alifyatua risasi darasani

    Msako unaendelea baada ya wanafunzi wawili kuuawa na watu wengine tisa kujeruhiwa katika ufyatuaji risasi mkubwa katika Chuo Kikuu cha Brown huko Providence, Rhode Island.

    Mshambuliaji huyo alifyatua risasi darasani karibu saa 16:00 kwa saa za huko (21:00 GMT) siku ya Jumamosi, katika jengo ambalo mitihani ilikuwa ikifanyika.

    Chuo kikuu, kimojawapo kikongwe na chenye hadhi kubwa zaidi nchini Marekani, kiliwekwa kizuizini huku polisi wakimtafuta mshambuliaji huyo, ambaye bado hajakamatwa.

    Wanafunzi katika sehemu za chuo kikuu wanaendelea kuambiwa wajikinge mahali hapo hadi polisi watakapowasindikiza kutoka eneo hilo.

    Maafisa kutoka Hospitali ya Rhode Island walisema wengi wa waliojeruhiwa wako katika hali "mahututi lakini imara".

  5. Belarus yawaachilia huru wafungwa 123 huku Marekani ikiondoa vikwazo

    Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Ales Bialiatski awasili Vilnius

    Chanzo cha picha, Reuters

    Belarus imewaachilia huru wafungwa 123, akiwemo mwanaharakati maarufu wa upinzani Maria Kolesnikova, baada ya Marekani kukubali kuondoa vikwazo dhidi ya nchi hiyo.

    Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Ales Bialiatski pia ni miongoni mwa wale walioachiliwa huru kufuatia mazungumzo huko Minsk na mjumbe maalum wa Rais Donald Trump wa Marekani kwa Belarus, John Coale.

    Marekani imekubali kuondoa vikwazo dhidi ya potashi, kiungo muhimu katika mbolea na usafirishaji muhimu kwa Belarus, ambayo ni mshirika wa karibu wa Urusi.

    Coale alisema: "KadIri uhusiano kati ya nchi hizo mbili unavyozidi kurejea katika hali ya kawaida, vikwazo zaidi na zaidi vitaondolewa." Kiongozi wa Belarusi Alexander Lukashenko hatambuliwi kama rais na EU.

    Kolesnikova amekuwa gerezani tangu 2020, muda mwingi akiwa peke yake.

    Akizungumza baada ya kuachiliwa kwake, alielezea "hisia ya furaha isiyomithilika" kwa kuweza kuwaona na kuwakumbatia watu "wapendwa wangu". Alisema:

    "Ni furaha kubwa kuona machweo ya kwanza ya uhuru wangu, uzuri wa ajabu. "Lakini pia tunawafikiria wale ambao bado hawajawa huru.

    Ninasubiri wakati ambapo sote tunaweza kukumbatiana, wakati wote watakapokuwa huru." Kolesnikova alikabidhiwa Ukraine pamoja na wafungwa wengine 113, kulingana na Makao Makuu ya Uratibu wa Matibabu ya Wafungwa wa Vita ya Kyiv.

    Katika taarifa kwenye Telegram, Ukraine ilisema kwamba baada ya kupokea msaada wa kimatibabu unaohitajika, wafungwa hao watasafirishwa hadi Poland na Lithuania.

  6. Israel yamlenga afisa mkuu wa Hamas katika shambulio baya la Gaza

    Athari za mashambulizi

    Chanzo cha picha, Reut

    Israel ilisema ilimuua kamanda mkuu wa Hamas siku ya Jumamosi katika shambulio dhidi ya gari ndani ya Gaza.

    Katika taarifa ya pamoja, shirika la kijeshi na usalama la Israeli Shin Bet lilitangaza kuwa "limemuua" Raed Saad, mkuu wa uzalishaji wa silaha wa tawi la kijeshi la Hamas, Brigedi za Qassam, katika jiji la Gaza.

    Saad alikuwa akichukuliwa kama mmoja wa makamanda mashuhuri wa Qassam na aliongoza brigedi kadhaa wakati wa mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 dhidi ya jamii za Israel mashariki mwa Jiji la Gaza.

    Msemaji wa Ulinzi wa Raia anayeongozwa na Hamas, Mahmoud Basal, aliiambia BBC kwamba watu wanne waliuawa katika shambulio hilo. Alisema wapita njia wengi pia walijeruhiwa na mlipuko huo.

    Afisa wa Hamas wa eneo hilo huko Gaza aliiambia BBC kwamba shambulio hilo pia lilimuua msaidizi wa Saad na afisa mwingine wa cheo cha chini aliyetambuliwa kama Abu Imad al-Laban.

    Taarifa ya pamoja ya IDF na ISA iliongeza kuwa Saad alikuwa "anahusika na vifo vya wanajeshi wengi" waliouawa katika Ukanda wa Gaza kutokana na vifaa vya kulipuka.

    Saad anaaminika kuwa mwanachama wa baraza jipya la kijeshi la uongozi lenye wanachama watano lililoanzishwa tangu kusitisha mapigano kulipoanza Oktoba.

    Unaweza kusoma;

  7. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu leo