Yaelewe mazoezi ya kijeshi ya Taiwan ya kujilinda dhidi ya China

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Tessa Wong
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mazoezi ya kijeshi ya kila mwaka ya Taiwan, Han Kuang, yameanza Jumatano ya wiki hii, kisiwa hicho kinaimarisha ulinzi wake dhidi ya uvamizi wowote kutoka China.
Mazoezi ya Han Kuang yatadumu kwa siku 10, ni muda mrefu zaidi, mara mbili ya muda wa mazoezi ya mwaka jana.
Yanalenga kuutayarisha umma wa Taiwan kwa shambulio lolote, lakini pia yanakusudiwa kuonyesha hadharani ulinzi wa kisiwa hicho na kutuma salamu za wazi kwa Beijing.
China inadai Taiwan inayojitawala, ni eneo lake na imeapa "kuiunganisha tena na China" siku moja, na haijaondoa uwezekano wa matumizi ya nguvu kufanikisha hilo. Na hilo limezua hofu ya kutokea mzozo mkubwa hasa kwa Marekani, mshirika mkuu wa Taiwan.
Han Kuang ni nini?
Hufanyika kila mwaka tangu 1984, mazoezi ya Han Kuang hushirikisha maelfu ya wanajeshi wanaoshiriki katika mazoezi makubwa ya ardhini, baharini na angani ambayo huonyesha zana za hivi punde zaidi za kijeshi za Taiwan.
Mwaka huu, serikali ya Taiwan ilifanya mfululizo wa mazoezi ya kijeshi kwenye kompyuta mwezi Aprili, kama utangulizi wa mazoezi ya kweli ambayo yanafanyika kuanzia tarehe 9 hadi 18 Julai.
Wakati wa mazoezi ya mwezi huu, vifaa kama vile mifumo ya kurusha makombora, ndege zisizo na rubani, na makombora yaliyotengenezwa nchini humo yatatumiwa.
Ni pamoja na mfumo mpya wa kurusha makombora wa Himars unaotolewa na Marekani – ni mfumo ule ule ambao Washington imeutoa kwa Ukraine – hurusha makombora masafa makubwa zaidi kuliko mfumo wa sasa unaotumiwa na jeshi la Taiwan.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mazoezi hayo yatahusisha wanajeshi wa akiba wapatao 22,000 - karibu 50% zaidi ya mwaka jana.
Tofauti na mwaka jana, mazoezi hayo hayataandaliwa katika skripti ili kuona uwezo wa wanajeshi wakati wa shambulio la kushtukiza.
Mabadiliko haya yanaonekana kufanywa kujibu ukosoaji wa mazoezi ya miaka ya nyuma ambayo yalionekana kuwa zaidi kama matangazo badala ya mazoezi halisi ya kijeshi.
Mwaka huu, sehemu ya mazoezi yatalenga katika kupambana na vitisho vya China dhidi ya Taiwan, ambavyo vimeshuhudia ndege za kivita za Beijing na meli zikiingia mara kwa mara katika anga na maji ya Taiwan.
Katika miaka ya hivi karibuni, Han Kuang yamejumuisha ulinzi wa raia. Pia raia kote kisiwani watashiriki katika mazoezi mengi ya kujiokoa.
Wakati wa mazoezi ya mwaka huu ya "vita vya mijini," ambayo kila moja yatadumu kama dakika 30, jumbe za simu zitatumwa kuhusu mashambulizi yanayokuja na ving'ora juu ya uvamizi wa anga vitasikika katika miji. Usafiri barabarani utasimamishwa huku vituo vya usafiri, maduka, hoteli na masoko yatalazimika kusimamisha shughuli.
Ripoti pia zinasema, mamlaka pia itatoa mtihani kwa watu wa Taiwan kujua uwezo wao wa kukabiliana na habari potofu na uwelewa wao juu ya Chama cha Kikomunisti cha China cha United Front, ingawa haijulikani ni jinsi gani hilo litafanyika.
Kwanini mazoezi yanaongezwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
China imekuwa ikiongeza kampeni zake za vita na kampeni za kutoa taarifa potofu nchini Taiwan, baadhi ya waangalizi wanasema zinalenga kudhoofisha ulinzi wa kisiwa hicho.
Marekani imeonya kuwa China ni "tishio la wazi" kwa Taiwan, ikirejelea tarehe ya mwisho ya 2027 ambayo Rais Xi Jinping anadaiwa kutoa kwa jeshi la China liwe tayari katika uwezo wa kuivamia Taiwan.
Hii ni tarehe ambayo haijawahi kuthibitishwa na Beijing - hata hivyo Marekani inasisitiza kwamba China "inajiandaa kwa uwezekano wa kutumia nguvu za kijeshi Asia.
Uhusiano kati ya Taiwan na China pia umekuwa wa mvutano hasa chini ya Rais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo William Lai, ambaye alichaguliwa mwaka jana.
Anashutumiwa na Beijing kama "mtu anayetaka kujitenga," Lai amechukua msimamo mkali zaidi dhidi ya China ikilinganishwa na mtangulizi wake, ikiwa ni pamoja na kuimarisha jeshi la Taiwan.
Haishangazi, mazoezi ya Han Kuang hayaifurahishi Beijing.
Kanali Mwandamizi Jiang Bin, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China, alisema siku ya Jumanne kwamba mazoezi ya mwaka huu "si chochote ila ni upuuzi na ujanja wa kujidanganya unaofanywa na mamlaka ya Chama cha Kidemokrasia cha eneo hilo."
Kwa nini mazoezi ni muhimu?
Mabadiliko katika mazoezi ya Han Kuang ni sehemu ya kuleta mageuzi katika jeshi na ulinzi wa Taiwan, mazoezi ambayo yamekosolewa ndani na nje katika miaka ya hivi karibuni.
Imani ya umma wa Taiwani kwa jeshi lao inabadilika-badilika lakini kwa ujumla imekuwa ya kati, huku uchunguzi wa mwaka jana ulionyesha ni 47.5% tu ya raia wana imani na uwezo wao wa ulinzi.
Wakati wa tawala zote mbili za Trump, Marekani imesisitiza mara kwa mara Taiwan kutumia pesa zaidi katika ulinzi wake na kufanya jeshi lake kuwa la kisasa.
Hatua ya kuimarisha ulinzi wao inakuja huku mashaka yakiongezeka nchini Taiwan kwamba Marekani chini ya Donald Trump haitaingilia kijeshi katika tukio la shambulio la China.
Marekani inalazimishwa na sheria kuisaidia Taiwan kujilinda, lakini Trump amekuwa na utata kuhusu hilo na hivi karibuni alikataa kutoa maoni yake iwapo ataiuzuia China kuichukua Taiwan kwa nguvu.
Kando na mabadiliko ya Han Kuang, Taiwan katika miaka ya hivi karibuni pia imepanua mafunzo ya kijeshi ya lazima, na kuunda nyambizi na makombora yake, na kujenga uwezo wake wa ulinzi katika miji na kwa raia.
Pia imewekeza katika mifumo midogo na silaha zinazohamishika zikiwemo ndege zisizo na rubani, na kuongeza mafunzo yake kwa wanajeshi kama sehemu ya mkakati unaolenga kufanya iwe vigumu kisiwa hicho kutekwa.















