Siri za kimkakati na kiuchumi za Taiwan zilivyo muhimu kwa mataifa yenye nguvu

China imesema inaiona ziara ya Pelosi kama ukiukaji mkubwa wa mamlaka yake

Chanzo cha picha, Getty Images

Mara tu baada ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi kutua Taiwan, maoni ya papo hapo kutoka China yalikuwa kwamba 'wale wanaocheza na moto wataungua.' 

Pelosi ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa Marekani kuzuru kisiwa hicho (Taiwan) katika kipindi cha miaka 25 iliyopita. Alikaa Taiwan kwa chini ya saa 24. 

China imesema inaiona ziara hiyo kama ukiukaji mkubwa wa mamlaka yake na changamoto kwa kanuni ya 'Sera ya China Moja'. 

Ikiwa ni kisasi cha kwanza kujibu ziara hiyo, China ilitangaza mazoezi ya kijeshi kuzunguka Taiwan ambayo ni pamoja na utumiaji wa makombora mazito. 

Pelosi alipotembelea Taiwan

Chanzo cha picha, Getty Images

China inakiona kisiwa hicho (Taiwan) kama jimbo la waasi ambao hivi karibuni au baadaye litaunganishwa tena nchini China, hata ikiwa itabidi kufanywa kwa nguvu. 

Lakini Taiwan, kwa upande mwingine, inajiona kuwa nchi huru, yenye serikali ya kidemokrasia, licha ya kwamba Taiwan haijawahi kutangaza rasmi uhuru wake kutoka kwa China. 

Ziara ya Nancy Pelosi imefanyika huku kukiwa na mvutano mkubwa kati ya Washington na Beijing na hali ambayo China imeanzisha mashambulizi kadhaa ya anga na majini kwenye kisiwa hicho kilichopo jirani. 

Hali hii inatia wasiwasi kwa sababu Taiwan ni mdau mkuu wa kimataifa ambaye hatima yake itaathiri siasa za kimataifa na uchumi. Umuhimu wa Taiwan umechambuliwa hapa chini. 

1. Kwa nini eneo la Taiwan ni muhimu? 

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kisiwa hiki kipo kilomita 120 hivi kutoka pwani ya kusini mashariki mwa bara la China. Ni eneo la bahari ambapo china, nchi ya pili duniani yenye nguvu kiuchumi imependekeza kupanua utawala wake katika miaka ya hivi karibuni. 

Taiwan haswa ni sehemu ya kile ambacho wataalamu wanakiita 'kisiwa cha kwanza'. 

Zeno Leoni, mtaalamu wa masuala ya kimataifa, ulinzi na uhusiano wa Sino-West katika Chuo cha King's College London, aliiambia BBC: "Ni aina ya kizuizi cha kijiografia kinachoanzia kusini mwa Japani kupitia Taiwan na Ufilipino hadi Bahari ya Kusini ya China. huenda Ni dhana ya enzi ya Vita Baridi.' 

Maeneo katika 'msururu huu wa kwanza wa visiwa' ni washirika wa Marekani na ni muhimu kwa sera yake ya kigeni.

Hakika, China imekiri kuhisi 'imezingirwa' kutoka kwa mtazamo wa kimkakati, anasema Leoni. 

Iwapo Taiwan ingekuwa sehemu ya China, wataalamu wengi wa nchi za Magharibi wanaamini kuwa China ingekuwa huru kupanua mamlaka yake katika eneo la Pasifiki na kutishia kambi za kijeshi za Marekani kama vile Guam na Hawaii. 

"China tayari ina ushawishi mkubwa wa kijeshi katika Bahari ya Kusini ya China, lakini ikiwa pia ina Taiwan, inaweza kuongeza ushawishi wake wa majini na kupata udhibiti kamili wa eneo hilo," anasema Leoni. Suala ambalo huenda likawa na athari katika biashara ya kimataifa.' 

Anasema kuwa 'Taiwan ni kiungo cha China kujilinda dhidi ya mzozo wowote wa kijeshi katika Bahari ya Kusini na Mashariki. 

Hata hivyo, China imesisitiza kuwa nia yake katika eneo hilo ni ya amani tu. 

2. Taiwan ina umuhimu gani katika uchumi wa Dunia? 

Uchumi wa Taiwan una umuhimu mkubwa sana. 

Kuanzia simu mahiri, kompyuta za mkononi, saa na vifaa vya michezo, vifaa vingi vya kielektroniki tunavyotumia kila siku duniani kote hutumia chip zilizotengenezwa Taiwan. 

Kampuni moja, Taiwan Semiconductor Manufacturing Company (TSMC), inahudumu nusu ya soko la kimataifa katika sekta hii. 

Katika mwaka wa 2021, TSMC ilikadiriwa kuwa na thamani ya karibu dola bilioni 100. 

Iwapo Taiwan ingeungana na China, Beijing ingepata udhibiti wa mojawapo ya sekta muhimu zaidi duniani. 

Soko la hisa la Taipei liliona mwelekeo mzuri baada ya ziara ya Nancy Pelosi

Chanzo cha picha, EPA

"Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa China ipo nyuma katika maendeleo ya chip na vifaa maalum vya kompyuta na itachukua takriban miaka 20," Leoni anasema. Hii ni moja ya udhaifu wake na hatua nyingine ya mvutano.' 

Ikiwa China itafanikiwa kuvipata vitu hivi kutoka kwa Taiwan, kutakua na matokeo makubwa sana ndani ya siku za hivi karibuni. 

"China na Marekani zinashindana kuendeleza teknolojia hizi," anasema Leoni. Ikiwa vifaa hivi maalum vya Taiwan vitaangukia mikononi mwa Wachina, nchi za Magharibi zinaweza kupoteza nafasi yake kuzipata, na watalazimika kuzalisha wanazohitaji wenyewe, na bei zitapanda sana. 

Huu ni mwelekeo ambao unaweza kuendelezwa katika tasnia nyingine pia hadi Magharibi itakapokuza minyororo mingine ya usambazaji na uwezo wa uzalishaji. 

3. Kwa nini hali ya Taiwan ni ya kutatanisha sana? 

Vyanzo vya kihistoria vinaonyesha kuwa kisiwa hicho kilikuwa chini ya udhibiti wa Wachina katika karne ya 17 wakati nasaba ya Qing ilipochukua utawala wake. 

Kisha mwaka wa 1895, baada ya kushindwa katika Vita vya Kwanza vya Sino-Kijapani, walikabidhi kisiwa hicho kwa Japani. 

Baada ya Japan kushindwa katika Vita vya pili vya dunia, China iliikalia tena Taiwan mwaka 1945. 

Lakini vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka katika ardhi ya China kati ya vikosi tawala vya Nationalist vikiongozwa na Chiang Kai-shek na Chama cha Kikomunisti cha Mao Zedong. 

Wakomunisti walishinda mwaka 1949 na kuchukua udhibiti wa Beijing. 

Mao Zedong akitangaza kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China

Chanzo cha picha, Getty Images

Chiang na wajumbe waliosalia wa serikali yake ya Kuomintang (KMT) walikimbilia kisiwa cha Taiwan mapema mwaka wa 1949 na kutangaza 'Jamhuri ya Uchina' katika eneo hilo, wakidai kwamba bado walikuwa serikali halali. 

Takriban watu hawa milioni 1.5, wanaoitwa Wachina wa bara, walitawala siasa za Taiwan kwa miaka kadhaa ingawa walikuwa asilimia 14 tu ya idadi ya watu. 

Baada ya kurithi utawala sambamba na kufahamu ukweli na shinikizo kutoka kwa jamii inayoipinga serikali na harakati changa ya kidemokrasia, mtoto wa Chiang Chiang Ching-kuo aliruhusu mchakato wa kidemokrasia kustawi katika kisiwa hicho. 

China hutumia historia kusema kwamba Taiwan ilikuwa mkoa wa Uchina, lakini WaTaiwan wengi pia wanatumia historia kudai kwamba hawakuwahi kuwa sehemu ya serikali ya kisasa ya China, ambayo ilianzishwa mara ya kwanza baada ya mapinduzi ya 1911. Wala Jamhuri ya Watu wa Uchina, iliyoanzishwa na Mao Zedong mnamo 1949. 

Nchi nyingi za Magharibi ziliitambua Jamhuri ya China iliyoanzishwa na Chiang nchini Taiwan kuwa serikali pekee halali, lakini mwaka 1971, Umoja wa Mataifa ulianzisha uhusiano wa kidiplomasia na Jamhuri ya Watu wa China mjini Beijing. 

Tangu wakati huo, idadi ya nchi zinazoitambua serikali ya Taipei imepungua hadi 15 pekee. Nyingi ya nchi hizi ziko Amerika Kusini na eneo la Karibea ambako serikali hii inaungwa mkono zaidi. 

Kwa kuzingatia pengo kubwa kati ya misimamo ya China na Taiwan, nchi nyingi zimetambua hali ya kutatanisha ambayo Taiwan inakaribia kuwa na sifa ya taifa huru, ingawa mfumo wake wa kisheria bado haujafahamika. 

Nchi nyingi za Magharibi ziliitambua Jamhuri ya China iliyoanzishwa na Chiang

Chanzo cha picha, Reuters

Nguvu za kijeshi za China ni kubwa maradufu kuliko za Taiwan. 

Ndio maana baadhi ya wataalam wa nchi za Magharibi wanaamini kwamba Taiwan inaweza kuzuia uvamizi wa Wachina kwa kiasi kidogo sana hadi msaada wa kigeni upatikane. 

Usaidizi huu unaweza kuwa wa mauzo ya silaha ya Marekani kwa Taiwan. 

Hadi sasa, sera ya Washington ya 'utata wa kimkakati' haijafahamika iwapo Marekani ingeilinda Tiwan au la katika tukio la shambulio, na kama ni hivyo, ni kwa njia ipi. 

Kidiplomasia, Marekani kwa sasa inafuata sera ya 'China Moja', ambayo China iko chini ya utawala wa kisheria wa Beijing. Kwa hivyo Marekani ina uhusiano wa kidiplomasia na Beijing badala ya Taipei. 

Lakini mwezi Mei, Rais wa Marekani Joe Biden inaonekana alisisitiza msimamo huu na kusema kwamba ikiwa ni lazima, ataitetea Taiwan kijeshi.