Nancy Pelosi: Kwa nini ziara ya Spika wa bunge la Marekani Taiwan inaikera China?

Nancy Pelosi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nancy Pelosi

Mamlaka ya China imekasirishwa na ziara ya Spika wa Bunge la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi nchini Taiwan na kuionya Washington kuhusu madhara makubwa. Lakini kwa nini ziara ya mwanasiasa mashuhuri wa Marekani inaweza kuwa suala la kisiasa?

Beijing inaichukulia Taiwan kuwa eneo la Uchina, ingawa haidhibiti rasmi kisiwa hicho na serikali yake. Pelosi ndiye mwanasiasa wa ngazi ya juu zaidi wa Marekani kuzuru kisiwa hicho tangu 1997.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema kuwa ziara ya Pelosi inachukuliwa kudhoofisha uhuru wa China, na Marekani itawajibika kwa hilo.

Hapo awali Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilikuwa imetangaza kwamba hakuna taarifa rasmi kuhusu safari ya Pelosi, na sera ya Marekani kuelekea Taiwan bado haijabadilika.

Licha ya kukosekana kwa uhusiano rasmi wa kidiplomasia, Washington inadumisha "uhusiano usio rasmi" na Taiwan na kuipatia msaada wa kijeshi na kiufundi.

Hata hivyo, Marekani haitambui Taiwan kama taifa huru.

Kwa nini Pelosi alizuru Taiwan?

Katika kazi yake yote ya miaka 35 katika bungee la Congress, Nancy Pelosi amekuwa mkosoaji mkubwa wa Uchina. Alishutumu ukiukwaji wa haki za binadamu, alikutana na wapinzani wa China, na alitembelea bustani ya Tiananmen kuwaheshimu wahasiriwa maandamano ya 1989 waliopigwa risasi.

Pelosi hapo awali alipanga kutembelea Taiwan mnamo Aprili 2022, lakini ziara hiyo iliahirishwa baada ya kugunduliwa na virusi vya corona. Pelosi alikataa kujadili maelezo ya ziara yake iliotarajiwa kufanyika mwezi Agosti, lakini alisema wiki iliyopita ilikuwa "muhimu kuisaidia Taiwan."

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Spika Pelosi azindua "mtu mbele ya tanki" sanamu kutoka Tiananmen Square kwenye mkutano na wapinzani wa China mnamo 2019.

Mamlaka ya Taiwan daima inaituhumu China kwa uchochezi wa kijeshi dhidi ya kisiwa hicho. Pamoja na kuanza kwa vita nchini Ukraine, hali ilizidi kuwa mbaya zaidi, na wataalamu walisema kwamba huenda Rais wa China Xi Jinping akaiga mfano wa Rais Vladmir Putin na kuanzisha "operesheni ya ukombozi" kisiwani humo ili kutambua utawala wa Kichina.

Serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ya Taiwan, ikijibu madai ya China, inasema kwamba ni wakaaji milioni 23 pekee wa kisiwa hicho wanaweza kuamua mustakabali wao, na wako tayari kujilinda iwapo watashambuliwa kijeshi.

Kwa nini China inapinga ziara hiyo na inatishia matokeo gani?

Beijing inachukulia Taiwan kuwa eneo lake na imetishia mara kwa mara kulichukua hata ikiwa ni lazima. Maafisa wa China tayari wameelezea hasira zao kwa kile wanachokiona kama kuongezeka kwa ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Taipei na Washington.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian alionya kwamba nchi hiyo itachukua hatua kali ikiwa Nancy Pelosi atazuru Taiwan.

Rais Joe Biden wa Marekani na mwenzake wa China Xi Jin Ping wakiwasiliana

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais Joe Biden wa Marekani na mwenzake wa China Xi Jin Ping wakiwasiliana

Ziara ya Pelosi, inakuja huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kati ya Washington na Beijing

Na msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China hakufutilia mbali jibu la kijeshi. Hatua yake inaweza kuwa uundaji wa eneo lisiloruhusu ndege kupita juu ya Taiwan na hata operesheni kamili ya kutua.

"Ikiwa upande wa Marekani utaendelea, jeshi la China halitanyamaza kuchukua hatua kali kuzuia uingiliaji wowote kutoka nje na majaribio ya kujitenga kufikia uhuru wa Taiwan," Kanali Tang Kefei aliiambia China Daily.

Kwa nini ziara ya Pelosi ni muhimu kwa Taiwan

Taiwan inakaribisha viongozi wote wa kigeni kutoka Marekani, Ulaya na Asia, kwa kutumia ziara zao kama ulinzi unaowezekana dhidi ya China na kukabiliana na kampeni yake ya kutengwa kidiplomasia.

Hata hivyo, Taiwan inajaribu kuzidhibiti ziara hizo ili kuepusha makabiliano na China, ambayo inasalia kuwa mshirika muhimu wa kiuchumi wa nchi hiyo. Isitoshe, takriban WaTaiwani milioni moja wanaishi China Bara.

Taiwan ikifanya zoezi la kijeshi

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Taiwan ikifanya zoezi la kijeshi

Raia wa Taiwan wanapinga vikali madai ya China ya kuungana, lakini uwezo wa majeshi ya kisiwa hicho kujilinda dhidi ya uvamizi unaowezekana wa Wachina bila msaada wa Marekani ni wa kutilia shaka sana, hivyo mamlaka ya kisiwa hicho inahitaji kuimarisha uhusiano na Washington ili kuweza kupata silaha.

Je Marekani inasemaje

"Jeshi linadhani hili si wazo zuri kwa sasa. Hata hivyo, sijui hali ya [safari ya Pelosi] ikoje," Rais wa Marekani Joe Biden alinukuliwa akisema wiki iliyopita.

Kama Pentagon ilivyoelezea, "si wazo zuri" inamaanisha kuwa jeshi linawafahamisha washauri wa Washington juu ya hatari, ambayo China inaweza kufanya na jinsi Marekani itafanya.

Vyombo vya habari pia viliripoti kuwa utawala wa Biden ulikuwa ukijaribu kumzuia spika wa Bunge hilo kuzuru Taiwan. Wakati huo huo, Ikulu ya White House iliita matamshi ya Wachina kuhusu ziara hiyo kama yasio na maana .

Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi

"Safari ya Pelosi inaweza kuleta madhara zaidi kuliko mema?" Ufafanuzi wa Rupert Wingfield-Hayes, Mwandishi wa BBC Taipei

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ikiwa wewe ni taifa dogo la kisiwa, lisilotambuliwa na Umoja wa Mataifa, na upo chini ya tishio la uvamizi kutoka kwa jirani mkubwa zaidi na mwenye nguvu zaidi, basi ziara ya mwanasiasa wa tatu mwenye nguvu zaidi nchini Marekani inapaswa kuwa tukio la kupendeza kwako.

Ndio maana serikali ya Taiwan haikumzia Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi kutozuru kisiwa hicho.

Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen kwa muda mrefu ametoa wito wa kuwepo kwa kiwango cha juu cha ushirikiano na Marekani. Lakini pia kuna wasiwasi kuhusu kwa nini Pelosi anafanya ziara hiyo hivi sasa, na uiwapo kama safari yake inaweza kuleta madhara zaidi kuliko manufaa.

Rais Joe Biden alisema mara tatu mwaka uliopita kwamba Marekani itaingilia kati kuiunga mkono Taiwan iwapo China itavamia, lakini wafanyakazi wake walipunguza sauti hiyo wakisisitiza kwamba sera ya Marekani haijabadilika.

Wakati ziara ya Pelosi kuzuru Taiwan ilipovuja, Rais Biden hakuiunga mkono, lakini badala yake alisema, "Idara ya Ulinzi haioni kuwa ni wazo zuri."

Huko Beijing, hii inaonekana kama udhaifu, huko Taipei - kama mkanganyiko. Lakini ni nini sera halisi ya serikali ya Marekani katika kisiwa hicho?

Nancy Pelosi ana umri wa miaka 82 na anatarajiwa kustaafu katika msimu wa joto. Je, amewasili Taiwan kwa nia nzuri ya kutoa uungwaji mkono wa kweli, au huu ni mkwamo wa kisiasa? Haya yote hayako wazi kufikia sasa.