"Wanaocheza na moto wataungua": China yalaani ziara ya Nancy Pelosi nchini Taiwan na kutangaza mazoezi ya kijeshi

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la China litafanya mazoezi makali karibu na kisiwa cha Taiwan kuanzia tarehe 4 hadi 7 Agosti.
Itafanya hivyo kujibu ziara ya Spika wa Bunge la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi, nchini Taiwan, ambako aliwasili Jumanne.
Beijing inadai kisiwa hicho kama eneo lake na imechukua safari ya kiongozi huyo wa bunge, amnbaye pia ni afisa wa ngazi ya juu zaidi wa Marekani kisiwani Taiwan katika miaka 25, kama dharau kubwa.
Muda mfupi baada ya Pelosi kutua Taipei, vyombo vya habari vya China vilitangaza zoezi hilo la kijeshi na kupiga marufuku meli na ndege zote za raia kuingia katika maeneo ya jirani.
"Wale wanaocheza na moto wataungua," Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema, ikiitaja safari hiyo kuwa "hatari sana."
Kiongozi wa Marekani Nancy Pelosi aliikaidi Uchina na kuwasili Taiwan katika safari ya kwanza ya ngazi ya juu ya Marekani katika "kisiwa " hicho baada ya takriban miaka 25.

Chanzo cha picha, Getty Images
China yatoa onyo
Mazoezi ya kijeshi ya China yatajumuisha "ufyatuaji risasi wa masafa marefu kwenye Mlango wa Bahari wa Taiwan," kulingana na jeshi.
"Hatua hii inaelekezwa kujibu ongezeko la hivi karibuni la kushtua la Marekani kuhusu suala la Taiwan," msemaji wa kijeshi alisema katika taarifa.
Pia alihakikisha kwamba "ni onyo kubwa kwa majeshi ya uhuru wa Taiwan au kwa wale wanaotafuta uhuru."












