China yarusha makombora karibu na Taiwan baada ya ziara ya Pelosi

Makombora ya masafa marefu
Maelezo ya picha, Makombora ya masafa marefu ya China

China imerusha makombora karibu na Taiwan kama sehemu ya mazoezi makubwa ya kijeshi kufuatia ziara ya mwanasiasa mkuu wa Marekani Nancy Pelosi katika kisiwa hicho.

Taiwan ilisema China ilirusha makombora 11 ya masafa marefu kwenye maji karibu na pwani ya kaskazini-mashariki na kusini-magharibi mwa Taiwan.

Japan ilisema makombora matano ya China yalianguka katika maji yake pia, ikitoa wito wa "kusimamishwa mara moja" kwa mazoezi hayo.

Uchina iliona ziara hiyo, ya Spika wa Bunge la Merika Bi Pelosi, kama changamoto kwa madai yake ya uhuru juu ya Taiwan.

Jimbo lililojitenga

Inaiona Taiwan kama jimbo lililojitenga ambalo hatimaye litaletwa chini ya udhibiti wake - kwa nguvu ikiwa ni lazima.

Marekani, kwa upande wake, haitambui rasmi Taiwan, ambayo kwa madhumuni yote ya kivitendo imekuwa huru tangu 1950. Hata hivyo, Washington inadumisha uhusiano mkubwa na kisiwa hicho - ambao ni pamoja na kuiuzia silaha ili kujilinda.

"Mazoezi hayo yanazingatia vikao muhimu vya mafunzo ikiwa ni pamoja na kuzuia kwa pamoja, mashambulizi ya shabaha baharini, mashambulizi ya shabaha ardhini, operesheni ya udhibiti wa anga," kwa mujibu wa kitengo cha maonyesho ya Mashariki ya jeshi la China katika taarifa.

Ziara fupi ya Bi Pelosi nchini Taiwan siku ya Jumatano ilichochea mvutano, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi akiielezea kama "mwenda wazimu, asiyewajibika na asiye na akili". Yeye ndiye mwanasiasa mkuu zaidi wa Marekani kuzuru kisiwa hicho katika miaka 25.

Maelezo ya video, Tazama Makombora ya China yalivyofyatuliwa karibu na Taiwan baada ya ziara ya Nancy Pelosi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

China ilijibu kwa kurusha makombora ya balestiki na mazoezi ya kijeshi karibu na pwani ya Taiwan ambayo hayajawahi kushuhudiwa.

Wizara ya ulinzi ya Taiwan ilisema kuwa imewasha mifumo yake ya ulinzi na inafuatilia hali hiyo.

Wizara ya mambo ya nje ya Taiwan iliishutumu China kwa "kufuata mfano wa Korea Kaskazini katika kufanyia majaribio makombora kwenye maji yalio karibu na nchi nyingine".

Korea Kaskazini - mshirika mkubwa wa China - imeshutumiwa kwa kuchochea hali ya wasiwasi katika eneo hilo kwa kuzindua majaribio ya makombora mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni.

Siku ya Alhamisi, Japan ilitoa malalamiko yake makali dhidi ya urushaji huo wa makombora unaotekelezwa na China.

"Tunalaani vikali kitendo hicho kwani ni suala zito linalohusu usalama wa Japan na usalama wa watu wa Japan," Waziri wa Ulinzi wa Japani Nobuo Kishi alisema.

Urushaji wa makombora ya China unasababisha usumbufu kwa njia za meli na safari za ndege kwenda na kutoka Taiwan.

Meli zimelazimika kusafiri tena, huku usumbufu wa siku nzima ukitarajiwa kuwa na athari kwenye minyororo ya usambazaji na kucheleweshwa kwa usafirishaji wa kimataifa.

Zaidi ya safari 50 za ndege za kimataifa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Taoyuan nchini Taiwan zimekatishwa.

Katika bandari ya wavuvi ya Bi Sha Yu, wavuvi walioketi kando ya bandari wanatengeneza nyavu zao na kunung’unika kwa sauti kubwa: “Sikuzote ni sisi watu wadogo ambao tunateseka wanasiasa wanapopigana,” asema nahodha mmoja.

"Lakini tunaweza kufanya nini, ni hatari sana kwenda huko sasa."

Mwingine alikuwa akijifunga baada ya kurudi bandarini. "Nilitoka asubuhi ya leo, lakini walinzi wa pwani walitumia redio na kutuambia turudi bandarini mara moja," anasema.

Watu wengi ambao BBC ilizungumza nao hawaamini kuwa China iko karibu kushambulia Taiwan. "Wao ni kundi la majambazi," asema mwanamume mmoja anayevua samaki kwenye kizimba.

Unaweza pia kusoma

"Wakomunisti hao wanazungumza sana, lakini hawatafanya lolote. Tumeishi na vitisho vyao kwa miaka 70."

Taarifa ya Mwandishi wa BBC Rupert

Kutokana na kuongezeka kwa mvutano huo, jeshi la wanamaji la Marekani lilisema limekituma chombo chake cha majini - USS Ronald Reagan - ambacho kinaelekea sehemu ya bahari inayojumuisha maji ya kusini-mashariki mwa Taiwan.

Meli ya kivita ya "USS Ronald Reagan na kundi lake la mashambulizi linaelekea katika Bahari ya Ufilipino ikiendelea na shughuli za kawaida, zilizopangwa kama sehemu ya kupiga doria ya kawaida ya kuweka huru mkondo wa bahari wa Indo-Pacific ," msemaji wa jeshi la wanamaji alisema Alhamisi.

Ndege ya Marekani inayoweza kufuatilia makombora ya masafa marefu pia imepaa kutoka Japan ikielekea Taiwan.

China na Taiwan: Tunachojua

Kwa nini China na Taiwan zina uhusiano mbaya? China inakiona kisiwa hicho kinachojitawala kama sehemu ya eneo lake na inasisitiza kuwa inapaswa kuunganishwa na bara, kwa nguvu ikiwa ni lazima.

Taiwan inatawaliwa vipi? Kisiwa hicho kina katiba yake, viongozi waliochaguliwa kidemokrasia, na takriban wanajeshi 300,000 wanaofanya kazi katika vikosi vyake vya jeshi.

Nani anaitambua Taiwan? Ni nchi chache tu zinazoitambua Taiwan. Wengi wanaitambua serikali ya China iliyoko Beijing badala yake. Marekani haina uhusiano rasmi na Taiwan lakini ina sheria inayoitaka kukipa kisiwa hicho njia ya kujilinda.

Taiwan
Maelezo ya picha, Taiwan