Kombe la Mataifa ya Afrika: Timu tano zinazopigiwa upatu kushinda AFCON 2025

Chanzo cha picha, Getty Images
Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025, inayoendelea nchini Morocco ni kati ya michuano isiyotabirika zaidi katika historia ya hivi majuzi.
Tangu kuanzishwa kwa AFCON 1957 mashindano hayajakuwa wazi hali ya kwamba mataifa matano au sita yanaweza kuwania taji hilo kwa umakini.
Mbali na mwenyeji,Morocco, mataifa kadhaa ni miongoni mwa washindani wakuu: Senegal, Misri, Ivory Coast na Algeria, zote tayari zimefuzu kwa Kombe la Dunia la 2026.
Moja ya maajabu ya Kombe la Mataifa ya Afrika ni kutotabirika kwake. Hakuna mashindano mengine ya bara yanayokaidi utabiri kama huo.
Matoleo manane ya mwisho yameshuhudia mabingwa saba tofauti, huku Ivory Coast ikiwa ndiyo pekee iliyotawazwa mara mbili katika matoleo matano yaliyopita, mwaka wa 2015 na 2024.
Morocco: Simba wa Atlas wanataka kuweka historia nyumbani

Chanzo cha picha, Pablo Morano/BSR Agency/Getty Images Images
Takriban nusu karne baada ya taji lao pekee la bara, Wamorocco wanaota ndoto ya ushindi kwenye ardhi ya nyumbani.
Chini ya kocha Walid Regragui, Morocco, taifa lililoorodheshwa juu zaidi barani Afrika katika viwango vya FIFA, lilifikia kilele cha kandanda ya dunia mnamo 2022, na kuwa timu ya kwanza ya Afrika kucheza nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Simba wa Atlas inaingia katika mashindano hayo sio tu kwa fursa nzuri walio nayo nyumbani, lakini pia kwa dhamira ya kupata taji lao la pili la Ubingwa wa Mataifa ya Afrika tangu 1976.
Mbele ya umati wao wa nyumbani, Wamorocco wanaota hatma ya mtindo wa Ivory Coast, ushindi wa nyumbani lakini bila hofu ya raundi ya kwanza.
Lakini kuandaa mashindano sio fursa nzuri pekee. Katika matoleo 34 ya Kombe la Mataifa ya Afrika tangu 1957 (ikiwa ni pamoja na toleo la uzinduzi), nchi mwenyeji imeshinda mashindano hayo mara 12 pekee, au karibu 35% ya muda wote.
Tangu mwaka 2000, ni Tunisia (2004), Misri (2006) na Ivory Coast (2024) pekee ndizo zimeshinda katika ardhi ya nyumbani.
Misri: Mafarao wanaopigiwa upatu zaidi

Chanzo cha picha, Haykel Hmima/Anadolu Agency via Getty Images
Mabingwa mara saba wa Afrika, Mafarao hawako mbali na taji hilo.
Taifa lenye sifa zaidi barani Afrika lina ndoto ya kutwaa taji la nane ili kufuta tamaa ya fainali iliyopotea mwaka wa 2022 dhidi ya Senegal.
Timu ya Misri inachanganya furaha ya vijana na uzoefu, mchanganyiko ambao umeiruhusu kuchukua majukumu makubwa katika mashindano ya bara.
Chini ya uongozi wa Hossam Hassan, Misri inacheza kwa kasi, wima zaidi, huku ikidumisha nidhamu yake ya kimbinu.
Omar Marmoush na Mostafa Mohamed wanawakilisha kizazi hiki kipya chenye matamanio, wakiongozwa na nyota Mohamed Salah ambaye atatarajiwa kuomyesha ubora wake nchini Morocco.
Wasiostaajabisha, lakini wenye ufanisi wa kutisha, Mafarao wamesalia waaminifu kwa sifa yao kama washindani wa kutisha.
Ivory Coast: Tembo wanaotaka kurudi kileleni

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakiwa wameshinda Kombe la Mataifa ya Afrika katika ardhi ya nyumbani mnamo 2024 baada ya kuonesha mchezo mzuri, Tembo wanaingia kwenye AFCON kama mabingwa watetezi.
Hii inawafanya kuwa wapendwa katika shindano ambalo wameshinda mara tatu, ikijumuisha mara mbili katika matoleo matano yaliyopita.
Chini ya uongozi wa Emerse Faé, Tembo wanawasili Morocco wakiwa na nia ya kuhifadhi taji lao. Lakini changamoto inathibitisha kuwa kubwa.
Tangu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ilipoanza mwaka 1957, ni timu tatu pekee ambazo zimefanikiwa kuhifadhi taji lao.
Misri ilifanya hivyo mwaka wa 1957 na 1959, na tena wakati wa ushindi wa tatu wa kihistoria mwaka wa 2006, 2008, na 2010. Ghana ilishinda mwaka wa 1963 na 1965, na Cameroon mwaka wa 2000 na 2002.
Senegal, mpinzani mkubwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Senegal, ambayo hatimaye ilishinda nyota wake wa kwanza miaka minne iliyopita baada ya kusubiri kwa muda mrefu na kushindwa kwa fainali mbili (2002 na 2019), bado ni mshindani mkubwa.
Baada ya kushinda AFCON 2021, lakini wakaondolewa mapema miaka miwili baadaye, inaonekana kurejesha usawa wake chini ya uongozi wa Pape Thiaw, mrithi wa Aliou Cissé.
Kando na wachezaji wenye uzoefu kama Sadio Mané, Kalidou Koulibaly na Idrissa Gueye, Simba wa Teranga pia wataweza kutegemea ujio wa wachezaji wachanga wenye vipaji wanaoingia kwenye mwisho wa mashindano ya bara.
Simba ya Teranga, pamoja na zile za Atlas Morocco, ndizo timu mbili bora za Afrika katika viwango vya FIFA, zikiwa za 18 na 12 mtawalia.
Senegal, ambao walitawala kundi lao la kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026, watategemea mwendelezo na utulivu kurudia ushindi wa 2022.
Algeria wakati wa ukombozi

Chanzo cha picha, Billel Bensalem / APP/NurPhoto via Getty Images
Baada ya mchuano wa awamu mbili kwenye mashindano ya AFCON 2021 na 2023 ambapo walitolewa katika hatua ya makundi, Fennecs wanataka kufungua ukurasa mpya.
Djamel Belmadi alibaki katika nafasi yake, ameamua kujenga tena timu ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa na iliyotiwa moyo.
Kizazi kilichoshinda ubingwa wa 2019 kinadidimia taratibu, na kutoa nafasi kwa wimbi jipya lililojumuisha Fares Chaïbi, Houssem Aouar, Rayan Aït Nouri, na Badredine Bouanani. Timu hiyo ina vipaji, lakini changamoto itakuwa ya kiakili: kugundua tena ugumu na mshikamano ambao ulikuwa nguvu ya timu.
Algeria bado ni mpinzani mkubwa, mwenye uwezo. Iwapo Belmadi ataweza kuleta utulivu wa kikosi chake na kufufua shauku yao, Fennecs wanaweza tena kuwa kikosi cha pamoja ambacho kiliiduwaza Afrika mwaka wa 2019.
Lakini Algeria italazimika kugundua upya makali yake, umoja na ubunifu uliopelekea kutwaa taji la 2019.















