Uturuki yawakamata washukiwa 115 wa IS

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka nchini Uturuki inasema kuwa imetibua jaribio la mashambulizi yaliyopangwa kufanyika wakati wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya baada ya kuwakamata zaidi ya watu 100 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi linalojiita Islamic State.
Uvamizi mkubwa ulifanyika katika nyumba 124 kote Istanbul, mwendesha mashtaka mkuu wa jiji hilo alisema, huku bunduki, risasi na "hati za shirika" zikikamatwa.
Maafisa walisema wafuasi wa IS wamekuwa wakipanga mashambulizi kote Uturuki wiki hii, haswa dhidi ya wasio Waislamu.
Polisi waliwazuilia washukiwa 115 lakini juhudi zinaendelea kuwatafuta wengine 22, taarifa rasmi ilisoma.
Ofisi ya mwendesha mashtaka ilisema washukiwa hao walikuwa wakiwasiliana na maafisa wa IS nje ya Uturuki.
Tangazo hilo linakuja siku mbili baada ya maafisa wa ujasusi wa Uturuki kufanya uvamizi dhidi ya kundi hilo kwenye mpaka wa Afghanistan na Pakistan.
Raia wa Uturuki ambaye anadaiwa kushikilia wadhifa wa juu katika mrengo wa IS unaohudumu katika eneo hilo alizuiliwa kwa tuhuma za kupanga mashambulizi dhidi ya raia.
Huduma za usalama za Uturuki mara kwa mara huwalenga watu wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na IS.









