Mazungumzo ya amani yakiendelea, Urusi yaishambulia Ukraine kwa makombora

Urusi imefanya mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya miundombinu ya Ukraine wakati mazungumzo kati ya Marekani na Ukraine yakiingia siku ya tatu huko Florida.
Usiku wa kuamkia Jumamosi, Ukraine ilisema Urusi ilirusha ndege zisizo na rubani 653 na makombora 51, ambapo mengi yalidunguliwa, huku shambulio moja likilenga kituo cha reli cha Fastiv na kuharibu jengo kuu la stesheni.
Rais Volodymyr Zelensky alisema mashambulizi hayo hayakuwa na maana kijeshi, huku Urusi ikidai inalenga viwanda vinavyohusiana na jeshi pamoja na miundombinu ya nishati na bandari. Wizara ya nishati ya Ukraine ilisema mashambulizi mapya yameathiri mikoa minane na kusababisha kukatika kwa umeme.
Wakati huohuo, shirika la nyuklia la Umoja wa Mataifa lilisema kuwa Kiwanda cha Nyuklia cha Zaporizhzhia kilichodhibitiwa na Urusi kilipoteza nguvu za umeme za nje kwa muda, jambo ambalo limekuwa likijirudia tangu uvamizi wa Urusi kuanza.
Huko Florida, mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff na Rustem Umerov wa Ukraine walisema mazungumzo yao yamekuwa “ya kujenga” na wamekubaliana juu ya mfumo wa mipango ya kiusalama ambayo inaweza kuandamana na makubaliano ya amani. Walisema kumaliza vita kunategemea utayari wa Urusi kuchukua hatua za kupunguza mvutano na kusitisha mauaji.
Mazungumzo hayo yameingia siku ya tatu, na timu ya Ukraine ikipokea taarifa kuhusu mkutano wa hivi karibuni kati ya Witkoff na Rais Vladimir Putin mjini Moscow.






