Benki ya Dunia yaondoa marufuku ya mikopo kwa Uganda iliyowekwa kwa kubagua watu wa LGBTQ
Benki ya Dunia imesema inaondoa marufuku ya mikopo kwa Uganda ambayo ilikuwa imeweka miaka miwili iliyopita wakati nchi hiyo ilipopitisha sheria mpya dhidi ya watu wa LGBTQ.
Muhtasari
- Chad yaapa kulipiza kisasi dhidi ya marufuku ya kusafiri ya Marekani
- Wanane wajeruhiwa kwenye ndege ya Ryanair iliyokumbwa na 'msukosuko mkubwa'
- Benki ya Dunia yaondoa marufuku ya mikopo kwa Uganda iliyowekwa kwa kubagua watu wa LGBTQ
- Rais wa zamani wa Zambia Lungu afariki dunia
- Kondomu ya miaka 200 ikiwa bado 'katika bora wake' - jumba la makumbusho
- Urusi yatambua British Council kuwa "shirika lisilofaa"
- Tulielekezewa bunduki kichwani na wanajeshi wa Israel - Timu ya BBC
- Mfanyikazi wa waziri mkuu ashtakiwa kwa kurekodi wanawake kwa siri
- Jeshi la Israel laipata miili miwili ya mateka kusini mwa Gaza
- Hatua zilizochukuliwa na Saudi Arabia katika Hijja ya mwaka huu
- Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yapiga marufuku kuripoti habari za rais wa zamani Josep Kabila
- Chama tawala nchini Burundi chaazimia kuendelea kubaki mamlakani
- Shahidi asema Sean "Diddy" Combs alimning'iniza kwenye roshani ya ghorofa
- Ni nani ambaye ameondolewa kwenye marufuku ya kusafiri na Trump?
- Trump asaini marufuku ya kusafiri kwenda Marekani dhidi ya raia wa nchi 12
- Putin atalipiza kisasi kwa shambulio la ndege zisizo na rubani za Ukraine, anaonya Trump
Moja kwa moja
Na Dinah Gahamanyi & Asha Juma
Chad yaapa kulipiza kisasi dhidi ya marufuku ya kusafiri ya Marekani

Chanzo cha picha, Reuters
Chad inasema itasimamisha utoaji wa viza kwa raia wa Marekani kama kulipiza kisasi marufuku ya kusafiri iliyowekwa dhidi ya taifa hilo la Afrika ya Kati na Rais Donald Trump.
Katika taarifa iliyowekwa kwenye mitandao yake ya kijamii Rais Mahamat Deby alisema: "Nimeagiza serikali kuchukua hatua sawa na hiyo na kusimamisha utoaji wa viza kwa raia wa Marekani".
Aliongeza kuwa "Chad haina ndege wala mabilioni ya dola ya kutoa lakini ina hadhi na fahari yake."
Chad ni kati ya nchi saba za Afrika zilizoathirika na marufuku ya kusafiri ya Rais Trump.
Alielezea viza ya nchi hiyo ya kupitisha muda wa kukaa nchini Marekani kama isiyokubaliki, akisema inaonyesha kutojali kabisa sheria za uhamiaji za Marekani.
"Kuingia Marekani kwa raia wa Chad kama wahamiaji na wasio wahamiaji kwa sasa kumesimamishwa kabisa".
Kinachosubiriwa ni kuona jinsi Marekani itakavyoitikia hatua ya Chad.
Soma zaidi:
Wanane wajeruhiwa kwenye ndege ya Ryanair iliyokumbwa na 'msukosuko mkubwa'

Chanzo cha picha, PA Media
Abiria wanane walijeruhiwa kwenye ndege ya Ryanair iliyoelekezwa kwenye uwanja wa ndege kusini mwa Ujerumani baada ya kukumbwa na "msukosuko mkali" kutokana na hali mbaya ya hewa, polisi walisema.
Miongoni mwa waliojeruhiwa Jumatano usiku ni mtoto wa miaka miwili ambaye alipata michubuko na mwanamke aliyejeruhiwa kichwani, kulingana na polisi wa Bavaria.
Watu watatu walipelekwa katika hospitali ya eneo hilo kwa matibabu, wakati wengine walitibiwa kwenye eneo la tukio, walisema.
Ryanair iliomba msamaha kwa abiria walioathirika. Ilisema nahodha wa ndege hiyo, kutoka Berlin hadi Milan, aliomba msaada wa matibabu na ndege "ilitua kawaida" kwenye uwanja wa ndege wa Memmingen.
Soma zaidi:
Benki ya Dunia yaondoa marufuku ya mikopo kwa Uganda iliyowekwa kwa kubagua watu wa LGBTQ

Chanzo cha picha, RAJESH JANTILAL / AFP
Benki ya Dunia imesema inaondoa marufuku ya mikopo kwa Uganda ambayo ilikuwa imeweka miaka miwili iliyopita wakati nchi hiyo ilipopitisha sheria mpya dhidi ya watu wa LGBTQ.
Mnamo 2023, Uganda ilipiga kura na kuidhinisha moja ya sheria kali zaidi za kupinga mapenzi ya jinsi moja duniani ikimaanisha kwamba mtu yeyote anayejihusisha na vitendo vya mapenzi ya jinsi moja anaweza kuhukumiwa kifo.
Tangu wakati huo, mamia ya watu wamefurushwa kutoka kwa nyumba zao, kufanyiwa ukatili au kukamatwa kwa sababu ya jinsi zao, kulingana na Jukwaa la Uhamasishaji na Ukuzaji wa Haki za Kibinadamu la Uganda.
Lakini Benki ya Dunia inasema kuwa ina imani kwamba "hatua mpya za kupunguza athari iliyopo" zitairuhusu kusambaza ufadhili kwa njia ambayo haidhuru au kubagua watu wa LGBTQ.
BBC imetuma maombi kwa serikali ya Uganda na Benki ya Dunia kwa maoni zaidi.
"Benki ya Dunia haiwezi kutekeleza dhamira yake ya kumaliza umaskini na kukuza ustawi wa pamoja isipokuwa watu wote wawe wanaweza kushiriki, na kufaidika na, miradi tunayofadhili," msemaji aliliambia shirika la habari la AFP siku ya Alhamisi, akiongeza kuwa shirika hilo "limeshirikiana na serikali [ya Uganda] na wadau wengine nchini humo kuanzisha, kutekeleza na kufanyia majaribio" hatua za kupinga ubaguzi.
Wachambuzi wanasema Benki ya Dunia ni mojawapo ya vyanzo vikubwa vya ufadhili nchini Uganda kutoka nje, ikiwa na jukumu muhimu katika maendeleo ya miundombinu.
Uganda ni miongoni mwa mataifa kadhaa ya Afrika - ikiwa ni pamoja na Ghana na Kenya - ambayo katika miaka ya hivi karibuni yameshuhudia hatua za kukandamiza haki za watu wa LGBTQ.
Taarifa za sheria ya Uganda ya kupinga mapenzi ya jinsi moja mwaka 2023 zilisababisha shutuma kimataifa.
Soma zaidi:
Rais wa zamani wa Zambia Lungu afariki dunia

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa zamani wa Zambia Edgar Lungu amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, chama chake kimesema.
"Amekuwa akipokea matibabu maalum nchini Afrika Kusini" kwa ugonjwa ambao haujatajwa, chama cha Patriotic Front kilisema kikithibitisha habari hiyo.
Lungu aliongoza Zambia kwa miaka sita kuanzia 2015, na kushindwa katika uchaguzi na Rais wa sasa Hakainde Hichilema kwa kura nyingi.
Baada ya kushindwa katika uchaguzi huo alijiondoa kwenye siasa lakini baadaye akarejea na kuonekana kuwa na nia ya kugombea tena urais.
Kondomu ya miaka 200 ikiwa bado 'katika bora wake' - jumba la makumbusho

Chanzo cha picha, Rijksmuseum
Kondomu ya karibu miaka 200 – ambayo bado "iko katika ubora wake" - imeonyeshwa katika jumba la makumbusho la Rijksmuseum huko Amsterdam.
Inadhaniwa kuwa ilitengenezwa kwa kibofu cha mkojo cha kondoo na ina chapa inayoonekana kuwakilisha mtawa wa kike na makasisi watatu.
Kondomu hiyo ya kale adimu ni ya mwaka 1830 na ilinunuliwa na jumba la makumbusho katika mnada mwaka jana.
Kondomu hiyo ni sehemu ya maonyesho ya masuala ya ukahaba na ngono ya Karne ya 19. Machapisho, michoro na picha pia ni sehemu ya maonyesho.
Msimamizi wa makumbusho ya Rijksmuseum Joyce Zelen aliambia BBC wakati yeye na mwenzake walipoona kondomu hiyo kwenye mnada kwa mara ya kwanza "walikuwa wakicheka".
Bi Zelen alisema "hakuna mtu mwingine aliyegundua" na ni wao pekee walionadi.
Baada ya kupata kondomu hiyo, waliikagua kwa miale ya UV na kubaini kuwa haijatumika.
"Iko katika ubora wake," alisema Bi Zelen.
Pia unaweza kusoma:
Urusi yatambua British Council kuwa "shirika lisilofaa"

Chanzo cha picha, EPA
Urusi imetambua British Council taasisi ya elimu ya Uingereza kama "shirika lisilofaa," huku ikisema London ndio chanzo cha migogoro inayoshuhudiwa ulimwenguni na "mchocheaji wa vita."
Mahusiano kati ya Uingereza na Urusi yalisambaratika hata kabla ya Urusi kuanzisha uvamizi wake dhidi ya Ukraine mnamo mwaka 2022, ukijumuisha kashfa za ujasusi na kuingiliana, ikiwa ni pamoja na mpelelezi wa zamani wa Urusi Sergei Skripal kuwekewa sumu mnamo mwaka 2018 kwenye ardhi ya Uingereza.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Urusi alishutumu taasisi ya elimu ya British Council kwa kujaribu kuendeleza masilahi ya Uingereza "chini ya mwongozo wa kufundisha Kiingereza" na kuunga mkono "harakati za LGBT," ambazo Urusi imekataza" na kuitaja kuwa yenye msimamo mkali."
Moscow imetaja mashirika kadhaa yanayoungwa mkono na Magharibi kuwa "yasiyofaa," jina ambalo linakataza uendeshaji wa kazi zao nchini Urusi na kumfanya mtu yeyote ambaye anashirikiana nao kuwa katika hatari ya kuhukumiwa kifungo cha miaka kadhaa jela.
Uingereza imekuwa moja ya wafadhili wakubwa wa Ukraine tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake.
Urusi chini ya Rais Vladimir Putin kwa miaka mingi imekuwa ikichukua hatua kali dhidi ya asasi za kiraia, kuharamisha makundi wanayokinzana nayo na kuwashtaki wapinzani katika kampeni ambayo imeongezeka huku vita vya Ukraine vikiendelea.
Tulielekezewa bunduki kichwani na wanajeshi wa Israel - Timu ya BBC

Asubuhi ya tarehe 9 Mei, nilikuwa sehemu ya timu ya BBC Kiarabu iliyoondoka mji mkuu wa Syria, Damascus, kuelekea jimbo la kusini la Deraa. Kutoka hapo tulipanga kwenda mpakani na Milima ya Golan inayokaliwa na Israel.
Tulitaka kuwa karibu na eneo la Syria ambalo limetekwa na jeshi la Israel tangu mwezi Disemba, wakati waziri mkuu wa Israel aliposema kuwa lilikuwa linadhibiti kwa muda usiojulikana eneo salama na maeneo jirani kufuatia kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad.
Tulikuwa timu ya watu saba - mimi mwenyewe (raia wa Uingereza), wafanyakazi wawili wa BBC Iraq, na Wasyria wanne - wafanyakazi watatu wa kujitegemea na mpiga picha mmoja wa BBC.
Tulikuwa tukipiga picha karibu na kituo kimoja cha waangalizi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kukabiliana na Uharibifu (UNDOF), karibu na mji wa al-Rafeed, wakati afisa kutoka Umoja wa Mataifa alipotuambia kuwa upande wa Israel ulikuwa umeulizia kuhusu utambulisho wetu na umefahamishwa kuwa sisi ni wafanyakazi wa BBC.
Baadaye tulielekea kaskazini mji wa Quneitra, ambao umekuwa ndani ya eneo salama tangu makubaliano ya mwaka 1974 ya kujitenga kati ya Syria na Israel.
Takriban mita 200 (futi 660) kutoka mjini, katika kituo cha ukaguzi kisichokuwa na ulinzi kilifunga barabara.
Kando ya kituo hicho tuliona vifaru vya Merkava, kimoja kikiwa kinapeperusha bendera ya Israel.
Kutoka kwenye mnara wa karibu, wanajeshi wawili wa Israel walikuwa wakitutazama - mmoja wao kupitia darubini - na mwenzangu akawa ameshikilia kitambulisho chake cha BBC ili kuwaonyesha.
BBC imelalamika kwa jeshi la Israel kuhusu kile kilichotokea baada ya hapo kwa timu yangu, lakini bado haijapata jibu.

Chanzo cha picha, AFP
Dakika moja baada ya kuanza kupiga picha eneo lile, gari jeupe lilikuja kutoka upande wa pili wa kizuizi.
Wanajeshi wanne wa Israel walishuka kwenye gari na kutuzingira.
Walituelekezea bunduki zao vichwani na kutuamuru tuiweke kamera kando ya barabara. Nilijaribu kueleza kwamba sisi tulikuwa wafanyakazi wa BBC, lakini mambo yaliendelea kuwa mabaya bila kutarajia tena kwa haraka mno.
Nilifanikiwa kutuma ujumbe kwa wenzangu wa BBC mjini London kwamba tumezuiliwa na jeshi la Israel kabla ya simu zetu kuchukuliwa na vifaa vyote tulivyokuwa navyo, wanajeshi zaidi wa Israel walifika kwa gari la kijeshi la Humvee, na gari letu likapekuliwa.
Wanajeshi hao walitusindikiza kupitia kizuizi hadi katika jiji la Quneitra na kusimama kwenye kivuko kinachotenganisha Quneitra na Golan inayokaliwa kwa mabavu.
Tukiwa hapo wanajeshi walianza kukagua picha wakati sisi tumeketi kwenye gari letu, huku mmoja akielekeza bunduki yake kichwani kwangu kutoka umbali wa mita kadhaa. Baada ya zaidi ya saa mbili mwanajeshi mmoja alinitaka nishuke kutoka kwenye gari huku akiwa anazungumza na simu.
Sikujua ni nani aliyekuwa akizungumza naye. Aliongea kiarabu cha kuunga unga kisha akaniliuliza kwa nini tunarekodi maeneo ya kijeshi ya Israel.
Nilimwambia mimi ni mwandishi wa habari wa Uingereza wa BBC na nikamweleza kazi yetu ilivyo. Nilirudi kwenye gari langu, na bunduki ikaelekezwa tena kichwani kwangu.
Baada ya saa nyingine ya kusubiri, gari moja zaidi lilifika. Kundi la wanajeshi walishuka kwenye gari wakiwa wamebeba vitambaa vya kufunika macho na tai za plastiki na kuniomba nitoke ndani ya gari kwanza.
Afisa kiongozi, ambaye alizungumza kwa ufasaha lahaja ya Kiarabu ya Kipalestina, alinishika mkono kuelekea kwenye moja ya vyumba vilivyokuwa kwenye kivuko ambacho kitambo kilikuwa kikitumiwa na jeshi la Syria. Sakafu ilikuwa imetapakaa vioo vilivyovunjika na takataka.
Aliniambia kuwa watanichukulia tofauti na wenzangu - sitafungwa pingu wala kufungwa macho - tofauti na wengine.
Nilikuwa katika mshtuko. Nikamuuliza kwa nini walikuwa wanafanya hivi wakati walijua sisi ni wafanyakazi wa BBC.
Alisema alitaka kutusaidia kututoa nje haraka na kwamba tulipaswa kufuata maagizo yao.
Baada ya mengi kufanyika ndani ya takriban saa saba tangu tulipozuiliwa - tulichukuliwa na magari mawili, moja mbele ya gari letu na jingine nyuma yetu, hadi eneo la kijijini karibu kilomita 2 (maili 1.2) nje ya Quneitra.
Huko, magari yalisimama na begi lenye simu zetu likatupwa kuelekea kwetu kabla ya magari kuondoka.
Tukiwa tumepotea hatujui tuendako wala tutokako, tuliendelea kuendesha gari hadi tukafika kwenye kijiji kidogo.
Kikundi cha watoto kilituelekeza kwenye barabara kuu, na kutuonya kwamba tukishika njia nyingine tu, kuna uwezekano wa upande wa Israel kufyatua risasi.
Dakika kumi za mshtuko zilizofuata, tuliona barabara. Dakika arobaini na tano baada ya hapo, tulikuwa Damascus.
Soma zaidi:
Mfanyikazi wa waziri mkuu ashtakiwa kwa kurekodi wanawake kwa siri

Chanzo cha picha, Michael Forbes/LinkedIn
Mfanyakazi wa Waziri Mkuu wa New Zealand Christopher Luxon amejiuzulu baada ya kushutumiwa kwa kupiga picha na video za wanawake kwa siri, na kurekodi sauti za wafanyabiashara ya ngono.
Michael Forbes, naibu katibu mkuu wa waandishi wa habari wa Luxon, aliomba "radhi kwa wanawake ambao nimewadhuru".
Madai hayo yalifichuliwa baada ya mfanyabiashara wa ngono kusema aligundua kuwa simu ya Forbes ilikuwa ikirekodi sauti alipokuwa akioga, tovuti ya habari ya eneo hilo Stuff iliripoti mapema wiki hii.
Baadaye simu yake iligundulika kuwa na picha na video zaidi za wanawake pamoja na sauti zilizorekodiwa za ngono.
Kulikuwa na picha za wanawake kwenye ukumbi wa mazoezi na kwenye duka kubwa, Stuff NZ iliripoti , pamoja na video nne za wanawake majumbani mwao, na picha hizo zilichukuliwa mtu akiwa dirishani.
Luxon alisema kesi ya Forbes ilipokelewa kwa "mshtuko mkubwa" na kwamba "hakustahimili kabisa kuwa na tabia yoyote ambayo inawafanya wanawake au mtu yeyote kuhisi kutokuwa salama".
"Niko pamoja na wanawake walioibua madai haya na ambao walifanywa kuhisi hawako salama kutokana na vitendo vya mtu huyu," alisema Alhamisi, siku moja baada ya Forbes kujiuzulu.
Pia unaweza kusoma:
Jeshi la Israel laipata miili miwili ya mateka kusini mwa Gaza

Chanzo cha picha, Hostages and Missing Families Forum
Maelezo ya picha, Judi Weinstein Haggai na mumewe Gadi Haggai waliuawa wakati wa shambulio la Kibbutz Nir Oz. Wanajeshi wa Israel wameipata miili ya Waisraeli wawili waliorudishwa Gaza kama mateka wakati wa shambulio lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, jeshi la Israel linasema.
Judi Weinstein Haggai, 70, ambaye pia alikuwa raia wa Canada, na mumewe Gadi Haggai, 72, waliuawa na watu wenye silaha kutoka kundi la Mujahideen Brigades waliposhambulia Kibbutz Nir Oz, taarifa ilisema.
Miili yao iliopolewa kutoka eneo la kusini la Khan Younis huko Gaza na kurejeshwa Israel kwa utambuzi wa kitaalamu.
Sasa kuna mateka 56 ambao bado wanazuiliwa na Hamas huko Gaza, na takriban 20 kati yao wanaaminika kuwa hai.
Unaweza pia kusoma:
Hatua zilizochukuliwa na Saudi Arabia katika Hijja ya mwaka huu

Chanzo cha picha, Getty Images
Zaidi ya Waislamu milioni 1.4 wanatekeleza ibada ya Hija katika mji mtakatifu wa Mecca nchini Saudi Arabia mwaka huu, baada ya mwaka mmoja ambapo watu 1,300 walifariki, wengi wao kutokana na joto kali.
Mamlaka za Saudia zilisema zimeongeza tahadhari za usalama kwa mahujaji. Wamepanda maelfu ya miti na kuweka mamia ya viyoyozi katika sehemu mbali mbali za ibada ili kusaidia kupunguza halijoto kali huko.
Serikali ya Saudi Arabia pia imeweka marufuku ya kupeleka watoto walio chini ya umri wa miaka 12 na kuonya kuwa watu watakaojaribu kuhiji kinyume cha sheria bila kibali rasmi watakabiliwa na faini ya dola 5,000 na kupigwa marufuku kwa miaka 10 kuingia Saudi Arabia.
Unaweza pia kusoma:
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yapiga marufuku kuripoti habari za rais wa zamani Josep Kabila

Chanzo cha picha, reuters
Maelezo ya picha, Joseph Kabila amerejea DRC baada ya kuondoka nchini kwa hiari mwaka 2023 Serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC) imevipiga marufuku vyombo vya habari kuripoti shughuli za Rais wa zamani Joseph Kabila na kuwahoji wanachama wa chama chake.
Haya yanajiri baada ya Kabila kurejea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwezi uliopita huku akiwa na mvutano mkali kati yake na serikali, inayoongozwa na mrithi wake, Rais Félix Tshisekedi.
Mamlaka zinashinikiza kumfungulia mashtaka Bw Kabila huku kukiwa na tuhuma za uhaini na madai ya kuwa na uhusiano na waasi wa M23 ambao wamekuwa wakipigana na jeshi - jambo ambalo amelikanusha hapo awali.
Ukiukaji wa marufuku hiyo unaweza kusababisha kusimamishwa, alisema mkuu wa udhibiti wa vyombo vya habari nchini DRC, Christian Bosembe.
Ikijibu tangazo la taasisi hiyo, msemaji wa M23 alisema vyombo vya habari katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wake havitatii marufuku hiyo.
Unaweza pia kusoma:
Chama tawala nchini Burundi chaazimia kuendelea kubaki mamlakani

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Chama tawala cha CNDD-FDD kimekuwa madarakani kwa miaka 20 Wapiga kura nchini Burundi wanaelekea kupiga kura huku kukiwa na ongezeko la mfumuko wa bei, uhaba wa mafuta na malalamiko ya ukandamizaji wa kisiasa.
Viti katika Bunge la Kitaifa na mabaraza ya mitaa vinawaniwa lakini Évariste Ndayishimiye yuko salama katika nafasi yake kama rais kwa kuwa anahudumu kwa muhula wa miaka saba unaomalizika 2027.
Uchaguzi huo utapima umaarufu wa chama tawala cha CNDD-FDD, kikundi cha waasi cha zamani ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 20 iliyopita.
Taifa hilo la Afrika Mashariki tayari ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, lakini wakazi wa huko wamewekewa shinikizo zaidi na ongezeko la bei ya bidhaa kama vile chakula hivi karibuni.
Vyama vya upinzani vimelalamika kuwa wafuasi wao wamekuwa wakinyanyaswa na kutishwa na wanachama wa vuguvugu la vijana wa CNDD-FDD, Imbonerakure.
Gabriel Banzawitonde, kiongozi wa chama cha APDR, alisema: ''Watu wanaogopa sana hadi wanakuambia hawawezi kuvaa rangi za chama chochote isipokuwa zile za chama tawala'.
Unaweza pia kusoma:
Shahidi asema Sean "Diddy" Combs alimning'iniza kwenye roshani ya ghorofa

Chanzo cha picha, Reuters
Mbunifu wa picha Bryana Bongolan ametoa ushahidi mahakamai kwamba Sean "Diddy" Combs aliwahi kumning'iniza kwenye roshani ya ghorofa ya 17, na kwamba alimwona akimrushia kisu rafiki yake Casandra Ventura.
Siku ya Jumatano, waendesha mashtaka walionyesha picha zilizopigwa na Bi Bongolan na Diddy ambaye alikuwa mpenzi wake wa wakati huo za michubuko ya Bi Bongolan, ambayo alidai kuwa aliipata wakati wa tukio hilo linachodaiwa kutokea mwaka 2016.
Mawakili wa Combs walielezea kuwa na mashaka ya uaminifu wa Bi. Bongolan.
Combs anakabiliwa na mashtaka ya ulaghai, kula njama na biashara ya ngono. Amekana kuhusika na hatia yoyote.
Kesi hiyo ya serikali, ambayo sasa iko katika wiki ya nne ya ushuhuda, ilifuatia kesi kadhaa za madai zilizowasilishwa dhidi yake na wanaume na wanawake wakimtuhumu kwa unyanyasaji, akiwemo Bi Ventura, ambaye ni mpenzi wa zamani wa Combs, na Bi Bongolan.
Unaweza pia kusoma:
Ni nani ambaye ameondolewa kwenye marufuku ya kusafiri na Trump?
Marufuku kuu ya Trump ya kusafiri ina mambo ya kipekee.
Kulingana na tangazo lake, hawa hapa ni baadhi ya watu ambao bado wanaweza kuingia Marekani:
- Wanariadha wanaosafiri kwa hafla kuu za michezo, kama vile Kombe la Dunia au Olimpiki
- Wanaomiliki "viza za wahamiaji kwa makabila madogo na wafuasi wa dii wanaokabiliwa na mateso nchini Iran"
- Raia wa Afghanistan walio na vizaa Maalum ya Wahamiaji
- "Mkazi halali wa kudumu" wa Marekani
- Raia wawili ambao wana uraia katika nchi ambazo hazijajumuishwa katika marufuku ya kusafiri
Kwa kuongeza, Waziri wa Mambo ya Nje anaweza kutoa msamaha kwa watu binafsi kwa msingi wa "kisa na kisa", ikiwa "mtu huyo atatumikia maslahi ya kitaifa ya Marekani".
Unaweza pia kusoma:
Trump asaini marufuku ya kusafiri kwenda Marekani dhidi ya raia wa nchi 12

Chanzo cha picha, Getty Images
Donald Trump ametia saini tangazo la kupiga marufuku kusafiri kwenda Marekani dhidi ya raia wanaotoka nchi 12, akitaja hatari za usalama wa kitaifa, kulingana na Ikulu ya White House.
Nchi hizo ni Afghanistan, Myanmar, Chad, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Equatorial Guinea, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen.
Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia Jumatatu, tarehe 9 Juni.
Hatua hiyo ya Trump imepingwa na mataifa yaliyoathiriwa.
Venezuela ni mojawapo ya nchi saba zilizoathiriwa na vikwazo vya sehemu.
Waziri wa Mambo ya Ndani Diosdado Cabello ameonya kuwa "kuwa nchini Marekani ni hatari kubwa kwa mtu yeyote, si kwa raia wa Venezuela pekee".
"Watu wanaotawala Marekani ni watu wabaya - ni mafashisti, ni watu wa itikadi kali ambao wanadhani wanamiliki dunia na kuwatesa watu wetu bila sababu", aliongeza.
Wakati huo huo, Somalia - ambayo sasa raia wake wapigwa marufuku kusafiri - imejibu kwa kuahidi mara moja kufanya kazi na Marekani kushughulikia masuala ya usalama.
Katika taarifa, balozi wa Somalia nchini Marekani, Dahir Hassan Abdi, anasema nchi yake "inathamini uhusiano wake wa muda mrefu" na Marekani.
Unaweza pia kusoma:
Putin atalipiza kisasi kwa shambulio la ndege zisizo na rubani za Ukraine, aonya Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Wito wa Trump na Putin ulikuwa wa kwanza tangu shambulio kubwa la Ukraine dhidi ya ndege za kubeba makombora ndani kabisa ya Urusi Vladimir Putin amesema atalazimika kujibu shambulio kubwa la ndege zisizo na rubani za Ukraine dhidi ya vituo vya anga vya Urusi, Rais wa Marekani Donald Trump ameonya.
Akizungumza baada ya kupigiwa simu na rais wa Urusi, Trump alisema: "Rais Putin alisema, na kwa nguvu sana, kwamba atalazimika kujibu mashambulizi ya hivi majuzi kwenye viwanja vya ndege."
Maafisa wa Urusi walikataa kuthibitisha hili Jumatano usiku, lakini Moscow ilikuwa imesema hapo awali kuwa chaguzi za kijeshi "ziko mezani" kwa majibu yake.
Trump alionya katika chapisho la mtandao wa kijamii kwamba simu hiyo, iliyochukua zaidi ya saa moja, "haitaleta amani ya haraka" kati ya Urusi na Ukraine.
Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Urusi- RIA Novosti, lilisema Putin alimwambia Trump kwamba Ukraine imejaribu "kuvuruga" mazungumzo na kwamba serikali ya Kyiv "kimsingi imegeuka kuwa shirika la kigaidi".
Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yanakuwa ya kwanza tangu Ukraine ilipofanya mashambulizi ya kushtukiza kwa kutumia ndege zisizo na rubani kushambulia vituo vya anga vya Urusi tarehe 1 Juni, yakilenga kile ilichosema kuwa ni washambuliaji wa masafa marefu wenye uwezo wa nyuklia.
Trump alimwambia Putin katika mazungumzo ya njia ya simu kwamba Marekani haikuonywa mapema kuhusu shambulio hilo, msaidizi wa rais wa Urusi Yury Ushakov alisema.
Wito wa Trump na Putin ulikuwa wa kwanza tangu shambulio kubwa la Ukraine dhidi ya ndege za kubeba makombora ndani kabisa ya Urusi
Vladimir Putin amesema atalazimika kujibu shambulio kubwa la ndege zisizo na rubani za Ukraine dhidi ya vituo vya anga vya Urusi, Rais wa Marekani Donald Trump ameonya.
Akizungumza baada ya kupigiwa simu na rais wa Urusi, Trump alisema: "Rais Putin alisema, na kwa nguvu sana, kwamba atalazimika kujibu mashambulizi ya hivi majuzi kwenye viwanja vya ndege."
Maafisa wa Urusi walikataa kuthibitisha hili Jumatano usiku, lakini Moscow ilikuwa imesema hapo awali kuwa chaguzi za kijeshi "ziko mezani" kwa majibu yake.
Trump alionya katika chapisho la mtandao wa kijamii kwamba simu hiyo, iliyochukua zaidi ya saa moja, "haitaleta amani ya haraka" kati ya Urusi na Ukraine.
Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Urusi- RIA Novosti, lilisema Putin alimwambia Trump kwamba Ukraine imejaribu "kuvuruga" mazungumzo na kwamba serikali ya Kyiv "kimsingi imegeuka kuwa shirika la kigaidi".
Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yanakuwa ya kwanza tangu Ukraine ilipofanya mashambulizi ya kushtukiza kwa kutumia ndege zisizo na rubani kushambulia vituo vya anga vya Urusi tarehe 1 Juni, yakilenga kile ilichosema kuwa ni washambuliaji wa masafa marefu wenye uwezo wa nyuklia.
Trump alimwambia Putin katika mazungumzo ya njia ya simu kwamba Marekani haikuonywa mapema kuhusu shambulio hilo, msaidizi wa rais wa Urusi Yury Ushakov alisema.
Unaweza pia kusoma:
Hujambo na karibu tena kwa matangazo haya ya mubashara ya leo tarehe 05.06.2025, tukikuletea habari za kikanda na kimataifa
