Marekani yaja na 'programu ya simu inayoondoa wahamiaji kwa hiari

rf

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Programu ya CBP One inalengwa upya ili kuruhusu wahamiaji wasio na hati kujiondoa.
    • Author, Bernd Debusmann Jr
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Utawala wa Donald Trump umebadilisha matumizi ya programu ya simu ya mkononi inayohusu maombi ya hifadhi – na kuifanya kuwa ya wahamiaji wasio na vibali vya kuishi Marekani ambao wanapaswa kuondoka.

Programu hiyo, inayojulikana kama CBP Home, inawaruhusu wahamiaji kusajili "dhamira yao ya kuondoka," ambapo Idara ya Forodha na Doria ya Mipaka ya Marekani, inasema inawapa nafasi ya kuondoka bila ya kuondoshwa kwa nguvu.

Maafisa wa Marekani wameendelea kusema mara kwa mara kwamba wahamiaji wasio na vibali nchini humo wanapaswa kuondoka kwa hiari, badala ya kukamatwa na kufukuzwa.

Hii ni hatua ya hivi punde zaidi katika juhudi za Ikulu ya White House ya kurekebisha mfumo wa uhamiaji wa Marekani, ili kuendana na ahadi za Trump, ikiwemo kuwahamisha watu wengi kwa nguvu.

Hapo awali programu hiyo ikiitwa CBP One ilipozinduliwa mwaka 2020. Ni programu inayopatikana katika simu ya mkononi, iliyozinduliwa wakati wa utawala wa Biden ili kuruhusu wahamiaji watarajiwa kuweka miadi ya kuwasili kwenye bandari ya kuingilia.

Wakati huo, maofisa walisifu programu hiyo kwa kusaidia kupunguza watu kushikiliwa katika mpaka na kuielezea teknolojia hiyo kama sehemu ya juhudi za kuwalinda wanaotafuta hifadhi, ambao husafiri katika safari hiyo hatari.

Kwa sasa programu hiyo iliyopewa jina jipya, wahamiaji wasio na vibali wanajitambulisha na kutangaza dhamira yao ya kuondoka nchini Marekani.

Katika taarifa yake, Katibu wa Usalama wa Ndani, Kristi Noem amesema kwa kuondoka wenyewe nchini kupitia programu hiyo, wahamiaji "watakuwa na fursa ya kurejea kisheria katika siku zijazo na kuishi Marekani."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Ikiwa hawatafanya hivyo, tutawatafuta, tutawafukuza na hawatarejea tena," aliongeza.

Programu pia inawauliza wahamiaji kama wana "fedha za kutosha kuondoka Marekani" na ikiwa wana "pasipoti halali, ambayo muda wake haujaisha kutoka nchi yao ya asili."

BBC imewasiliana na DHS kwa maelezo zaidi kuhusu jinsi mchakato huo unavyofanya kazi, baada ya wahamiaji kujaza fomu zilizo kwenye programu hiyo.

Utawala wa Trump ulifanya haraka kufuta programu ya CBP One kama sehemu ya mabadiliko katika sera zake za uhamiaji. Pia ilisitisha ruhusa kwa wahamiaji wasio na vibali kuingia Marekani, na kuongeza kamatakamata ya wahamiaji kupitia Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE).

Takriban watu 30,000 walisemekana kukwama ndani ya Mexico tangu programu hiyo ilipoondolewa - wote wakiwa na miadi ambayo sasa imeghairishwa.

Kabla ya agizo hilo, wahamiaji waliweza kufika kwenye mpaka wa Marekani na walikuwa na haki ya kisheria ya kuomba hifadhi.

Trump pia amesitisha mpango wa kuwapatia wakimbizi makazi mapya Marekani. Chini ya utawala wa Joe Biden mwaka 2024, Marekani ilikubali zaidi ya wakimbizi 100,000 - idadi kubwa zaidi tangu 1995.

Pia unaweza kusoma
EC

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwishoni mwa Februari, utawala wa Trump ulisema utaunda daftari la kitaifa kwa wahamiaji wasio na hati na ambao watashindwa kujiandikisha wanaweza kukabiliwa na mashtaka ya jinai.

Kuna takriban wahamiaji milioni 13 wasio na vibali nchini Marekani. Haijulikani ni wangapi watasajili au wataathiriwa na agizo la usajili.

Usajili huo unahitaji wahamiaji wote wasio na hati walio na umri wa zaidi ya miaka 14 kutoa anwani ya makazi na alama za vidole kwa serikali ya Marekani.

Wataalamu wanasema mfumo huo wa usajili utakabiliwa na vikwazo, kwani ni vigumu kuutekeleza na unakabiliwa na changamoto za vifaa.

Takwimu za ICE zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 1,000 waliondolewa au kurudishwa makwao siku ya nne tu tangu Trump aingie madarakani.

Takwimu zilizopatikana na shirika la habari la Reuters zinaonyesha karibu watu 38,000 walifukuzwa wakati wa mwezi wa kwanza wa Trump ofisini, ikilinganishwa na wastani wa kila mwezi wa takriban 57,000 wakati wa mwaka mzima wa mwisho wa Joe Biden.

Ikulu ya White House imesherehekea kupungua kwa 36% kwa idadi ya watu wanaovuka mpaka hadi Januari 2025 ikilinganishwa na Desemba 2024.

Kwa jumla, Biden alifukuza watu milioni 1.5 katika miaka yake minne, kulingana na takwimu za Taasisi ya Sera ya Uhamiaji. Hiyo ni sawa na ile iliyotekelezwa chini ya muhula wa kwanza wa Trump.

Idadi hiyo ni ndogo kuliko ufurushaji uliofanywa chini ya muhula wa kwanza wa Barack Obama, ambao jumla ilikuwa ni watu milioni 2.9.

Wengi wa wahamiaji wanakimbia machafuko ya kisiasa au ghasia za uhalifu katika nchi zao, na kurudishwa kwao kunazusha maswali ikiwa watakuwa salama watakapo rejea.