Mambo matano ambayo huenda hukuyajua kuhusu Hijja

Chanzo cha picha, Getty Images
Hijja ni ibada takatifu kwa waumini wa dini ya Kiislamu na takriban watu milioni mbili huzuru mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia kila mwaka kufanya ibada ya Hajj.
Ni moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu na kila Muumini aliye na uwezo anatarajiwa kuitimiza kwenda kuhiji walau mara moja katika kipindi cha maisha yake.
Hijja ni wapo ya mikusanyiko mikubwa ya kila mwaka duniani inayovutia waumini kutoka pembe zote za ulimwengu. Makka ndio mahali alipozaliwa Mtume Muhammad (SAW) na eneo ambalo alipokea ufunuo wa kwanza wa Kitabu Takatifu, Quran.
Pia ndiko kunapopatikana Kaaba, jengo lenye umbo la mchemraba lililofunikwa kwa kitambaa cheusi ambalo liko katikati ya Masjid al-Haram, linalojulikana pia kama Msikiti Mtakatifu au Msikiti Mkubwa wa Makka, ambao unachukuliwa kuwa mahali patakatifu zaidi katika Uislamu.
Yajue mambo matano ya kipekee kuhusu ibada ya Hijja ambayo huenda hukuyajua.
Kaaba - Urithi wa Nabii Ibrahim
Ibada ya Hija ya kila mwaka ni moja ya nguzo za Uislamu, yenye kuhusishwa na Mtume Muhammad (SAW), mwanzilishi wa dini hiyo.

Chanzo cha picha, EPA
Hata hivyo, ibada hiyo ilianzia wakati wa Nabii Ibrahim, ambaye inaaminika ndio chanzo cha jengo la Kaaba, kulingana na Imani ya Kiisilamu.
Tamaduni za Hijja zinaadhimisha kipindi ambapo nusra Nabii Ibrahim amchinje mwanawe akimtii Mwenyezi Mungu - kitendo cha kujitolea ambacho kilimalizika kwa Mungu kuingilia kati.
Nabii Ibrahim, anayejulikana kama Abrahamu katika Ukristo na Uyahudi, pia ni kiungo muhimu katika imani hizo zote mbili.
Hakuna kutengwa kwa misingi ya kijinsia

Chanzo cha picha, Yassine Gaidi/Anadolu Agency
Tofauti na ibada zingine za Waislamu ambapo kila jinsia hufanya ibada ikiwa sehemu yake kama vile kutumia milango tofauti au kusali kwenye maeneo tofauti msikitini, hakuna ubaguzi wa kijinsia kati ya wanaume na wanawake wakati wa ibada ya Hijja.
Mavazi ya kipekee
Mahujaji wanaofanya ibada ya Hijja hufuata miongozo maalum ya mavazi ambayo yanaonyesha usawa wa kiroho na unyenyekevu.

Chanzo cha picha, EPA
Mahujaji wa kiume huvaa vazi jeupe, lisilo na mshono, linaloitwa Ihram, kuashiria usawa wa waumini wote, bila kujali hali ya kijamii au kiuchumi.
Mahujaji wa kike hawavai mavazi meupe kama ya wanaume, lakini wanaweza kuvaa mavazi yoyote yasiyowabana, ya kawaida tu ambayo yanawastiri.
Wanapaswa kufunika vichwa vyao kwa hijab, lakini nyuso zao zinapaswa kusalia wazi wakati wa Hijja.
Kupanda mlima
Mojawapo ya ibada maarufu za Hijja ni Tawaf, ambapo mahujaji huzunguka Kaaba mara saba - mwanzoni na mwisho wa ibada ya Hijja.
Lakini je! ulijua kuwa ibada nyingine muhimu inajumuisha kutembea kati ya vilima viwili?
Sehemu ya ibada ya Hijja ni pamoja na kuzuru na kutembea mara saba kati ya vilima vya Safa na Marwah, vilivyo ndani ya Masjid al-Haram.
Inachukuliwa kuwa kitendo cha kukumbuka changamoto na uvumilivu wa Hajar, mke wa Nabii Ibrahim, ambaye alikimbia kati ya vilima hivyo viwili akitafuta maji kwa ajili ya mtoto wake mchanga.
Kilele cha Mlima Arafat
Wakati Kaaba ndio msingi wa ibada ya Hijja, kilele chake hufanyika huko Mlima Arafat, bonde la jangwa lililo nje ya Makka.

Chanzo cha picha, EPA
Hapa, umati mkubwa wa waumini hukusanyika kuanzia jua linachomoza hadi linapotua huku wakifanya sala, kutafakari, na kusoma tena na tena Quran.
Maeneo haya takatifu yana umuhimu mkubwa katika Uislamu. Kulingana na imani ya Kiisilamu ni mahali ambapo Mtume Muhammad alitoa mahubiri yake ya mwisho.















