Je, unakifahamu kisima cha kale ambacho Waislamu wanaamini maji yake ni matakatifu?

Wanaume wa Saudia wakiwapatia mahujaji maji ya Zamzam

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanaume wa Saudia wakiwapatia mahujaji maji ya Zamzam
    • Author, Jannatul Tanvi
    • Nafasi, BBC News Bangla

Kisima cha Zamzam kiko ndani ya Msikiti Mkuu au Masjid al-Haram mjini Makka, Saudi Arabia. Ndio msikiti mkubwa zaidi duniani na ndani yake kuna sehemu takatifu zaidi ya Uislamu, Kaaba.

Maji yanayotoka kwenye kisima hicho yanachukuliwa kuwa matakatifu na mamilioni ya Waislamu ulimwenguni kote na inaaminika kuwa na nguvu za uponyaji.

Kukizuru kisima hicho ni jambo muhimu kwa wanaofika Makka na karibu mahujaji wote wanarudi nyumbani na maji kutoka kwenye kisima hiki. Maji hayo mara nyingi husambazwa miongoni mwa wanafamilia na marafiki, kwa imani kwamba yanaweza kuepusha hatari, magonjwa, na uovu. Pia inaaminika kuwa maji yenyewe ni muujiza, kutokana na chemichemi yake isiyo na mwisho.

Takriban watu milioni mbili wanatarajiwa kuwasili mjini Makka kwa ibada ya hija kutoka sehemu mbalimbali za dunia kila mwaka. Hata hivyo, inakadiriwa kuwa idadi ya watu wanaohudhuria hija ni kubwa zaidi, kwani si wageni wote walioandikishwa na wengi wao ni wenyeji au wanasafiri kwa bahari na nchi kavu kutoka nchi jirani.

Maelezo zaidi:
Maafisa wanatoa maji ya Zamzam kwa mahujaji watarajiwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mahujaji hunywa maji baada ya kuzunguka Kaaba

Kwanini maji ya Zamzam ni muhimu kwa Waislamu?

Maji haya ni muhimu kwa Waislamu kwa sababu yamejikita sana katika masimulizi ya kihistoria na kidini. Mwanachuoni wa Kiislamu Imam Bukhari Abdullah Ibn Abbas alikusanya juzuu sita za hadithi za Mtume Muhammad zinazojulikana kama Sahih al-Bukhari katika mwaka wa 860. Hadithi za mtume zinapewa daraja la pili kwa umuhimu baada ya Quran kama chanzo kikuu cha mwongozo wa kidini na maadili.

Hadithi hizo zinaaminika kuwa ni mkusanyiko wa mwenendo (sunnah) wa Mtume Muhammad, mila na mafundisho ya kibinafsi katika maisha yake yote, kama ilivyosimuliwa na wale waliokuwa karibu naye.

Kwa mujibu wa imani ya Kiislamu, hadithi zinawakilisha mafundisho ya Mtume na kanuni za tabia za kufuata. Uhalali wa vyanzo vya hadithi unatofautiana, hata hivyo, kati ya Waislamu wa Sunni na Shia na baina ya madhehebu mbalimbali ya fikra ndani ya matawi hayo mawili.

Kwa mujibu wa hadithi za Kiislamu, Mwenyezi Mungu alikiumba Kisima cha Zamzam maelfu ya miaka iliyopita ili kujibu maombi ya Hajar, baada ya kuachwa jangwani na mumewe Nabii Ibrahim na mwanawe Ismail jangwani wakiwa hawana chakula wala maji. Tukio hili limeandikwa katika Surah Ibrahim ya Quran na kuangaziwa katika maandishi mbalimbali ya historia ya Kiislamu.

Katika Sahih al-Bukhari, hadithi inaeleza jinsi Hajar, katika utafutaji wake wa maji wa kutokata tamaa, alikimbia mara saba kati ya vilima vya Safa na Marwa mpaka malaika Jibril akapiga ardhi kwa kisigino chake, na kusababisha maji kutiririka. Kwa kuogopa maji huenda yakaisha, inasemekana Hajar alitamka maneno ‘zam zam’ (ambayo ni msemo wa Kiarabu unaomaanisha ‘kusimamisha mtiririko’) mara kadhaa, hivyo kukipa kisima na maji jina lake.

Hujaji akinywa maji ya Zamzam kwenye Msikiti Mkuu katika mji mtakatifu wa Mecca mnamo Juni 25, 2023.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Kundi la lori za mizigo kisha hupeleka maelfu ya lita za maji ya Zamzam kila siku kwenye Bwawa la Mfalme Abdulaziz Sabeel huko Madina.

Je, yanahusiana vipi na Hajj?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Uhusiano wa kihistoria kati ya maji ya Zamzam na hija ni wa kina. Hija ni nguzo ya tano na ya mwisho ya Uislamu. Inafanyika katika mwezi wa Dhul Hijjah, mwezi wa mwisho (12) katika kalenda ya Kiislamu. Mwaka huu, 2024, Dhul Hijjah ilianza wiki ya pili ya Juni na inatarajiwa kukamilika katikati ya Julai. Kila Muislamu mtu mzima ambaye ana uwezo, analazimika (faradhi) kwenda hija angalau mara moja katika maisha yake.

Kuna ziara fupi zaidi ambayo si faradhi katika eneo hilo, na inayohusisha taratibu za hajj kwa ufupi na inaweza kufanywa wakati wowote wa mwaka. Hii inaitwa Umra.

Waislamu wanaamini baada ya kuijenga upya Kaaba, Nabii Ibrahim aliwaalika watu kuhiji kwa amri ya Mwenyezi Mungu anaeleza Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu-Kiarabu cha Bangladesh, Muhammad Abdur Rashid. Ibada za hija ni pamoja na kuzunguka kwa Kaaba inayoitwa Tawaf, na kutembea mara saba kati ya vilima vya Safa na Marwa ijulikanayo kama Sai. Ibada hizi zinahusiana kiuhalisia na hadithi ya Hajar na Kisima cha Zamzam, zinaiga alichofanya wakati wake.

Wakati kunywa maji ya Zamzam si wajibu wa kwa mahujaji, lakini inachukuliwa kuwa sunnah (mila na mafundisho) ya Mtume Muhammad. Mahujaji wengi hunywa maji hayo baada ya kuzunguka Kaaba na kabla ya kutembea kati ya vilima vya Safa na Marwa mara saba.

Mfanyikazi wa Saudia akipakia gari la "zamzam"

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Utafiti wa Jiolojia wa Saudi Arabia unaendesha Kituo cha Mafunzo na Utafiti cha Zamzam

Je, maji ya Zamzam yanauzwa?

Ingawa watalii wanaruhusiwa na kuhimizwa kuchukua maji ya Zamzam kurejea nyumbani, kuyasafirisha nje kwa matumizi ya kibiashara kumepigwa marufuku na Serikali ya Saudia. Licha ya hayo, visa vya maji ya Zamzam kuuzwa kinyume cha sheria nchini Uingereza vimeripotiwa.

Mnamo Mei 2011, uchunguzi wa BBC uligundua viwango vya juu vya madini ya arsenic katika maji ya chupa yanayouzwa kwa chapa ya maji ya Zamzam katika maduka nchini Uingereza. Hii ilisababisha msako wa wauzaji wake haramu, huku mamlaka za Saudia zikiweka udhibiti mkali wa ubora ili kuhakikisha maji hayo ni safi na salama kwa matumizi.

Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia wa Saudi Arabia inaendesha Kituo cha Mafunzo na Utafiti cha Zamzam, ambacho kinasimamia ubora wa maji ya kisima hicho. Maji hayo huchotwa kutoka kwenye kisima kupitia mabomba ya chini ya ardhi hadi kwenye mtambo mkubwa wa kuchuja na kutakasa maji na kuhifadhiwa kwenye tangi kubwa la maki.

Malori ya mizigo kisha husafirisha maelfu ya lita za maji ya Zamzam kila siku mpaka kwenye tangi kubwa la Mfalme Abdulaziz Sabeel huko katika mji waMadinah, na kuhakikisha upatikanaji wa kutosha wa maji hayo kwa Msikiti Mkuu wa Makka na Msikiti wa Mtume wa Madinah.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Athuman Mtulya