Nini ipi hatima ya mahujaji wanaofariki wakati wanapokwenda hijja Makka?

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Hijja ni mojawapo ya nguzo muhimu za Uislamu. Ni moja ya nguzo tano za dini na ni wajibu kwa kila mtu ambaye ana uwezo wa kuhiji kufanya hivyo angalau mara moja katika maisha yake.

Kila mwaka wakati huu, mamilioni ya Waislamu kutoka duniani kote husafiri hadi Makka, Saudi Arabia, mahali patakatifu zaidi katika dini ya Uislamu, kufanya sherehe hii takatifu.

Mara nyingi, baadhi ya watu wanaokwenda safari hii hawarudi wakiwa hai, baadhi yao hufariki kwa sababu moja au nyingine.

Unaweza pia kusoma:

Kwa hivyo ni nini kinatokea wakati watu wanapofariki wakiwa hija Makka? Je, kufariki dunia wakati wa Hijja kuna umuhimu wa kidini?

Ni bahati kufariki dunia kwa ajili ya Hijja - Mtaalamu wa Uislamu

Kwa ujumla, Waislamu hupendelea kuwazika ndugu zao waliofariki katika makaburi ya karibu ili waweze kuwatembelea na kuwaombea dua. Mara nyingi, linapokuja suala la watu wanaofariki mbali na nyumbani, wapendwa wao hutumia gharama nyingi ili tu kurejesha mwili wa mpendwa wao kwa mazishi.

"Sijawahi kuona mtu akifariki kwa ajili ya Hijja na mwili wake kurudishwa," alisema Umar Haruna, mtaalamu wa Uislamu.

“Kwa kweli, ni fursa nzuri kufariki katika nchi takatifu. Hata wazazi wa marehemu, ingawa wanahisi uchungu juu ya kifo cha mpendwa wao, wanakubali maumivu haya kutokana na imani kwamba ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Zaidi ya hayo, Uislamu unaagiza kwamba ni vizuri kuwazika watu waliokufa haraka iwezekanavyo baada ya kifo chao, kwa kawaida Muislamu aliyefariki huzikwa ndani ya saa 24 baada ya kifo.

"Haiwezekani kurudisha mwili wa mhujaji aliyekufa ndani ya saa 24, kwa hiyo tunauzika ndani ya siku moja katika ardhi ya Saudia," anaelezea Haruna.

Wanawazika wapi?

Imam Nurudeen wa Anoda, ambaye amekwenda kushiriki ibada ya Hija mara kadhaa, ameiambia BBC Idhaa ya Pidgin kwamba kuna makaburi kadhaa ambapo mahujaji wanaofariki wakati wa Hija wanaweza kuzikwa.

Baadhi ya makaburi yanayojulikana zaidi ni pamoja na Jannat Al-Mala huko Makka, Jannat Al-Baqi huko Madina, Makaburi ya Al-Adl, Makaburi ya Mashahidi wa Al-Haram, Makaburi ya Al-Rabway na Makaburi ya 'Arafat.

Mnamo mwaka wa 2015, wakati zaidi ya mahujaji 2,000 walipofariki katika mkanyagano uliotokea Mina, mamlaka ya Saudia ilisema walikuwa wametayarisha makaburi ya kutosha katika maeneo ya makaburi sita ili kuwazika waathiriwa.

Je, mazishi hufanyikaje?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Sulaiman Aliyu, mfamasia katika Hospitali ya mafunzo ya Ahmadu Bello huko Zaria, katika jimbo la Kaduna, ameiambia BBC taratibu za kuwazika mahujaji wanaofariki wakati wa Hijja.

Aliyu amekuwa sehemu ya timu ya matibabu ya Hija mara kadhaa.

Anasema: "Kwanza kabisa, yote inategemea mahali ambapo mhujaji alifariki. Huenda akafariki katika hospitali au zahanati ya Nigeria, kwa vile NAHCON (Tume ya Kitaifa ya Hija ya Nigeria) ina kliniki yake katika nchi takatifu, au anaweza kufia katika chumba chake cha hoteli.

"Iwapo msafiri atafariki hospitalini, wakuu wa hospitali huandaa ripoti na kuipeleka kwa Tume ya Hija ya Nigeria, kisha NAHCON hufahamisha serikali kuwajulisha kilichotokea, kisha huipeleka ripoti hiyo kwa usalama wa Saudia pamoja na Wizara ya Afya ya Saudia na serikali ya Saudia.

“Hii ni kuhakikisha taratibu zote zimefuatwa na wahusika wote wanashirikishwa kabla ya kuendelea na mazishi.

Zaidi ya hayo, Imam Tajudeen anaeleza kuwa utaratibu wa mazishi hauna tofauti na jinsi Mwislamu anavyozikwa katika sehemu yoyote ile ya dunia.

"Kwenye makaburi, imamu huwaongoza watu kuswali swala ya mazishi au Salat al-Janaza, kisha humzika mhujaji aliyekufa," anaeleza.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Je, Hija ina maana gani kwa Waislamu?

Hijja ni nguzo ya tano ya Uislamu. Ni wajibu kwa Waislamu wote wenye uwezo wa kimaumbile na kifedha kuhiji.

Lakini Muislamu anaweza kufanya hivyo kwa sharti tu kwamba kutokuwepo kwake kusilete matatizo kwa familia yake.

Mhujaji anaweza kuhiji kwa kutumia wakala, yaani anaweza kumteua mtu wa familia yake au rafiki kuhiji kwa ajili yake.

Takriban watu milioni mbili hufanya ibada ya Hija nchini Saudi Arabia kila mwaka.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi