Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Kenya 2022: Jinsi mauaji ya afisa wa tume ya uchaguzi IEBC Chris Msando yanavyoendelea kuandama Uchaguzi wa Kenya
- Author, Na Dickens Olewe
- Nafasi, BBC News, Nairobi
Uchaguzi uliotiliwa shaka Pamoja na mauaji ya kutisha ya afisa mkuu aliyesimamia teknolojia ya upigaji kura mwaka wa 2017 bado yanaikera Kenya, kabla ya uchaguzi wiki ijayo.
Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na Mipaka amekuwa akijaribu mara kwa mara kuwahakikishia wananchi wenye wasiwasi kwamba tume yake inaweza kusimamia uchaguzi wa haki, lakini pia amekuwa akionya kuhusu kampeni iliyoratibiwa hasa kwenye mitandao ya kijamii kuwakashifu na kuwatisha wafanyakazi wake.
"Wafanyikazi wetu katika tume, hasa [wale] walio katika kitengo cha teknolojia ICT wana hofu... Ninataka tu kuwasihi wale wanowatisha kuwacha kufanya hivyo'' ,Wafula Chebukati aliwaambia wanahabari.
Ana sababu za msingi za kuwa na wasiwasi: miaka mitano iliyopita mkuu wake wa teknolojia wakati huo, Chris Msando, alitekwa nyara na kuuawa kikatili, pamoja na rafiki yake Carol Ngumbu mwenye umri wa miaka 21.
Miili yao ilipatikana vichakani viungani mwa mji mkuu, Nairobi - na hakuna mtu aliyekamatwa au kushtakiwa kwa mauaji hayo ambayo yamegubikwa na siri.
"Hakika tukiwa na huduma ya polisi yenye utaalamu wa juu na serikali yenye weledi na ufanisi nadhani tungefaa kujua ukweli kuhusu tukio hili ... Taifa halijui ni nani aliyechukua maisha ya afisa wa uchaguzi ambaye alikuwa akishughulikia sehemu nyeti sana ya uchaguzi," alisema Mkurugenzi mkuu wa shirika la haki za kibinadamu la Amnesty International Kenya akizungumza na kituo kimoja cha runinga nchini humo.
Kwa urafiki na utulivu, Msando alikuwa akitangaza katika vituo vya runinga vya hapa nchini, akionyesha hatua alizochukua kuhakikisha uchaguzi hauibiwi.
"Wapiga kura waliokufa hawatafufuka chini ya usimamizi wangu ," alisema katika mahojiano.
Alikuwa ameweka imani yake katika data za kibayometriki ili kuthibitisha wapiga kura kwa kutumia alama za vidole na mfumo wa kielektroniki kusambaza matokeo.
Utumiaji wa teknolojia kama hiyo ulikubaliwa kufuatia kudorora kwa uchaguzi wa 2007 wakati shutuma za ujazo wa kura zilizusha ghasia za wiki kadhaa ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 600,000 kutoroka makazi yao. Wakati huo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wakati huo alikiri hakuwa na uhakika ni nani aliyeshinda.
Uchaguzi huu pia unaonekana kuwa kinyang'anyiro kikali cha urais - kati ya vinara Raila Odinga, kiongozi wa upinzani wa muda mrefu ambaye anawania kwa mara yake ya tano, na Naibu Rais William Ruto.
"Teknolojia sio demokrasia"
Kufanya mambo kuwa makubwa zaidi, Rais anayeondoka Uhuru Kenyatta anamuunga mkono Bw Odinga, ambaye ni adui aliyegeuka kuwa mshirika wake, kumrithi kufuatia kuvunjika kwa uhusiano wake na Bw Ruto.
Wapiga kura pia watakuwa wakichagua magavana, maseneta, wabunge na madiwani wa bunge la kaunti.
Hata hivyo ongezeko la matumizi ya teknolojia katika kura tatu za uchaguzi tangu 2007 halijatoa uaminifu - na mwaka wa 2017 ilisababisha Mahakama ya Juu kubatilisha kura hiyo na kuamuru uchaguzi mpya.
"Licha ya kushindwa mwaka wa 2013, teknolojia zaidi ilinunuliwa mwaka wa 2017. Gharama ya uchaguzi ilipanda kutoka $10 [£8] kwa kila mpiga kura aliyejiandikisha katika uchaguzi wa kwanza hadi $25 katika uchaguzi wa marudio, na hivyo kuifanya Kenya kuwa na umaarufu wa kuandaa uchaguzi ghali zaidi barani Afrika," Nanjira Sambuli, mchambuzi wa teknolojia na utawala aliambia BBC.
"Teknolojia sio demokrasia," Bi Sambuli alisema.
Mahakama ya Juu iliamua kwamba kura hiyo ya Agosti 2017 ni "batili, batili na batili" kwani baadhi ya vituo 10,000 vilishindwa kusambaza kura.
"Hii ilikuwa idadi kubwa, pamoja na tume ya uchaguzi ilitoa visingizio walivyopotakiwa kufungua sava za kompyuta kwa ajili yakuangazia kile kilichotokea,Wakili wa kikatiba James Mamboleo aliambia BBC.
"Walisema tume lazima iwajibike kwa wananchi katika michakato yote kuanzia uandikishaji wapigakura hadi mfumo madhubuti wa usambazaji."
Uamuzi huo ulidhoofisha imani na Bw Chebukati, lakini alifaulu kusalia kazini licha ya shinikizo la kumtaka ajiuzulu.
Wakati huu tume itatumia tena makumi ya maelfu ya vifaa vya kuthibitisha wapigakura vilivyonunuliwa kwa marudio ya uchaguzi wa Oktoba 2017 na imeimarisha taratibu zake.
Watu ambao wanaweza kuthibitishwa na mfumo wa kielektroniki pekee ndio watakaopiga kura na picha ya matokeo itatumwa kidijitali kutoka zaidi ya vituo 50,000 vya kupigia kura badala ya ujumbe mfupi wa maandishi.
Hivi ndivyo itakavyofanya kazi kwa kura ya urais:
• Wapiga kura wote watalazimika kuthibitishwa kwa kutumia alama ya vidole au kitambulisho
• Baada ya upigaji kura kufungwa, picha ya fomu ya matokeo, iliyotiwa saini na afisa msimamizi na mawakala wa vyama, itasambazwa kwa njia ya kielektroniki kwa kutumia vifaa vilivyounganishwa vya kupigia kura kwa jimbo na kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura.
• Nakala ya fomu itatolewa kwa mawakala wa vyama na kubandikwa nje ya kituo cha kupigia kura
• Vifaa vya uthibitishaji wa wapigakura vitafungwa katika vituo vya kupigia kura ili kuzuia udanganyifu
• Mshindi atatangazwa tu baada ya fomu halisi ya matokeo kupokelewa na tume ili kuthibitisha dhidi ya picha iliyotumwa mwanzoni.
"Itakuwa vigumu sana katika uchaguzi huu watu waende mahakamani kupinga matokeo tuliyonayo, kwa sababu tuko wazi kiasi kwamba hata wakitaka kwenda mahakamani wangefedheheka sana. "Mmoja wa makamishna wa tume ya uchaguzi, Justus Nyangaya, aliambia BBC.
Pia alisema kuwa kitambulisho cha wapigakura kitakuwa kikituma taarifa kwenye kituo cha kitaifa cha kujumlisha kura kila baada ya saa mbili, jambo ambalo anasema litapuuza majaribio ya kujaza masanduku ya kura.
Akiwa bado anaonekana kuumizwa na uchaguzi uliopita, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi pia amevitaka vyombo vya habari, vyama vya siasa na jumuiya za kiraia kufanya majumuisho yao ya kura.
"Chebukati ana nia ya kufanya marekebisho kwa kuwajibika kikamilifu kama mwenyekiti, na kuanzisha mfumo ambao utahakikisha uchaguzi huru, wa haki, wazi na unaoweza kuthibitishwa ili kujiondoa katika urithi wa mwenyekiti anayejulikana kwa chaguzi zenye mkanganyiko," mchambuzi wa kisiasa Hesbon Owila aliambia BBC.
"Kama mtu binafsi amejifunza kutoka zamani, lakini kama Wakenya, tunaweza tu kuunga mkono lakini pia kuwa macho."
Bw Mamboleo anakubali: "Je, tume ya uchaguzi imejaribu kufuata viwango vya juu vilivyowekwa na uamuzi huo wa Mahakama ya Juu wa 2017? Kwa maoni yangu, ni ndiyo. Wameshirikisha vyama vya siasa, wagombea na umma kwa njia ambazo hatujaona. katika chaguzi zilizopita."
Wito wa haki
Kwa mujibu wa sheria, tume ya uchaguzi ina siku saba baada ya kura ya kuwatangaza washindi - na kwa kuhimiza vyombo vya habari na wengine kujumlisha matokeo Bw Chebukati anatumai kuwa uwazi utamhalalisha yeye na tume.
Bila shaka itakuwa hatua muhimu kwa Kenya ikiwa hii ingeafikiwa.
Wakati familia za Msando na Ngumbu zikiadhimisha kumbukumbu ya miaka mitano ya mauaji yao mwezi uliopita, walisema tena demokrasia ya Kenya inapaswa kuegemezwa katika utawala wa sheria - na walitumai siku moja wao pia watapata haki.
"Tunaomba kwamba siku moja tupate kujua ukweli," familia ya Msando iliandika katika kumbukumbu katika moja ya karatasi za ndani.
Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma
UNAYOFAA KUJUA:Uchaguzi Kenya 2022: Je Naibu wa rais wa Kenya William Ruto anakabiliwa na changamoto gani katika kumteua naibu wake wa rais?
WAGOMBEAJI:Wafahamu wagombea 4 wanaowania urais nchini Kenya #