Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Kenya 2022: Wanaotarajiwa kuwa Mama taifa wa Kenya
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
Kenya inapoelekea kwa uchaguzi mkuu macho yanaelekezwa kwa wanawake walio katika maisha ya wagombea wanne wa urais.
Je ni nani kati ya wanawake hawa wanne atachukua mkoba kutoka kwa Margaret Kenyatta kama Mama Taifa wa Kenya?
Tunawaangazia kwa ufupi ili uwajue kwani mmoja wao ndiye atakayekuwa mama wa taifa wa nchi endapo mume wake atachaguliwa kuwa rais wa Kenya .
Ida Odinga
Ni mke wa mwanasiasa mkongwe na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Ida Anyango Oyoo, alizaliwa tarehe 27 Agosti, 1950, katika kaunti ya Migori Magharibi mwa Kenya.
Ida alikutana kwa mara ya kwanza na mume wake Raila Amollo Odinga alipokuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Aliolewa na Bw Odinga tarehe 1 Septemba 1973 na katika ndoa yao walijaaliwa watoto wanne, Fidel Odinga, Winnie Odinga, Raila Odinga Jr na Rosemary Odinga.
Japo kitaaluma Mama Odinga ni mfanyabiashara, mwanaharakati na mwalimu, lakini umaarufu wake zaidi umetokana na jinsi anavyosimama kidete katika harakati za kumuunga mkono bwana Raila Amollo Odinga katika siasa na azma yake ya kuongoza taifa la Kenya.
Kwa miaka mingi, amekuwa akijihusisha katika miradi tofauti ikiwa ni pamoja na kampeni dhidi ya uelewa kuhusu saratani ya matiti na fistula.
Pia amekuwa mshauri wa wanafunzi kadhaa wa kike na pia mdhamini mkubwa katika kujenga maktaba ya kisasa katika shule yake ya zamani ya sekondari.
Mwaka 2021, alipewa tuzo ya kutambua uungaji mkono wake mkubwa katika masuala ya afya, elimu, wanawake, amani, pamoja na uwezeshwaji wa watoto wavulana na wasichana.
Rachel Ruto
Rachel Chebet Ruto ni mke wa Naibu wa Rais wa Kenya William Ruto.
Alizaliwa tarehe 20 mwezi Novemba 1968 mjini Kakamega magharibi mwa Kenya na kupata masomo yake ya sekondari katika shule ya wasichana ya Butere hadi kidato cha sita.
Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta na kusomea shahada ya Elimu.
Bi Rachel na William Ruto walikutana mwanzoni mwa miaka ya tisini na wawili hao walianza kuchumbiana wakiwa chuo kikuu.
Alifunga pingu za maisha na mume wake William Ruto na kuanza familia yao mwaka wa 1991.
Rachel alijaaliwa watoto sita-mabinti watatu na wavulana watatu mkubwa wao akiwa Nick Ruto.
Amekuwa mstari wa mbele kupigania haki za wanawake na harakati za kuwawezesha katika jamii.
Anna Ngibuini Mwaure
Anna Ngibuini Mwaure ni mke wa mgombea wa Urais wa chama cha Agano David Mwaura Waihiga.
Mengi hayajulikani kumhusu kwa sababu ameishi maisha yake kimya kimya, na ni nadra sana kumpata kwenye mijadala ya umma.
Mnamo Juni 2021, alikula kiapo kama jaji wa Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi.
Uteuzi wake ulijiri wakati ambapo Rais Uhuru Kenyatta alichapisha kwenye gazeti rasmi la serikali majaji 34 na kuondoa sita waliopendekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama.
Kabla ya uteuzi wake kama jaji alifanya kazi kama mpatanishi.
Katika taarifa zilizopita zilizochapishwa katika vyombo vya habari nchini humo, Anne amekuwa mtetezi mkali wa kutumia mbinu ya upatanishi wa mizozo baina ya wahusika bila kuwaingiza wahusika zaidi. Alibainisha kuwa njia hii ni nzuri na ya gharama nafuu kinyume na kesi za madai.
Meller Lee Chatham
Bi Chatham ni mke wa mgombea urais George Wajackoyah.
Mengi hayajulikani kumhusu lakini taarifa zilizoangaziwa mtandaoni nchini Kenya zinaonyesha kwamba aliwahi kufanya kazi katika tasnia ya usafiri wa anga.
Alionekana hadharani maajuzi akiwa na mume wake wakati wa mdahalo wa wagombea wa urais ambao Wajackoyah hakushiriki licha ya kufika katika eneo la mdahalo huo na kisha kuondoka .
Katika mahojiano yaliyopita na vyombo vya habari nchini Kenya mume wake Bw Wajackoyah alisema mke wake anaishi Marekani na watoto wao watatu - mabinti wao wawili na mwana wao wa kiume.
Pia unaweza pia kusoma