Vita vya Ukraine: Urusi yaishutumu Uingereza kwa kuchochea mashambulizi kwenye ardhi yake

Chanzo cha picha, Reuters
Serikali ya Urusi imeishutumu Uingereza kwa "kuichochea" Ukraine kushambulia eneo la Urusi.
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema iko tayari kushambulia "vituo vya kufanya maamuzi" huko Kyiv iwapo mashambulizi kama hayo yatatokea.
Uwepo wa washauri wa nchi za Magharibi katika vituo hivyo huenda usiathiri uamuzi wake wa kulipiza kisasi, iliongeza.
Haya yanajiri baada ya waziri wa ulinzi wa Uingereza kusema "si lazima iwe tatizo" kwa Ukraine kutumia silaha zinazotolewa na Uingereza dhidi ya malengo ya kijeshi nchini Urusi.
James Heappey alisema mashambulizi ya kijeshi ya Ukraine kuvuruga njia za usambazaji bidhaa ni sehemu "halali" ya vita, na alielezea madai ya Urusi kuhusu Nato kuwa katika mzozo na Urusi kama "upuuzi".
Urusi imedai kuwa vikosi vya Ukraine vimeshambulia maeneo yaliyolengwa ndani ya ardhi yake, ikiwa ni pamoja na ghala la mafuta mjini Belgorod, lakini Ukraine haijathibitisha kuwepo kwa mashambulizi yoyote.
Nchi za Magharibi zimetoa msaada wa mamia ya mamilioni ya pauni za kijeshi kwa Ukraine tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake mwezi Februari, na maafisa wa Nato na Umoja wa Ulaya wamekuwa wakikutana nchini Ujerumani kujadili msaada zaidi wa kijeshi.
Serikali ya Uingereza imetangaza kuwa itavipa vikosi vya Ukraine idadi ndogo ya magari ya kuzuia ndege.
Katika taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la Interfax, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema: "Tungependa kusisitiza kwamba uchochezi wa moja kwa moja wa London wa serikali ya Kyiv katika shughuli kama hizo [kushambulia eneo la Urusi], ikiwa kuna jaribio la kuzitambua, itasababisha majibu yetu sawia mara moja."
Wizara hiyo pia ilisema kuwa vikosi vya jeshi la Urusi viko tayari "kutekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa kutumia silaha za masafa marefu zenye usahihi wa hali ya juu" dhidi ya "vituo vinavyochukua maamuzi muhimu" katika mji mkuu wa Kyiv wa Ukraine.
Waziri wa mambo ya nje Sergei Lavrov pia alishutumu Nato kwa kuendesha vita vya wakala, na kusema silaha za Magharibi zinazowasilishwa kwa Ukraine zitakuwa shabaha za haki.
Bw Lavrov alidai kuwa nchi za Magharibi "zinamwaga mafuta kwenye moto" kwa kuipatia Ukraine nguvu ya kuzima moto, na kuonya mara kwa mara kwamba mzozo huo unaweza kusababisha vita vya tatu vya dunia.

Lakini Bw Heappey alikiambia kipindi cha Leo cha BBC Radio 4 kwamba ni Ukraine ambayo hufanya maamuzi ya wapi na nini italenga, badala ya nchi au makampuni yanayotengeneza na kuuza nje silaha hizo.
Bw Heappey aliongeza: "Ni halali kabisa kufuata shabaha katika kina cha wapinzani wako ili kuvuruga vifaa na ugavi wao."
Aliongeza kuwa pia ni sehemu halali ya vita kwa vikosi vya Urusi kuwa shabaha inayolenga magharibi mwa Ukraine ili kuvuruga njia za usambazaji bidhaa za Ukraine, mradi tu waepuke kuwalenga raia - "jambo ambalo kwa bahati mbaya hawajalizingatia sana hadi sasa".

Chanzo cha picha, Getty Images
"Uingereza na washirika wengine wengi wa Magharibi sasa wanatoa mifumo ya silaha za masafa marefu kusaidia kukabiliana na milio ya risasi isiyobagua ambayo vikosi vya jeshi la Urusi vimekuwa vikimimina kwenye miji iliyozingirwa ya Ukraine," duru hizo ziliiambia BBC.
"Kulenga ni suala la Ukraine, lakini Uingereza inatarajia pande zote katika mzozo huu kuamua juu ya malengo yao ya kijeshi kwa kufuata kikamilifu sheria za migogoro ya silaha."
Baadaye, Waziri Mkuu Boris Johnson aliulizwa katika mahojiano ya Talk TV kama alikuwa anaridhika silaha za Uingereza kutumika dhidi ya shabaha kama vile vinu vya kusafisha mafuta ndani ya Urusi - na akajibu kwamba Ukraine ilikuwa na haki ya kujilinda.
"Hatutaki mgogoro kuongezeka zaidi ya mipaka ya Ukraine," alisema.
"Lakini Waukraine, kwa uwazi, kama James [Heappey] amesema, wana haki ya kujilinda. Wanashambuliwa kutoka ndani ya ardhi ya Urusi... wana haki ya kujilinda".
Kwa miezi kadhaa, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekuwa akiomba washirika wa Magharibi silaha zaidi ili kukabiliana na uvamizi wa Urusi.
Siku ya Jumatatu, Waziri wa Ulinzi Ben Wallace alitangaza kuwa Uingereza itatoa idadi ndogo ya magari ya Stormer yaliyowekwa kurushia makombora ya kutungulia ndege ya Starstreak ili kuwapa vikosi vya Ukraine "uwezo ulioimarishwa wa masafa mafupi ya kulinda anga mchana na usiku".
Pia aliliambia Bunge kuwa takriban wanajeshi 15,000 wa Urusi wameuawa tangu Urusi ilipofanya uvamizi kamili wa Ukraine, huku magari yake ya kivita 2,000 yakiwa yameharibiwa au kutekwa.
Wakati huo huo, Bw Johnson amesema hatarajii Urusi kutumia silaha za nyuklia nchini Ukraine, hata kama Rais Vladimir Putin atashindwa zaidi kijeshi huko.
Waziri Mkuu aliiambia TalkTV alidhani Bw Putin ana "nafasi ya kutosha ya kisiasa" kujiuzulu na kujiondoa, kutokana na "uungwaji mkono" mkubwa anaofurahia nchini Urusi na "dhahiri kutojali kwa vyombo vya habari vya Urusi".
Unaweza pia kusoma
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine












