Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Oligarch wa Urusi alaani 'mauaji' yanayofanywa na nchi hiyo
Mfanyabiashara tajiri wa Urusi ameshutumu "mauaji" ya nchi hiyo huko Ukraine na kutoa wito wa kumalizika kwa "vita vya kichaa".
Oleg Tinkov aliandika katika chapisho la Instagram lililojaa lugha chafu kwamba hakuona "mnufaika yeyote" wa mzozo huo.
Bw Tinkov ni mmoja wa wajasiriamali maarufu nchini Urusi na alianzisha benki ya kimataifa ya mtandao ya Tinkoff na kumiliki timu ya waendesha baiskeli Tinkoff-Saxo.
Yeye pia ni mmoja wa Warusi wenye hadhi ya juu kulaani vitendo vya Rais Vladimir Putin hadharani.
Wafanyabiashara wengine tajiri na wenye ushawishi mkubwa nchini humo Mikhail Fridman na Oleg Deripaska pia wametoa wito wa amani, lakini hawakukosoa moja kwa moja uamuzi wa serikali.
Bw Fridman, bilionea wa benki, amesema matamshi yoyote ya kibinafsi yanaweza kuwa hatari sio kwake tu bali pia wafanyikazi na wafanyikazi wenzake.
Hata hivyo, mfanyabiashara Boris Mints, ambaye alifanya kazi katika serikali ya Urusi katika miaka ya 1990 lakini akaachishwa kwa majukumu yake ya kisiasa siku nne baada ya Bw Putin kuchukua madaraka, ameungana na Bw Tinkov kumkosoa rais moja kwa moja.
Bw. Mints, ambaye anaishi nchini Uingereza, ni muathirika wa hatua ya sasa ya kisheria iliyochukuliwa na Kremlin. Aliambia BBC "kila mtu mwenye fikra sahihi ana wajibu wa kukemea vita hivi vya kutisha na kuongezeka kwa ubabe wa Vladimir Putin".
""Sote lazima tufanye tuwezavyo kusaidia wananchi wa Ukraine wanaoteseka kutokana na mashambulizi hayo mabaya, iwe katika Ukraine au kama wakimbizi nje ya mipaka yake," aliongeza.
Serikali ya Uingereza imemuwekea vikwazo Bw Tinkov pamoja na Warusi wengine kadhaa wanaotambuliwa kuwa na uhusiano wa karibu na Kremlim. Bw Mints hajaidhinishwa.
Onyo: lugha iliyotumika katika taarifa hii huenda ikawakera baadhi ya wasomaji.
Bw. Tinkov amekuwa akikanusha kuwa na uhusuano wa karibu na Rais Putin au Kremlin.
Katika chapisho lake la Instagram, Bw Tinkov alisema asilimia 90 ya Warusi wanapinga vita vya Ukraine na kuongeza "wajinga katika nchi yoyote ni 10%.
"Sioni mnufaika MMOJA wa vita hivi vya kichaa! Watu wasio na hatia na wanajeshi wanakufa," Bw Tinkov aliongeza.
"Baada ya kuamka wakiwa na uchovu, majenerali waligundua kuwa wana jeshi la kipuzi.
"Na jeshi litakuwa jema vipi, ikiwa kila kitu kingine nchini ni chafu na kimejaa upendeleo, urafiki na utumishi?"
Kabla ya Urusi kuivamia Ukraine mwishoni mwa Februari, utajiri wa Bw Tinkov ulikadiriwa kuwa zaidi ya dola bilioni 4.4 (£3.4bn).
Lakini tangu wakati huo amepoteza hadhi yake ya bilionea huku hisa katika benki yake zikishuka, Forbes iliripoti mwezi uliopita.
Akibadili kwa Kiingereza katika chapisho lake, Bw Tinkov aliandika: "Mpendwa 'collective West' tafadhali mpe Bwana Putin muda ili kuokoa uso wake na kukomesha mauaji haya. Tafadhali kuwa na busara zaidi na ubinadamu."
Katika taarifa, benki ya Tinkoff ilisema haitatoa kauli kuhusu "maoni ya kibinafsi" ya mwanzilishi wake, aliyejiondoa kama mwenyekiti mwaka 2020, akisema hafanyi tena maamuzi ya benki hiyo iliyoanza mnamo 2006.
Bw Tinkov, ambaye kwa sasa hayuko nchini Urusi, anamiliki 35% ya TCS Group Holding yenye makao yake Cyprus, ambayo kampuni zake thabiti chini ya Tinkoff zinahusisha sekta za benki na bima hadi huduma za simu.
Ameelezewa kama "mjasiriamali wa mahiri" ambaye kazi yake imeanzi kwa mbio za baiskeli, hadi kuagiza vifaa vya elektroniki, kupika vyakula vilivyogandishwa, kutengeneza bia, kutoa kadi za mkopo na kisha kurudi kwenye mbio za baiskeli kama mmiliki wa timu ya baiskeli ya Tinkoff-Saxo.
Unaweza pia kusoma
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine