Vita vya Ukraine: Je! bomu la kutawanya lilitumika katika shambulio kwenye kituo cha Ukraine?

Chanzo cha picha, Reuters
Uchunguzi wa BBC umepata ushahidi wa wazi kwamba bomu mtawanyiko (cluster), lililopigwa marufuku na nchi nyingi chini ya sheria za kimataifa, lilitumiwa katika shambulio kwenye kituo cha treni cha Kramatorsk nchini Ukraine.
Silaha hizi hutoa mzigo wa mabomu ambayo yanaenea na kulipuka katika eneo kubwa.
Zaidi ya watu 50 walikufa wakati kombora lilipopiga kituo hicho, ambacho kilikuwa na watu wengi wakijaribu kuondoka mashariki mwa nchi, tarehe 9 Aprili.
Zaidi ya nchi 120 zimekubali mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha hizi - lakini sio Urusi au Ukraine.
Kuna ushahidi gani wa silaha za mtawanyiko?
Waandishi wa habari wa BBC waliotembelea kituo hicho baada ya shambulio hilo walipata mifumo iliyo wazi ardhini inayoendana na matumizi ya vichwa vya risasi hizo.

Jengo karibu na kituo pia lilionesha muundo kama huo wa kutawanya kando, karibu na shimo kubwa lililoundwa ukutani.
Waandishi wa habari wa Washington Post, ambao walikuwa kwenye eneo la tukio mara tu baada ya shambulio hilo, waliambiwa na walioshuhudia kwamba walikuwa wamesikia "mlipuko wa awali uliofuatiwa na milipuko minne hadi mitano". Mtindo huu wa sauti unaendana na ule wa bomu la kutawanyika.
Mabaki ya kombora la Tochka-U ya zama za Sovieti yalipatikana baada ya shambulio hilo.
Ni kombora la masafa mafupi la balistiki linaloweza kuwekwa kichwa chake ambacho hubeba mabomu 50, ambayo yanaweza kulipuka yanapopigwa.

Kuna ushahidi kwamba Urusi iliwahi kusambaza makombora haya katika mzozo wa sasa, ingawa Ukraine pia ina silaha hii katika safu yake ya ushambuliaji.
Urusi hapo awali ilikana kuitumia katika mikoa ya Donetsk na Luhansk ya Ukraine, lakini madai haya yanapingwa.
Wataalamu wa kijeshi wanasemaje?
Sidharth Kaushal, mtaalam wa makombora katika Taasisi ya Huduma ya Royal United Services (Rusi), alisema: "Alama ya athari inalingana sana na risasi ndogo kama 9N24, safu ya silaha ya enzi ya Sovieti ambayo inaweza kubebwa na kombora la Tochka."
Aliashiria shimo la kati lenye kina kirefu na alama za mgawanyiko zinazong'aa ambazo zinaonekana kuwa katika mwelekeo mmoja, ambao unaendana na risasi ndogo za umbo hilo.

"Hii inalingana sana na athari ya silaha ndogo ya mtawanyiko - kwa hivyo bomu la mtawanyiko lilitumiwa."
Tumezungumza na wataalamu wengine wawili wanaokubaliana na matokeo haya.
BBC imejaribu kutambua eneo la kurushia kombora hilo, kwa kutumia video na picha za mitandao ya kijamii, lakini hadi sasa haijaweza kufanya hivyo.
Kwa nini silaha za mtawanyiko zimepigwa marufuku?
Matumizi ya silaha hizi yameibua ukosoaji mkubwa kutoka kwa vikundi vya kutetea haki za binadamu kutokana na uharibifu wao na madhara wanayoleta kwa raia katika maeneo yenye migogoro.
Silaha hizi zinaweza kutoa mabomu kama 50 katika eneo la hadi 400m, na uwezekano wa kusababisha vifo vingi vya raia katika maeneo lenye wakazi wengi.

Pia kuna hatari inayowakabili iwapo baadhi ya zana ndogo hazitalipuka , jambo ambalo ni la kawaida kwa makombora ya zamani ya Sovieti ambayo yamepitwa na wakati kwa miongo kadhaa, kama ilivyo kwa Tochka.
Mkataba wa 2008 kuhusu Mabomu ya kutawanywa unakataza matumizi ya silaha hizi, lakini Urusi na Ukraine sio watia saini wa mkataba huo.
Hapo awali katika mzozo huo, kulikuwa na shutuma kwamba vikosi vya Urusi vilikuwa vikitumia mabomu ya kutawanyika katika eneo la Kharkhiv, na kusababisha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutangaza kuwa inaanzisha uchunguzi.












