Vita vya Ukraine: Urusi yazionya Sweden na Finland dhidi ya kujiunga na Nato

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Urusi imezionya Finland na Uswidi dhidi ya kujiunga na Nato, ikisema kuwa hatua hiyo haiwezi kuleta utulivu barani Ulaya.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari kwamba "muungano unasalia kuwa chombo kinacholenga makabiliano".

Inakuja wakati maafisa wa ulinzi wa Marekani walisema uvamizi wa Moscow nchini Ukraine umekuwa "kosa kubwa la kimkakati" ambalo linaweza kuleta upanuzi wa Nato.

Maafisa wa Marekani wanatarajia majirani wa Nordic kutoa zabuni ya uanachama wa muungano huo, labda mapema Juni.

Washington inaaminika kuunga mkono hatua hiyo ambayo itaufanya muungano huo wa Magharibi kukua na kufikia wanachama 32. Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani walisema wiki iliyopita kuwa majadiliano yalifanyika kati ya viongozi wa Nato na mawaziri wa mambo ya nje kutoka Helsinki na Stockholm.

Kabla ya kuanza uvamizi wake, Urusi ilidai kwamba muungano huo ukubali kusitisha upanuzi wowote wa siku zijazo, lakini vita hivyo vimesababisha kutumwa kwa wanajeshi zaidi wa Nato kwenye ubavu wake wa mashariki na kuongezeka kwa uungaji mkono wa umma kwa uanachama wa Uswidi na Ufini.

th

Wabunge wa Ufini wanatarajiwa kupokea ripoti ya usalama kutoka kwa maafisa wa ujasusi wiki hii, na Waziri Mkuu Sanna Marin alisema anatarajia serikali yake "itamaliza mjadala kabla ya msimu wa joto" wa iwapo watatuma maombi ya uanachama.

Ufini inashiriki mpaka wa kilomita 1,340 (maili 830) na Urusi na imehofishwa na uvamizi wa Ukraine.

Na chama tawala cha Uswidi cha Social Democratic, ambacho kimekuwa kikipinga uanachama wa Nato, kilisema kinafikiria upya msimamo huu kutokana na mashambulizi ya Urusi dhidi ya jirani yake wa magharibi. Katibu wa chama Tobias Baudin aliambia vyombo vya habari vya ndani kwamba mapitio ya Nato yanapaswa kukamilika ndani ya miezi michache ijayo.

"Wakati Urusi ilipoivamia Ukraine, msimamo wa usalama wa Uswidi ulibadilika kimsingi," chama hicho kilisema katika taarifa siku ya Jumatatu.

Lakini Moscow imekuwa wazi kuwa inapinga uwezekano wowote wa upanuzi wa muungano huo. Bw Peskov alionya umoja huo "sio aina hiyo ya muungano unaohakikisha amani na utulivu, na upanuzi wake zaidi hautaleta usalama wa ziada katika bara la Ulaya".

Wiki iliyopita Bw Peskov alisema kuwa Urusi italazimika "kusawazisha hali" kwa hatua zake yenyewe iwapo Uswidi na Finland kujiunga na Nato.

Na mwezi Februari Maria Zakharova, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi, alionya kuhusu "matokeo ya kijeshi na kisiasa" ikiwa nchi hizo zitajiunga na umoja huo.

Nato iliundwa mwaka wa 1949 ili kukabiliana na tishio la upanuzi wa Soviet, ingawa tangu kuanguka kwa ukuta wa Berlin nchi kadhaa za zamani za kikomunisti za Ulaya Mashariki zimejiunga nao.

Nchi wanachama zinakubali kusaidiana iwapo kutatokea shambulio la silaha dhidi ya nchi yoyote mwanachama.

Licha ya vitisho, nchi zote mbili zimesonga mbele na zabuni zao na kuongeza matumizi ya ulinzi.

Siku ya Jumatatu, viongozi wa jeshi huko Helsinki walitangaza mpango mpya wa kutenga €14m (£10.88m) kununua ndege zisizo na rubani kwa jeshi la Finland.

Na mwezi uliopita maafisa wa Uswidi walisema wataongeza matumizi ya ulinzi kwa krona bilioni tatu ($317m; £243m) mnamo 2022.

Unaweza pia kusoma