Vita vya Ukraine: Jinsi raia wa Ukraine wanavyodaiwa kuuawa na wanajeshi wa Urusi

Ukraine imeanza uchunguzi wa uhalifu wa kivita baada ya miili ya raia kupatikana ikiwa imetapakaa mitaani huku wanajeshi wa Urusi wakiondoka katika maeneo yanayozunguka mji mkuu Kyiv.

Bucha na Irpin zilikuwa ishara za kupinga uvamizi wa Urusi, lakini sasa zinafanana na unyanyasaji mbaya zaidi wa vita.

Mamlaka ya Ukraine inasema miili ya raia 410 imepatikana katika maeneo karibu na Kyiv kufikia sasa.

Urusi, bila ushahidi, inasema picha na video hizo ni "onyesho la jukwaani" la Ukraine.

Lakini kile ambacho maafisa na wanahabari wamekiona huko kufuatia kujiondoa kwa Urusi kimewaacha wengi katika mshtuko mkubwa.

Onyo: Ripoti hii ina picha na maudhui ya kutatanisha.

Ni nini kilitokea huko Bucha?

Siku mbili au tatu baada ya Urusi kuzindua uvamizi wa 24 Februari kwa jirani yake, safu ya vifaru vya Kirusi na magari ya kivita ya (APC) ambayo yalikuwa yamewasili Bucha yalivamiwa na Waukraine, na kuwakwamisha kusonga mbele.

Warusi waliimarisha na kukaa katika eneo hilo nje kidogo ya mji mkuu, hawakuweza kusonga mbele sana, hadi walipoanza kujiondoa mnamo Machi 30.

Raia wengi walikuwa wamekimbia eneo hilo - lakini wengine walibaki nyuma, wakijaribu kuwaepuka Warusi. Ni katika kipindi hiki ambapo Warusi waliripotiwa kuanza kwenda nyumba kwa nyumba.

Mashahidi wameeleza jinsi wanajeshi wa Urusi walivyowafyatulia risasi wanaume waliokuwa wakitoroka baada ya kukataa kuwaruhusu kuondoka kupitia korido za kibinadamu.

Maafisa na waandishi wa habari walioingia baada ya Warusi kuondoka waliona mizinga na APCs, pamoja na watu wasiopungua 20 wamelala mitaani.

Wengi walikuwa na majeraha makubwa - wengine walikuwa wamepigwa risasi kwenye vichwa , kana kwamba wameuawa. Wengine walikuwa wamefungwa mikono au miguu. Nyingine zilikuwa zimevurugwa na mizinga.

Picha za satelaiti zilizopigwa na Maxar zinaonyesha kaburi la halaiki la mita 14 (futi 45) huko Bucha karibu na kanisa la St Andrew na Pyervozvannoho All Saints.

Kampuni hiyo inasema ishara za kwanza za kuchimba zilionekana mnamo Machi 10 - sio muda mrefu baada ya uzinduzi wa uvamizi wa Urusi wa Ukraine.

Na wakaazi wa Bucha wamesema miili ya kwanza ilizikwa huko katika siku chache za kwanza za vita, kwani Warusi waliua watu wengi kwa "kumpiga risasi kila mtu waliyemwona". Makadirio ya waliozikwa ni kati ya 150-300.

Onyo: Picha ya kuhuzunisha hapa chini

'Kupigwa risasi nyuma ya kichwa'

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekusanya ushahidi wa madai ya uhalifu wa kivita huko Bucha na miji mingine na miji iliyo chini ya udhibiti wa majeshi ya Urusi.

Katika ripoti iliyochapishwa tarehe 3 Aprili 2022, ilirekodi tukio la Bucha mnamo Machi 4 ambapo askari wa Urusi waliwalazimisha wanaume watano "kupiga magoti kando ya barabara, wakavuta fulana zao juu ya vichwa vyao, na kumpiga risasi mmoja ya wanaume nyuma ya kichwa."

Na maelezo zaidi ya kutisha yanaendelea kujitokeza.

Mwandishi wa BBC Yogita Limaye alitembelea orofa ya chini ya nyumba huko Bucha ambapo miili ya wanaume watano waliovalia nguo za kiraia iliachwa. Walikuwa wamefungwa mikono nyuma ya migongo yao na walionekana wameuawa kwa kupigwa risasi.

Waukraine wanasema simulizi kama hizo zinaonekana mahali pengine na zitachunguzwa.

Katika kijiji cha karibu cha Motyzhyn, timu ya BBC ilichukuliwa kuona kaburi lenye kina kirefu - miili minne ilionekana, na maafisa wa Ukraine walisema kunaweza kuwa na zaidi.

Miili mitatu kati ya hiyo imetambuliwa kuwa ya mkuu wa kijiji Olga Sohnenko, mumewe na mwanawe. Ya nne bado haijatambuliwa.

Haijulikani ni lini waliuawa.

Maeneo karibu na Kyiv sasa yamerudi chini ya udhibiti wa Ukraine ni pamoja na mji wa Irpin, ambapo picha za kuvunja moyo zilionyesha raia wakikimbia chini ya mashambulizi ya Urusi kwa siku nyingi.

Kulikuwa na visa vya watu kupigwa risasi walipokuwa wakifanya hivyo. Mnamo tarehe 6 Machi raia wanne - mwanamke, mwanawe wa kiume, binti yake wa karibu umri wa miaka minane, na rafiki wa familia - wote waliuawa kwa kombora walipokuwa wakijaribu kuvuka daraja lililovunjwa.

Unaweza pia kusoma

Katika tukio jingine, mama na mwanawe pia waliuawa na kuzikwa na majirani katika ua wa mtaa huo wa ghorofa.

Mnamo Machi 7, picha za drone zilionyesha gari kwenye barabara nje ya Kyiv, ambayo mtu anaibuka akiwa ameinua mikono. Mwili wake unaanguka chini. Maksim Iovenko, 31, aliuawa kwa kupigwa risasi na vikosi vya Urusi vilivyokuwa kando ya barabara. Mkewe Ksenia, ambaye alikuwa ndani ya gari, pia aliuawa.

Ripoti ya HRW inajumuisha kisa cha mama mmoja katika jiji la Kharkiv, ambaye alibakwa na mwanajeshi wa Urusi mwenye umri wa miaka 20 ndani ya shule ambayo raia walikuwa wamejificha

Na mengine mengi.

Tuhuma za uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki

Rais Volodymyr Zelensky hana shaka kwamba wanajeshi wa Urusi wanafanya uhalifu wa kivita na hata mauaji ya kimbari dhidi ya watu wake. Mauaji ya kimbari yanafahamika na wengi kuwa uhalifu mkubwa dhidi ya ubinadamu. Inafafanuliwa kama maangamizi makubwa ya kikundi fulani cha watu - kilichoonyeshwa na juhudi za Wanazi kuangamiza idadi ya Wayahudi katika miaka ya 1940.

"Ulimwengu tayari umeona uhalifu mwingi wa kivita. Kwa nyakati tofauti. Katika mabara tofauti. Lakini ni wakati wa kufanya kila linalowezekana ili kufanya uhalifu wa kivita wa jeshi la Urusi kuwa dhihirisho la mwisho la uovu huo duniani," Bw Zelensky alisema Jumapili. , kama ushahidi wa mauaji ya Bucha ulitangazwa hadharani.

Aliambia kipindi cha Face the Nation wa mtandao wa Marekani wa CBS: "Hakika. Haya ni mauaji ya halaiki.

"Kutokomezwa kwa taifa zima, na watu. Sisi ni raia wa Ukraine. Tuna zaidi ya mataifa 100. Hii ni kuhusu uharibifu na maangamizi ya mataifa haya yote."

Nchi nyingi za Magharibi zimeelezea kusikitishwa kwao na picha za miili iliyotapakaa kwenye mitaa ya miji.

Lakini Urusi inabaki kupuuza . Inasema operesheni yake - ambayo wanakataa kuiita vita vya uvamizi - inaendelea kulingana na mpango, na kwamba tuhuma za uhalifu wa kivita zote ni bandia.