Ukraine na Urusi: Ukraine inaweza 'kushinda' vita?

watu milioni nne wameikimbia Ukraine, na robo ya idadi ya watu nchini humo wanatajwa kuyakimbia makazi yao.

Chanzo cha picha, Getty Images

Urusi inaendelea kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Ukraine, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja sasa tangu iivamie. Vikosi vya Ukraine vimeanza majaribio ya kuyakomboa baadhi ya maeneo kutoka Urusi, ambayo ilisema wiki hii kuwa imepunguza operesheni zake za kijeshi karibu na Kyiv na mji wa kaskazini wa Chernihiv.

Wakati huo huo watu milioni nne wameikimbia Ukraine, na robo ya idadi ya watu nchini humo wanatajwa kuyakimbia makazi yao.

Waandishi wa habari wa BBC walioko karibu na uwanja wa vita, wanajibu maswali yako:

Orla Guerin yuko katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv

Jenny Hill, yuko katika mji mkuu wa Urusi, Moscow

Kwa kuzingatia mashambulizi ya hivi karibuni ya Ukraine kukabiliana na Urusi, na iwapo mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Ukraine na Urusi yatashindikana, Ukraine inaweza "kushinda" vita hivi kijeshi? - Harry Tinsley

Olga Guerin anaandika:

Kwa muktadha wa kijeshi hadi sasa mambo yanaonekana kuwaendelea vizuri Ukraine. Ukraine imemshangaza Rais Putin, na Ulimwengu kwa ujumla, kwa kuongezeka upinzani wenye ujuzi na ukaidi dhidi ya jeshi kubwa, lenye vifaa bora la Urusi.

Tuliona mfano wa mafanikio ya Ukraine katika vita hii huko Kyiv wiki iliyopita. Vikosi vya Ukraine vilituambia kuwa Warusi walijaribu kuingia mji huo mara nne mwezi uliopita, na kila wakati walikuwa wamekutana na ukinzani mkali.

Warusi hawajaweza kuingia katika mji mkuu Kyiv, kuiangusha serikali, au kuchukua mji wowote mkubwa achilia mbali Kherson - kusini. Urusi imeiharibu miji zaidi kuliko kuiteka.

Hata hivyo, ni mapema mno kutabiri matokeo ya vita hii. Tunaweza kuwa mwanzoni mwa vita vya muda mrefu. Urusi kwa sasa inasema itaelekeza nguvu zake katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine.

Warusi hawajaweza kuingia katika mji mkuu Kyiv

Chanzo cha picha, Getty Images

Pamoja na Urusi kuchukua wapiganaji kutoka Mashariki ya Kati, je, hii inaonyesha ukosefu wa imani na ubora wa vikosi vyake mwenyewe? - David Carter

Jenny Hill anaandika:

Kremlin kamwe haiwezi kukiri hilo, lakini kuna ushahidi kwamba angalau baadhi ya majeshi ya Urusi yanaonyesha kutokuwa na uzoefu na hayakujiandaa kwa misheni yao. Wizara ya Ulinzi hivi karibuni ililazimika kukubali kwamba kuna wapiganaji wa kuazimwa wamepelekwa Ukraine kupigana kinyume na madai ya Putin.

Moscow inadai kuwa na wanajeshi "wakujitolea" 16,000 wa Mashariki ya Kati, ambao wengi wao walipigana dhidi ya kundi la ISIS katika muongo uliopita, wako tayari kujiunga na vikosi vya Urusi. Wanaweza kuwa na uzoefu zaidi kuliko wenzao wa Urusi, na baadhi ya wataalam wanasema labda wana ujuzi zaidi katika aina ya mapambano muhimu ya mijini yenye lengo la kuteka miji na miji.

Je kuna uwezekano watu wa Urusi watampindua Putin au kusababisha machafuko makubwa ya wenyewe kwa wenyewe, ikiwa mzozo huu utadumu kwa muda mrefu zaidi? Damien Fieldhouse, Somerset

Jenny Hill anaandika:

Uwezekano ni mdogo.

Kremlin imekuwa ikiwashughulikia kwa nguvu wale wote wanaopinga vita na Warusi wengi ambao wanamtazamo huo wameikimbia nchi hiyo. Maandamano ya karibu kila siku yamepungua.

Kutokana na kwamba vyombo vingi huru vya habari vya Urusi vimezuiwa au kulazimishwa kufungwa, kuna njia mbadala chache za vyombo vya habari vya serikali, ambavyo vinashikamana na muelekeo wa Kremlin.

Vyombo hivyo vinasema kuwa majeshi ya Urusi yameingia Ukraine kwa lengo tu la kulinda jamii ya watu wanaozungumza Kirusi dhidi ya mashambulizi na "mauaji ya kimbari" toka kwa wazalendo wa Kiukreni na neo-Nazis.

Putin

Chanzo cha picha, Getty Images

Nani atalipa gharama za upa miundo mbinu nchini Ukraine iliyoharibiwa kwenye vita - achilia mbali gharaza za watu waliokufa? - Steve Sandercott, Rugby

Olga Guerin anaandika:

Gharama kubwa ni ile ya kuuawa kwa watu na hiyo inaongezeka kila siku. Idadi ya vifo vya raia waliothibitishwa, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ni watu 1,200, lakini idadi halisi itakuwa kubwa zaidi. Mbali na hilo, waukraine milioni nne wamekimbia na kuwa wakimbizi katika nchi nyingine.

Pia kuna uharibifu mkubwa katika miji kadhaa Ukraine mfano mji wa Kusini wa Mariupol ambao ulikumbwa na mshambulizi ya siku 10 mfululizo. Picha za satelaiti za mji wa Mariupol sasa zinaionyesha dunia namna ulivyoharibiwa, 90% ya majengo ya makazi yameharibiwa vibaya.

Wanajeshi wa Kiukreni wanajiandaa kwa vita mashariki mwa Kyiv

Chanzo cha picha, Getty Images

Zaidi ya watu 5,000 wanaelezwa kuuawa katika mji huo pekee, kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine. Wanasema idadi halisi ya vifo inaweza kuwa mara mbili zaidi ya hiyo.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameahidi kurejesha "kila nyumba, kila mtaa na kila mji". Anasema Urusi italazimika "kuelewa neno 'fidia'" na kulipa gharama kamili.