Mzozo wa Ukraine na Afrika: Athari kwa mafuta,wanafunzi na mkate

Chanzo cha picha, Getty Images
Vita vya Ukraine vinaweza kuwa na athari mbaya kwa baadhi ya mataifa ya Afrika, na kutishia uchumi wao na kuona serikali zinakabiliwa na shinikizo la kidiplomasia kuchukua upande katika mzozo unaoongezeka kati ya Urusi na madola ya Magharibi.
Kama makala katika tovuti ya habari ya Daily Maverick ya Afrika Kusini ilivyobainisha, vita katika sehemu za mbali za Ulaya "zitashuhudiwa katika kila kijiji na mji wa Afrika Kusini na ulimwengu".
"Hata kabla ya makombora ya kwanza kurushwa vita hivi vimesababisha athari mbaya: kugeuza mabilioni ya dola kwenye silaha tena na mbali na kukabiliana na umaskini, magonjwa ya milipuko, elimu, ukosefu wa usawa na mzozo wa hali ya hewa katika mwaka muhimu," Mark Heywood aliandika.
Je, majibu ya Afrika yamekuwaje kwa vita?
Afrika Kusini - ambayo ina uchumi mkubwa zaidi wa kiviwanda barani Afrika - imetoa wito wa kuondolewa mara moja kwa wanajeshi wa Urusi kutoka Ukraine, ikisema mzozo huo unapaswa kutatuliwa kwa amani.
"Migogoro ya kivita bila shaka itasababisha mateso na uharibifu wa binadamu, ambayo madhara yake hayataathiri Ukraine pekee bali pia yataenea kote ulimwenguni. Hakuna nchi ambayo haiwezi kuathiriwa na mzozo huu," taarifa ya serikali ilisema.
Unaweza pia kusoma:
Msimamo wa Afrika Kusini ni pigo kwa Urusi, ambayo inaiona kuwa mshirika mkuu barani Afrika. Nchi hizo mbili zina uhusiano mkubwa wa kiuchumi, huku zote zikiwa wanachama wa Brics - kundi linaloundwa na mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani.
Afrika Kusini ina vitega uchumi nchini Urusi vinavyofikia karibu randi 80bn za Afrika Kusini ($5bn; £3.7bn), wakati uwekezaji wa Urusi nchini Afrika Kusini jumla ya randi 23bn.
Kenya - nchi yenye nguvu ya kiuchumi ya Afrika Mashariki, na mwanachama asiye wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa - imeenda mbali zaidi katika kulaani Urusi.
Katika hotuba yake ya kusisimua, balozi wa Kenya katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Martin Kimani, alisema: "Uadilifu wa eneo na mamlaka ya Ukraine vinavunjwa. Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaendelea kufifia chini ya uvamizi wa watu wenye nguvu."
Ghana na Gabon - mataifa mengine mawili ya Kiafrika kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa - pia yalilaani Urusi.

Hakuna nchi yoyote ya Kiafrika ambayo hadi sasa imejitokeza kuunga mkono uvamizi wa Urusi, hata Mali na Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambapo vikosi vya Urusi vinasaidia serikali kupambana na uasi.
Lakini - katika ishara kwamba tawala za kiimla zitasimama karibu nayo - kamanda wa kijeshi mwenye nguvu wa Sudan, Jenerali Mohamed Hamdan "Hemeti" Dagolo, aliwasili Moscow vita vya Ukraine vilipoanza.
Safari yake ilikuwa na lengo la kuimarisha uhusiano na Urusi, wakati ambapo jeshi la serikali limegeuka kutengwa na nchi za Magharibi kwa kuvuruga kipindi cha mpito kuelekea demokrasia baada ya kupinduliwa kwa mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir.
Wakati huo huo, balozi wa Urusi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anasema Moscow iko tayari kusaidia taifa hilo la Afrika ya Kati kumaliza ghasia za kijeshi mashariki mwa nchi hiyo, televisheni ya taifa imeripoti.
Vita vitawaathiri vipi Waafrika wa kawaida?
Bei ya mafuta tayari imepanda hadi $100 kwa pipa hadi kufikia kiwango cha juu zaidi tangu 2014.
Bajeti za nchi zinazozalisha mafuta kama Nigeria na Angola zinaweza kuongezwa kutokana na kupanda kwa bei, lakini gharama ya usafiri huenda ikapanda kwa watu katika bara zima.
Hii itakuwa na athari kwa bei ya karibu bidhaa zingine zote.
"Inakuwa hali mbaya maradufu ya uwezekano wa bei ya juu ya chakula duniani na bei ya juu ya nishati kusukuma mfumuko wa bei. Na benki kuu zinapojibu kwa kupanda viwango vya riba, inakuwa mbaya mara tatu," alisema Charlie Robertson, mwanauchumi mkuu wa kimataifa katika Renaissance Capital.
Lakini mhariri wa chapisho Africa Confidential lenye makao yake makuu nchini Uingereza, Patrick Smith, alisema vita vilitoa fursa kubwa kwa nchi zinazozalisha mafuta na gesi.
"Ulaya inabidi kutafuta kwa haraka njia mbadala za gesi ya Urusi, na njia mbadala zinazotegemewa zaidi ziko barani Afrika. Ni fursa nzuri kwa mataifa ya Afrika kuhamia, na kupata mikataba mipya haraka," aliongeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Alisema hatari kubwa ambayo Afŕika inakabiliana nayo ni kutokana na uwezekano wa kupanda kwa bei ya mkate, kwani Russia na Ukraine zinasambaza kaŕibu asilimia 30 ya ngano duniani.
"Bei ya mkate imekuwa msukumo wa kukosekana kwa utulivu wa kisiasa, na kuibua Mapinduzi ya Kiarabu. Nchi za Maghreb - Misri, Tunisia, Morocco, Libya na Algeria, ambazo zinategemea sana ngano - zinaweza kuathiriwa zaidi na kukazwa kwa usambazaji. na kuongezeka kwa bei," Bw Smith alisema.
Kenya pia ina wasiwasi kuhusu athari ambazo vita - na vikwazo vya kifedha kwa Urusi - vinaweza kuwa na sekta yake muhimu ya chai. Urusi ni miongoni mwa watumiaji watano wakuu wa chai yake, na kusaidia Kenya kupata pesa za kigeni.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Chai na vinywaji vingine vimeainishwa kama vyakula na kwa kawaida havitaathiriwa na vikwazo vya kibiashara," Edward Mudibo, afisa mtendaji mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara wa Chai Afrika Mashariki (EATTA).
Hata hivyo, alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara huenda hawataki kuchukua hatari iwapo Urusi itazuiliwa kutoka kwa mifumo ya malipo ya kimataifa.
Vipi kuhusu Waafrika walioko Ukraine?
Kwa vile ina ada nyepesi za masomo na uhusiano mzuri na Afrika kuanzia enzi ya Usovieti, Ukraine ni kivutio kikuu cha wanafunzi wa Kiafrika, na maelfu wanasoma katika vyuo vikuu vyake - haswa udaktari. Waafrika wengine pia wanaishi na kufanya kazi nchini Ukraine.
Pamoja na kuzuka kwa vita, wasiwasi unaongezeka juu ya usalama wao. Wizara ya Mambo ya Nje ya Ghana imewataka raia wake zaidi ya 1,000 "kujilinda" katika nyumba zao au katika makazi yaliyoteuliwa na serikali.
Lakini Umoja wa Kitaifa wa Wanafunzi wa Ghana uliitaka serikali kupanga mpango wa kuhamishwa, ikisema vita hivyo vinadai jibu sawa na lile lililochukuliwa wakati janga la coronavirus lilipoanza.
"Tunaamini mtindo uliotumika kwa uhamishaji wa wanafunzi kutoka Uchina katika kilele cha janga la Covid-19 unaweza kupitishwa katika kesi hii pia," ilisema katika taarifa.
Nchi za Kiafrika zenye wanafunzi wengi zaidi nchini Ukraine ni Morocco (8,000), Nigeria (4,000) na Misri (3,500). Wanasheheni - kama jarida la Afrika nzima la Quartz linavyoonyesha - karibu 20% ya wanafunzi wote wa kigeni wanaosoma nchini Ukraine mnamo 2020.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imesema "imepokea kwa mshangao" habari za uvamizi wa Urusi, na hatua zinachukuliwa kuwaweka raia wake walioko Ukraine salama na "kuwezesha uhamishaji wa wale wanaotaka kuondoka" mara tu viwanja vya ndege vitakapofunguliwa tena. .
Mwanafunzi wa matibabu raia wa Nigeria nchini Ukraine, Fatima Halilu, aliambia BBC kwamba aliondoka Kyiv karibu wiki mbili zilizopita.
"Marafiki zangu wote bado wako Kyiv. Wanaonekana kukwama, kupotea na kuchanganyikiwa," kijana huyo wa miaka 18 alisema.














