Mzozo wa Ukraine: Tunayofahamu mpaka sasa kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

raia

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Raia wakiukimbia mji mkuu wa Ukraine Kyiv kufuatia mashambulio ya vikosi vya Urusi

Urusi imeanza mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi ya Ukraine, jirani yake kwenye mpaka wa Kusini, kwa amri ya Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Kuna ripoti za mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kijeshi ya Ukraine nchini kote, na misafara ya Urusi inayoingia kutoka pande zote.

Hiki ndicho tunachojua hadi sasa.

Putin aamuru kuanza kwa mashambulizi

Katika hotuba ya televisheni saa 05:55 za Moscow, Putin alitangaza "operesheni ya kijeshi" katika eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine. Eneo hili ni nyumbani kwa raia wengi wa Ukrainiane wanaozungumza Kirusi. Sehemu za eneo hilo zimekuwa zikikaliwa na kuendeshwa na waasi wanaoungwa mkono na Urusi tangu mwaka 2014.

Rais Putin alisema Urusi inaingilia kati kama hatua ya kujilinda. Urusi haikutaka kuimiliki Ukraine, alisema, lakini itaiangamiza na "kuiangamiza" nchi hiyo.

Aliwataka wanajeshi wa Ukraine katika eneo la mapambano kuweka chini silaha zao na kurudi nyumbani, na kusema mapigano hayaepukiki na "ni suala la muda tu".

Na aliongeza kuwa uingiliaji wowote kutoka kwa mataifa ya nje ili kupinga shambulio la Urusi utakabiliwa na majibu ya kijeshi "mara moja".

Milipuko yasisika kote nchini

Waandishi wa BBC walisikia milio mikubwa katika mji mkuu Kyiv, pamoja na Kramatorsk katika eneo la Donetsk mashariki mwa Ukraine. Milipuko hiyo pia imesikika katika mji wa bandari wa kusini wa Odesa.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi imefanya mashambulizi ya makombora dhidi ya miundombinu ya Ukraine na walinzi wa mpakani.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imekanusha kuishambulia miji ya Ukraine - ikisema mashambulizi yake yanalenga miundombinu ya kijeshi, ulinzi wa anga na vikosi vya angani kwa kwa kutumia "silaha za hali ya juu".

Vifaru na vikosi vya wanajeshi waingia Ukraine

Vifaru na wanajeshi wa Urusi wamemiminika nchini Ukraine katika maeneo ya mashariki, kusini na kaskazini mwa mipaka, Ukraine imesema.

Msafara wa kijeshi wa Urusi umevuka mpaka kutoka Belarus hadi mkoa wa kaskazini mwa Ukraine wa Chernihiv, na kutoka Urusi hadi eneo la Sumy, ambalo pia liko kaskazini, kikosi cha ulinzi wa mpaka wa Ukraine (DPSU) kimesema.

convoy enters from crimea

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Msafara wa Urusi ukiingia kwenye jimbo la Ukraine la Kherson kutoka Crimea

Belarus ni mshirika wa muda mrefu wa Urusi. Wachambuzi wanaitaja nchi hiyo ndogo kama "mteja" wa Urusi.

Vikosi vingine pia vimeingia katika mikoa ya mashariki ya Luhansk na Kharkiv, na kuhamia katika mkoa wa Kherson kutoka Crimea - eneo ambalo Urusi ililitwaa kutoka Ukraine mwaka 2014.

Mashambulizi ya Urusi yalitanguliwa na kurushiana risasi za moto na kulikuwa na majeruhi kwa walinzi wa mpakani, DPSU ilisema.

Pia kumekuwa na ripoti za wanajeshi kuingia Ukraine kwa njia ya bahari katika miji ya bandari ya Bahari Nyeusi ya Mariupol na Odesa kusini mwa nchi hiyo.

Vifo vyaripotiwa

Takriban watu wanane wanaripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya mabomu yaliyofanywa na vikosi vya Urusi, polisi wa Ukraine imesema.

people leave kharkiv by driving acros fields

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Watu wamekuwa wakiendesha magari yao kupitia vichakani kuutoroka mji wa mashariki mwa Ukraine wa Kharkiv

Shambulio dhidi ya kitengo cha kijeshi huko Podilsk nje ya Odesa liliua watu sita na kujeruhi saba, maafisa wamesema. Watu 19 hawajulikani walipo.

Mtu mmoja alifariki katika mji wa mashariki wa Mariupol, Polisi imeongezea.

Ukraine yasema inajibu mapigo

Jeshi la Ukraine linasema limedungua ndege tano za Urusi na helikopta na kusababisha vifo vya wanajeshi kadhaa waliovamia.

"Endelea kuwa na utulivu na muamini vikosi vya ulinzi vya Ukraine", taarifa kutoka kwa vikosi vya Ukraine inasema.

Hata hivyo wizara ya ulinzi ya Urusi imekanusha kuwa ndege yake ilidunguliwa.

Ukraine imetangaza sheria ya kijeshi - ambayo inamaanisha kuwa jeshi linachukua udhibiti kwa muda - na imepunguza uhusiano wa kidiplomasia na Urusi.

Rais Zelensky amewataka Warusi kupinga uvamizi huo na kusema silaha zitasambazwa kwa mtu yeyote nchini Ukraine ambaye anataka.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba ameiomba dunia kuweka vikwazo vikali, ikiwa ni pamoja na kuipiga marufuku Urusi kutumia mfumo wa kibenki wa kuhamisha fedha kimataifa.

Wananchi wasaka makazi

Katika mji wa Kyiv kuna msongamano mkubwa kwenye vyombo vya usafiri watu wakijaribu kukimbia mji.

Shuhuda za mitandao ya kijamii zinazungumzia hofu inayoongezeka, huku baadhi wakisema wanakimbilia katika maeneo ambayo hawawezi kufikiwa na mabomu ikiwemo mahandaki. Picha za televisheni zimeonyesha watu wakisali mitaani.

resident shelter in metro

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wakazi wamekuwa wakitafuta makao katika vituo vya usafiri wa treni

Watu wengi huko Kyiv wametafuta makazi katika vituo vya treni vya chini ya ardhi. Pia kuna foleni ndefu katika vituo vya mafuta na mashine za fedha.

Katika eneo la Kramatorsk, mashariki mwa jimbo la Donetsk, mwandishi wa BBC wa Ulaya Mashariki Sarah Rainsford alisema watu hawakutarajia shambulio kama hilo.

"Watu walikuwa nje ya mitaa jana usiku katika mji huu - walikuwa wakipeperusha bendera ya Ukraine. Walisema kuwa hii ni nchi yao. Walikuwa hawaendi popote," alisema.

"Hiki ndicho ambacho watu wamekuwa wakitarajia, wamekuwa wakisubiri, lakini hakuna mtu yeyote hapa anayeweza kuamini kabisa kwamba kinatokea."

Unaweza pia kusoma:

Bei ya mafuta yapanda

Bei za mafuta zilipanda juu ya dola $ 100 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka saba.

Wakati huo huo sarafu ya Urusi, Rouble, imeendelea kushuka dhidi ya dola na euro.

Na ripoti inayoongoza ya Soko la Hisa la London FTSE 100 ilianguka zaidi ya pointi 200, au 2.7%, ndani ya muda mfupi tu.

Dunia yalaani Putin

Rais wa Marekani Joe Biden amesema Kuwa Putin "amechagua vita vilivyopangwa ambavyo vitasababisha hasara kubwa ya maisha na mateso ya binadamu". Dunia itawajibika, alisema.

Alisema atahutubia Wamarekani siku ya Alhamisi kuhusu madhara ambayo Urusi itakabiliana nayo.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema "ameshtushwa na matukio ya kutisha nchini Ukraine" na kwamba Putin "amechagua njia ya umwagaji damu na uharibifu kwa kuanzisha shambulio hili lisilotarajiwa".

Katibu Mkuu wa Nato Jens Stoltenberg amelaani "shambulio lisilo na maana" la Urusi akisema "linahatarisha maisha ya raia wengi".

Ulaya ilikuwa "inakabiliwa na masaa yake ya giza tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia", mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema.

Hata hivyo rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amesema Kuwa Putin alitumia fursa ya "udhaifu" wa Marekani.

Alikiambia kituo cha Televisheni cha Fox News kuwa hakuamini kwamba Putin "alitaka kufanya hivyo, awali".

"Nadhani alitaka kufanya kitu na majadiliano, lakini ilizidi kuwa mbaya zaidi na zaidi, na kisha aliona udhaifu," Trump alisema