Uvamizi Ukraine: Ghadhabu zazuka baada ya Waafrika kubaguliwa Ukraine

Kumekuwa na ripoti nyingi za maafisa wa usalama wa Ukraine kuwazuia Waafrika kupanda mabasi na treni zinazokwenda mpakani.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

Serikali ya Nigeria imelaani ripoti kwamba raia wake, na wale wa mataifa mengine ya Afrika, wamezuiwa kuondoka Ukraine iliyokumbwa na vita.

Isaac, raia wa Nigeria anayejaribu kuingia Poland, alisema wafanyakazi wa mpakani walimwambia "hawawajali Waafrika".

"Tumerudishwa nyuma, tumepigwa na polisi waliokuwa wamejihami kwa fimbo," aliiambia BBC.

Afisa wa ofisi ya mambo ya nje wa Afrika Kusini Clayson Monyela pia alisema wanafunzi "wametendewa vibaya" mpakani.

Pia kumekuwa na ripoti nyingi za maafisa wa usalama wa Ukraine kuwazuia Waafrika kupanda mabasi na treni zinazokwenda mpakani.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

1px transparent line

Osemen, kutoka Nigeria, aliiambia BBC kuwa alijaribu kupanda treni mjini Lviv ili kumpeleka kwenye mpaka wa Poland lakini aliambiwa ni raia wa Ukraine pekee ndio watakaoruhusiwa kupanda.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alisema kuna takriban Wanigeria 4,000 nchini Ukraine, wengi wao wakiwa wanafunzi.

Alisema kundi moja lilikuwa limekataliwa kuingia Poland kwa hivyo walisafiri kurudi Ukraine kuelekea Hungary badala yake.

"Wote wanaokimbia hali ya mzozo wana haki sawa ya kupitishwa kwa usalama chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na rangi ya hati zao za kusafiria au ngozi zao hazipaswi kuleta tofauti," Bw Buhari alisema kwenye Twitter.

Pia unaweza kusoma

Zaidi ya raia 350,000 wa Ukraine wameweza kuondoka Ukraine hadi sasa.

'Hoteli ni kwa ajili ya raia wa Ukraine tu'

Mwanafunzi wa chuo kikuu Ruqqaya, kutoka Nigeria, alikuwa akisomea udaktari huko Kharkiv mashariki mwa Ukraine wakati mji huo uliposhambuliwa. Alitembea kwa saa 11 usiku kucha kabla ya kufika kwenye kivuko cha Medyka na Poland.

"Nilipokuja hapa kulikuwa na watu weusi wamelala barabarani," aliiambia BBC.

Anasema aliambiwa na walinzi waliokuwa na silaha kusubiri kwani raia wa Ukraine walipaswa kupitishwa kwanza.

Alitazama mabasi ya watu, ambao aliwataja kuwa wazungu, wakiruhusiwa kupita mpakani huku Waafrika wachache tu wakichaguliwa kutoka kwenye foleni. Baada ya kungoja kwa saa nyingi, hatimaye aliruhusiwa kuvuka na kuelekea Warsaw kwa ndege kurudi Nigeria.

Asya, mwanafunzi wa utabibu kutoka Somalia anayesoma huko Kyiv, alikumbana na tukio kama hilo. Hatimaye alipofika Poland, alisema aliambiwa "malazi katika hoteli ni ya Waukraine pekee".

Kikosi cha mpakani cha Poland kiliiambia BBC kwamba kila mtu anayekimbia mzozo nchini Ukraine anakaribishwa nchini Poland bila kujali utaifa. BBC imejaribu kuwasiliana na kikosi cha mpakani cha Ukraine lakini bado haijapata jibu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Geofrey Onyeama amesema kuwa amezungumza na mwenzake wa Ukraine Dmytro Kuleba na kuhakikishiwa kwamba walinzi wa mpaka wa Ukraine wamepewa amri ya kuwaruhusu wageni wote wanaotoka Ukraine kupita bila vikwazo.

Wizara ya mambo ya nje ya Nigeria sasa imewashauri raia wake wanaoondoka Ukraine kuelekea Hungary au Romania, badala ya kujaribu kuingia Poland.

Balozi wa Nigeria nchini Romania ameambia BBC kwamba hadi sasa takriban Wanigeria 200 - wengi wao wakiwa wanafunzi - wamewasili katika mji mkuu wa Bucharest kutoka Ukraine. Safiya Nuhu alisema wengine wengi walikuwa bado wanawasili.