Ngono nzuri inaweza kuwa ngono salama, watafiti wa WHO wasema

Chanzo cha picha, Getty Images
Kufundisha watu kuhusu kupata furaha ya kujamiiana kunaweza kusaidia kusambaza ujumbe wa ngono salama, watafiti kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni wanasema.
Programu zinazotumia mbinu hii huboresha matumizi ya mipira ya kiume zaidi ya zile zinazozingatia tu hatari za ngono isiyo salama, utafiti wao umegundua.
Wanasema starehe - badala ya hofu - ni motisha yenye afya.
Ngono inaweza kuwa salama na vilevile kufurahisha, kulingana na mmoja wa waandishi wa mradi wa utafiti.
Mabilioni ya dola hutumika kote ulimwenguni kila mwaka kwa huduma za afya ya ngono na uzazi , lakini programu nyingi hazishughulikii mojawapo ya sababu kuu za watu kufanya ngono - kujisikia vizuri.
Anne Philpott, mtaalamu wa afya ya umma, alianzisha The Pleasure Project - kundi ambalo lilifanya kazi na timu ya WHO - mwaka 2004, kutokana na kuchanganyikiwa kwa "mikutano isiyo na mwisho ya Ukimwi ambapo hakuna aliyezungumza kuhusu motisha za watu kufanya ngono".
Maambukizi milioni ya magonjwa ya zinaa hupatikana kila siku duniani
Alisema: "furaha bila shaka ndicho kichocheo chenye nguvu zaidi cha kufanya ngono na bado kumekuwa hakuna elimu ya kujamiiana au afua za afya ya ngono.
"Ukiwauliza watu wengi, 'Je, elimu yako ya ngono ilikuwezesha kwa ajili ya mahusiano yako na maisha ya kujamiiana?' watasema, Hapana.
"Kujamiiana kunaweza kuwa salama - na kwa kufurahisha. Inahusu kuwa na mazungumzo ya wazi na kuwapa watu hali ya kujiamini."
Ulimwenguni, maambukizi milioni ya magonjwa ya zinaa hupatikana kila siku, mengi bila dalili.
Kutumia mpira kunaweza kulinda dhidi ya haya, na pia kuzuia mimba.
Anne alisema mpira ya kiume au ya kike inapaswa kuuzwa kama zana za kufurahisha - kama njia ya kuongeza hisia na uhakika.
Watafiti walipitia maandiko ya kitabibu ili kupata mifano ya hivi karibuni ya programu tofauti za ngono salama na kupima athari zake kwenye mabadiliko ya tabia.
Walipata miradi 33 inayokuza furaha pamoja na ujumbe wa ngono salama. Na hizi zilielekea kuwa na mafanikio zaidi katika suala la kuongeza matumizi ya mipira kuliko yale ambayo yalilenga tu magonjwa ya zinaa na kupunguza hatari.
Kufundisha kuhusu raha, hamu na furaha pamoja na ridhaa, ustawi na usalama ni malengo ya mpango wa elimu kuhusu kujamiiana unaozingatia starehe.
Dk Lianne Gonsalves wa WHO, mwandishi mwenza wa utafiti huo, uliochapishwa katika jarida la Plos One, alisema: "Tathimini hii inatoa ujumbe rahisi: programu ambazo zinaonesha vyema sababu za watu kufanya ngono - ikiwa ni pamoja na kwa furaha - wanaona matokeo bora ya kiafya.
"Matumaini ni kwamba matokeo haya yanachangamsha jumuiya ya haki za afya ya uzazi na ujinsia ili kukuza huduma zinazoelimisha na kuwawezesha watumiaji kushiriki ngono ambayo ni salama, ya kuridhiana na ya kufurahisha."














