Mzozo wa Ukraine: Mradi wa Bomba la Nord Stream 2 huenda ukalengwa na nchi za Magharibi

Chanzo cha picha, Getty Images
Ujerumani na Marekani zimeonya kuwa huenda zikalenga bomba muhimu la gesi la Urusi iwapo nchi hiyo itaivamia Ukraine.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alisema bomba la Nord Stream 2 "halitaendelea ikiwa Urusi itashambulia.
Mradi huo wa nishati wenye utata umeundwa kuongeza mtiririko wa gesi mara mbili na unaanzia Urusi moja kwa moja hadi Ujerumani kupitia Bahari ya Baltic.
Inakwepa Ukraine, ambayo inategemea mabomba yaliyopo kwa mapato na iko chini ya tishio kutoka kwa vikosi vya Urusi.
Makumi ya maelfu ya wanajeshi wa Urusi wamekusanyika kwenye mipaka ya Ukraine katika wiki za hivi karibuni, na kusababisha hofu ya uvamizi - licha ya Urusi kukanusha mara kwa mara kuhusu mpango wa kulivamia taifa .
Siku ya Jumatano Marekani ilikataa ombi la Urusi la kuizuia Ukraine kujiunga na muungano wa kijeshi wa Nato, huku ikionya Moscow kwamba uhusiano kati ya mataifa hayo utazorota zaidi.
Rais Vladimir Putin kwa sasa anatathmini mapendekezo hayo, msemaji wake alisema siku ya Alhamisi.
Mradi wa bomba la gesi la Nord Stream 2
Bomba hilo la urefu wa kilomita 1,225 (maili 760) lilichukua miaka mitano kujengwa na kugharimu $11bn (£8bn). Lakini bado halijaanza kufanya kazi, kwa kuwa kulingana na wasimamizi halikuzingatia sheria za Ujerumani na kusitisha idhini yake.
Akizungumza na shirika la utangazaji la NPR, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price alisema nchi yake itashirikiana na Ujerumani kuhakikisha mradi huo hauendelei iwapo Urusi itavamia.
"Nataka kuwa wazi kabisa: ikiwa Urusi itavamia Ukraine kwa njia moja au nyingine, mradi wa Nord Stream 2 hautaendelea," alisema, lakini akaongeza kuwa "hataingia katika maelezo maalum" ya jinsi gani utasitishwa.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, baadaye aliliambia bunge la Ujerumani kwamba washirika wa Magharibi "wanafanya kazi katika mpango mkubwa wa vikwazo" vinavyojumuisha vipengele "ikiwa ni pamoja na Nord Stream 2", akiahidi madhara makubwa kwa Urusi ikiwa itashambulia.
Hatua hiyo inajiri baada ya balozi wa Ujerumani nchini Marekani Emily Haber kutweet kwamba "hakuna kitakachowachwa ikiwa ni pamoja na mradi wa Nord Stream 2" ikiwa Urusi itakiuka "uhuru wa Ukraine".


Biashara kuu za Ulaya zimewekeza fedha nyingi katika mradi wa Nord Stream 2, ambao unaendeshwa na Kansela wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schröder.
Hivi sasa serikali ya Ujerumani inaamini kwamba "gesi asilia itaendelea kutoa mchango mkubwa katika usambazaji wa nishati nchini Ujerumani katika miongo ijayo", ikisema "ni rafiki zaidi wa hali ya hewa ikilinganishwa na mafuta mengine".
Lakini makundi mengi yanapinga Nord Stream 2. Wanamazingira wanahoji jinsi itakavyoendana na juhudi za Ujerumani za kupunguza hewa chafu na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na binadamu, huku wanasiasa wa nyumbani na nje ya nchi wakihofia kuwa huenda ukaongeza utegemezi wa Ulaya kwa nishati ya Urusi - takriban nusu ya gesi ya Umoja wa Ulaya kwa sasa inatoka Urusi.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky hapo awali ameelezea bomba hilo kama "silaha hatari ya kisiasa ya kijiografia".
Nchi yake kwa sasa inakabiliwa na takriban wanajeshi 100,000 wa Urusi walioko kwenye mipaka yake, huku hofu ikiongezeka kuwa Rais Putin anapanga kufanya mashambulizi.
Hatua za kidiplomasia
Urusi ilikuwa imetoa orodha ya wasiwasi wake kuhusu upanuzi wa Nato na masuala yanayohusiana na usalama. Miongoni mwao lilikuwa ni sharti la Nato kuondoa uwezekano wa Ukraine na wengine kujiunga na muungano huo.
Siku ya Jumatano, Marekani na Nato zilitoa jibu rasmi kwa Urusi kwa madai yake ya kutatua mzozo wa Ukraine. Halitawekwa hadharani, lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema waraka huo uliweka wazi "kanuni zao za msingi", ikiwa ni pamoja na uhuru wa Ukraine na haki yake ya kuchagua kuwa sehemu ya miungano ya usalama kama vile Nato.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema jibu rasmi haliangazii "wasiwasi mkuu" wa Urusi kuhusu upanuzi wa muungano huo. Lakini alisema kwamba "inatoa matumaini kwa kuanza kwa mazungumzo mazito", akiongeza kuwa Rais Putin ataamua jinsi ya kujibu.
Afisa kutoka wizara ya mambo ya nje baadaye alisema ilikuwa ni kipaumbele "kufikia ufahamu wa kanuni" kuhusu silaha za nyuklia, huku kukiwa na wasiwasi wa Urusi kwamba Marekani inaweza kupeleka makombora ya masafa mafupi na ya kati ndani ya eneo la Urusi. Mgogoro wa makombora ya nyuklia "hauwezi kuepukika", alisema.
Wakati huo huo, msemaji wa rais Dmitry Peskov aliwaambia waandishi wa habari kwamba Urusi itachukua "muda kuchambua" majibu
Kando na hayo, wanadiplomasia kutoka Urusi, Ukraine, Ufaransa na Ujerumani walithibitisha tena kujitolea kwao kwa makubaliano ya muda mrefu ya kusitisha mapigano nchini Ukraine, ambayo yameshuhudia waasi wanaoungwa mkono na Urusi wakiteka eneo la mashariki mwa mkoa wa Donbas.
Mataifa yote manne yanaendelea kuunga mkono usitishaji mapigano "bila kujali tofauti katika masuala mengine" kuhusiana na makubaliano ya Minsk ya 2015, taarifa iliyochapishwa na ofisi ya rais wa Ufaransa ilisema.
Naibu mkuu wa wafanyakazi wa Kremlin Dmitri Kozak alitaja mazungumzo ya saa nane mjini Paris kama "yasio rahisi", na kundi hilo linatazamiwa kukutana tena baada ya wiki mbili mjini Berlin.
Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi kwamba uamuzi wa Urusi kuja kwenye mazungumzo mjini Berlin ni "habari njema", kwani ina maana kwamba "Urusi kwa muda wa wiki mbili zijazo huenda ikasalia kwenye mkondo wa kidiplomasia".












