Mzozo wa Ukraine: Marekani yakataa dai la Urusi la kuizuwia Ukraine katika Nato

Chanzo cha picha, Reuters
Marekani imekataa dai la Urusi la kuizuwia Ukraine kuwa mwanachama wa Nato, huku kukiwa na tahadhari kuwa Urusi inaweza kumvamia jirani yake Ukraine.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alikuwa akitoa jibu lake rasmi kuhusu utatuzi wa mzozo wa Ukraine.
Katika jibu lake Blinken hakutoa hakikisho bali alisema anaipatia Urusi "njia makini ya kidiplomasia ya kuendelea mbele, iwapo Urusi itaichagua ".
Waziri wa Urusi alisema nchi yake itachunguza jibu la Bw Blinken, alilotoa kwa ushirikiano na Nato.
Urusi ilikuwa imetoa orodha ya hofu zake kuhusu kupanuka kwa jeshi la Muungano wa Nato na masuala ya usalama yanayohusiana nayo.
Miongoni mwake lilikuwa ni dai kwa Nato kuondoa uwezekana wa Ukraine na nchi nyingine wa kujiunga na muungano huo.
Katika kipindi cha wiki za hivi karibuni, Urusi imekuwa ikilimbikiza idadi kubwa ya wanajashi kwenye mpaka wake na Ukraine-kitu ambacho nchi za Magharibi zimekiona kama maandalizi ya uwezekano wa uvamizi. Urusi inakana hilo.
Bw Blinken alisema jibu la Marekani limeweka wazi "kanuni zake za msingi'' , ikiwa ni pamoja na kuhusu hadhi ya Ukraine na haki yake ya kuchagua kuwa shehemu ya miungano ya usalama kama Nato.
"Hapapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu umakini wa lengo letu inapokuja katika diplomasia, na tunachukua hatua kwa mtazamo sawa na kulazimika kuimarisha ulinzi wa Ukraine na kujiandaa kwa jibu la pamoja na la haraka kusitisha uchokozi wa Urusi," alisema.
"Kilichobaki ni jukumu la Urusi kuamua jinsi ya kujibu," aliongeza. "Tuko tayari kwa njia nyingine tofauti."
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani alisema kuwa Marekani ilituma shehena tatu za "usaidizi'' wa kijeshi wiki hii- yakiwemo makombora ya Javelin na silaha za kuzuwia makombora, pamoja na mamia ya tani za silaha na vifaa.
Mazungumzo ya siri

Bw Blinken pia alikanusha kuwepo kwa mpasuko au tofauti yoyote ya maoni baina ya Marekani na washirika wake wa Ulaya. Alisema Nato, ilikuwa imeandaa mpango wake wa mapendekezo ambao "uliimarisha kikamilifu mpango wetu, na sisi tulikuwa mpango wetu ulioimarisha wao".Lakini waraka wa Marekani wa mpango wake hautatolewa kwa umma.
"Diplomasia ina fursa bora ya kufanikiwa iwapo tutatoa nafasi kwa ajili ya mazungumzo ya siri ," alisema waziri huyo wa Marekani wa mashauri ya kigeni.
Katibu mkuu wa Nato Jenerali Jens Stoltenberg alisema kuwa waraka wa muungano huo pia ulikuwa umewasilishwa kwa utawala wa Moscow, na akasema huku akiwa tayari kusikiliza hofu za Urusi, nchi zote zina haki ya kuchagua mipango yake ya kiusalama.
Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, hatahivyo, alisema mapema siku ya Jumatano kwamba Bw Stoltenberg "hapati uhalisi", wakati alipoulizwa suala la Nato kuongeza uwepo wake karibu na mipaka ya Urusi.
"Unajua, niliacha kuzungumzia maoni yoyote ya kauli zake zamani ," Bw Lavrov aliwaambia waandishi wa habari katika Bunge la Urusi, katika matangazo ya moja kwa moja kwenye mtandao wa habari wa kijamii.
Unaweza pia kusoma:
Kando na hayo, wanadiplomasia kutoka Urusi, Ukraine, Ufaransa na Ujerumani walielezea utashi walionao wa kujitolea kufikia mapatano ya usitishaji mapigano wa muda mrefu katika Ukraine, ambao ulishuhudia waasi wa wanaoungwa mkono wakitwaa jimbo la mashariki la Donbas.

Nchi zote nne zinaendelea kuunga mkono usitishaji wa mapigano "licha ya tofauti zilizopo kuhusu masuala mengine", juu ya makubaliano ya Minsk, taarifa iliyochapishwa na ofisi ya rais wa Ufaransa ilisema.
Naibu mkuu wa wafanyakazi katika ofisi ya Waziri Mkuu wa Urusi Dmitri Kozak aliyataja mazungumzo ya saa nane mjini Paris kama "yasiyo rahisi", na kundi hilo la wanadiplomasia linatarajiwa kukutana tena katika kipindi cha wiki mbili mjini Berlin.












