Russia Ukraine: EU kuionya Moscow dhidi ya kuivamia Ukraine

TH

Chanzo cha picha, AFP

Viongozi wa Ulaya wanatarajiwa kuionya Urusi kwamba hatua za uhasama dhidi ya Ukraine zinaweza 'kuigharimu vikali' huku kukiwa na wasi wasi juu ya kuongezeka kwa idadi ya vikosi vya Urusi kwenye mpaka wa Ukraine.

Ujumbe huo, utakaokubaliwa wakati wa mkutano wa kilele wa Baraza la Ulaya mjini Brussels, utakuwa onyo ya hivi punde kutoka kwa nchi za Magharibi dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Kremlin inakanusha kuwa inapanga kuishambulia Ukraine.

Wakati huo huo, Urusi imeweka masharti yake kwa hakikisho la usalama kwa Marekani.

Idara za kijasusi za nchi za Magharibi zinaamini kuwa hadi wanajeshi 100,000 wa Urusi wamekusanyika karibu na mipaka ya Ukraine. Mamlaka ya Ukraine imesema kuwa Moscow inaweza kupanga mashambulizi ya kijeshi mwishoni mwa Januari, ingawa maafisa wa Marekani wanasema bado haijabainika iwapo Rais Putin amefanya uamuzi.

TH

Chanzo cha picha, EPA

Siku ya Jumatano, mkuu wa Tume ya Ulaya, inayoongoza EU, aliitaka tena Urusi kupunguza mvutano. Ursula von der Leyen alisema vikwazo vya ziada tayari vimetayarishwa, vikilenga "sekta zote tofauti unazoweza kufikiria".

Ujumbe wake uko wazi sana: ikiwa Urusi itachukua hatua kali zaidi dhidi ya Ukraine, gharama zitakuwa kali na matokeo yake ni makubwa," alisema.

Bado haijabainika ni nini kinasheheni vikwazo vitakavyolekezwa Urusi. Mojawapo ya sehemu zinazolengwa ni mradi wa Nord Stream 2, bomba jipya la gesi kutoka Urusi hadi Ujerumani ambalo halijaanza kufanya kazi.

Maoni yake yalikuja baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kutafuta kufufua mazungumzo na Urusi, walipokutana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, huko Brussels.

Urusi inataka hakikisho la kisheria kisheria dhidi ya upanuzi wa Nato kueleka mashariki na kupelekwa kwa silaha karibu na mpaka wake. Nato inasema shughuli zake ni za kujihami na kwamba hakuna nchi inayoweza kupinga matumaini ya Ukraine ya kujiunga na muungano huo.

Ukraine inapakana Umoja wa Ulaya na Urusi lakini ina uhusiano wa kina wa kijamii na kiutamaduni na Urusi. Wakati huo huo Urusi imeishutumu Ukraine kwa uchochezi.