Maya Angelou: Mshairi ndiye mwanamke wa kwanza mweusi katika sarafu ya Marekani

Chanzo cha picha, US TREASURY
Hazina ya Marekani imetengeneza sarafu yenye mchoro wa mshairi Maya Angelou - mwanamke wa kwanza mweusi kuwahi kuonyeshwa kwenye sarafu ya Marekani ya senti 25 inayojulikana kama 'quarter' (robo).
Angelou, mshairi na mwanaharakati, alikuwa mwanamke wa kwanza mweusi kuandika na kufanya shairi katika hafla ya kuapishwa kwa rais.
Sarafu zimepangwa kwa ajili ya wanawake wengine waanzilishi, ikiwa ni pamoja na mwanaanga, chifu wa kabila na mwigizaji - kama sehemu ya mpango wa American Women Quarters.
Hatua hiyo ilipongezwa na katibu wa kwanza wa hazina mwanamke wa taifa hilo.
"Kila wakati tunapounda upya sarafu yetu, tuna nafasi ya kusema jambo kuhusu nchi yetu - kile tunachothamini, na jinsi tumeendelea kama jamii," Janet Yellen alisema katika taarifa yake Jumatatu.
Angelou - mwandishi na mwanaharakati wa kijamii - alikufa mnamo 2014 akiwa na umri wa miaka 86.
Alijipatia umaarufu na wasifu wake wa kihistoria mnamo 1969, I Know Why the Caged Bird Sings, kuhusu maisha yake ya utotoni kule Deep South.
Alipokea digrii kadhaa za heshima na aliandika zaidi ya kazi 30 za vitabu zilizouzwa sana. Mnamo 2010, alipewa Medali ya Urais ya Uhuru - tuzo ya juu zaidi kwa raia wa Marekani - na Rais Barack Obama.
Robo mpya inaonyesha Angelou akiwa na mikono iliyofunguliwa na iliyonyoshwa. Nyuma yake ni ndege anayeruka na jua likichomoza, ambalo "limechochewa na mashairi yake na ishara ya jinsi alivyoishi", idara ya hazina ya Marekani ilisema.
Upande wa mbele wa robo unaonyesha tukio la jadi la George Washington, rais wa kwanza wa nchi.
Marekani inapanga kutoa sarafi nyingine za robo 20 zaidi katika kipindi cha miaka minne ijayo, inayoonyesha wanawake wengine wa Marekani ambao walitekeleza majukumu muhimu katika historia ya nchi.
Sarafu pia zimepangwa mwaka huu kwa Sally Ride, mwanaanga wa kwanza wa kike wa Marekani; Wilma Mankiller, chifu wa kwanza wa kike wa Taifa la Cherokee na mwanaharakati wa haki za asili; na Anna May Wong, ambaye anachukuliwa kuwa nyota wa kwanza wa filamu wa China na Marekani katika Hollywood.
Mipango ya kuchukua nafasi ya Rais Andrew Jackson katika noti ya $20 na mtu mweusi Harriet Tubman - ambaye aliwaokoa watu waliokuwa watumwa kupitia Barabara ya Reli ya Chini - bado inaendelea.
Wanawake wa kihistoria wameonekana mara chache sana kwenye sarafu ya Marekani.
Katika Karne ya 19, mke wa kwanza wa rais wa Marekani, Martha Washington, alikuwa kwenye cheti cha fedha cha $1 na shujaa wa asili wa Marekani Pocahontas alikuwa katika picha ya pamoja ya noti ya $20.
Kwenye sarafu, Sacagawea, mvumbuzi Mzawa wa Marekani, anaonekana kwenye dola ya dhahabu. Susan B Anthony na mwanaharakati mwenye ulemavu wa kuona na kusikia Helen Keller walionekana kwenye dola ya fedha na robo ya Alabama mtawalia.














