Biden amtunuku medali ya heshima mwanajeshi wa kwanza mweusi tangu vita vya Vietnam

H

Chanzo cha picha, US ARMYT

Rais wa Marekani Joe Biden ametoa tuzo ya juu zaidi ya kijeshi katika taifa hilo kwa wanajeshi watatu, akiwemo askari wa kwanza mweusi kupokea tuzo hiyo tangu vita vya Vietnam.

Sajenti wa jeshi Alwyn Cashe alikufa kwa kuchomwa moto wakati akiwaokoa wanajeshi kutoka kwa gari la kivita lililokuwa linateketea moto nchini Iraq.

Pia anakuwa mwanajeshi mweusi wa kwanza kupokea medali ya Heshima wakati wa vita vya Marekani nchini Iraq na Afghanistan.

Wanajeshi wengine wawili waliopewa sifa ya kuokoa maisha pia walipewa tuzo hiyo.

Sgt Cashe, 35, alikufa baada ya bomu lililotegwa kando ya barabara kulipulika chini ya Gari la Kupambana la Bradley alilokuwa akiliongoza mnamo Oktoba 2005, likiwasha tanki lake la mafuta.

Baada ya yeye na askari mwingine kuzima moto uliokuwa umemteketeza dereva wao na kumtoa salama, sare yake iliyokuwa imemwagiwa mafuta ya petroli ilishika moto.

Huku akikumbwa na majeraha ya moto ya kiwango cha pili na tatu kufunika karibu 75% ya mwili wake, aliokoa askari sita mmoja baaday ya mwingine na mkalimani mmoja wa Kiiraki kutoka kwenye gari hilo - wakati wote akirushiwa risasi na maadui . Alikufa kutokana na majeraha yake takriban wiki tatu baada ya shambulio hilo.

"Hakuna mwanajeshi atakayeachwa nyuma chini ya uangalizi wangu," Bw Biden alisema katika hafla ya Ikulu ya White House siku ya Alhamisi.

"Mwanajeshi ni mwanajeshi, shujaa ambaye alipita motoni kwa ajili ya askari wake," alisema, wakati mke wa Sgt Cashe na watoto wakitazama wakiwa miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo.

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Sheria zinahitaji kwamba askari wateuliwe ndani ya miaka mitano ya hatua yao ya ujasiri, lakini mwaka jana Congress ilipitisha msamaha ili Sgt Cashe apokee tuzo hiyo. Ilikuja baada ya miaka ya askari na wanafamilia kutetea medali yake ya Silver Star kuboreshwa.

Kulingana na gazeti la Washington Post, Rais wa zamani Donald Trump angetunuku Nishani ya Heshima kwa Sgt Cashe kabla ya kuondoka Ikulu ya White House mnamo Januari, lakini mpango huo uliahirishwa huku kukiwa na wasiwasi wa usalama baada ya wafuasi wa Trump kufanya ghasia katika bunge la Marekani.

Bw Biden pia alimpa Green Beret Sgt Earl Plumlee, 41, nishani ya Heshima kwa jukumu lake la kuzima shambulio katika kituo chake katika jimbo la Ghazni nchini Afghanistan mwaka wa 2013.

Baada ya waasi kulipua bomu la lori nje ya kituo chake cha kijeshi, na kusababisha kuingia kwa walipuaji wa kujitoa mhanga na washambuliaji waliokuwa na bunduki kuingia ndani, yeye na askari wengine waliweka ulinzi wa askari wao waliojeruhiwa kwa kuendesha gari katikati ya mashambulio ya risasi ya adui.

"Bila ya kujificha na kwa kupuuza kabisa usalama wake, alipambana na makali ya risasi za adui kwa bastola yake tu," kulingana na memo ya Ikulu ya White House inayoelezea ushujaa wake.

Sgt Plumlee alirushwa chini na milipuko mingi ya mabomu ya kujitoa mhanga, lakini alipata majeraha madogo tu.

"Bado sijui kwa nini hawakuweza kunipiga," aliambia Washington Post.

Mwanajeshi Sgt Christopher Celiz alikufa katika Mkoa wa Paktia nchini Afghanistan mnamo 2018 alipokuwa akisaidia majeruhi wa kusafirishwa kwa helikopta ya matibabu.

Baada ya kundi kubwa la waasi kushambulia kitengo chake, alikimbia kwenye mvua ya risasi ili kurejesha mfumo wa silaha nzito na kuchukua hatua katika mapambano, kulingana na White House.

Helikopta ilipokuwa ikijiandaa kuondoka, aliutumia mwili wake kuwa kizuizi cha kuwalinda waliokuwa ndani ya ndege hiyo wasipigwe na risasi. Ilipokuwa ikiinuka, alipigwa na risasi za adui, lakini akatoa ishara kwa askari wenzake kuendelea bila yeye.

"Alijua alipigwa, lakini aliwapungia mkono wafanyakazi wa anga kuondoka bila yeye," Bw Biden alisema. "Katika hali ya hatari kubwa, aliweka usalama wa timu yake na wafanyakazi juu ya usalama wake."