Rais Samia:Tamaa za 2025 zinaondoka

Chanzo cha picha, Ikulu
Rais wa Tanzania Samia Hassan leo ameelezea anachofikiria kinasababisha kauli zinazoonekana kupinga hatua ya serikali kuchukua mikopo ya kufanya maendeleo.
Katika hotuba yake wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, rais Samia amesema kauli hizo zinahusiana na azma ya baadhi ya viongozi kutaka kugombea kiti cha urais mwaka wa 2025 .
"Nataka niwambie ndicho kinachotokea, kwasababu huwezi kufikiria mtu miliyemuamini, mshika Muhimili aende akasimame aseme yale ni stress za 2025"
Bila kutaja jina la kiongozi yeyote rais Samia alielezea kuhusu jinsi alivyowahi kupokea ushauri kwamba 'atakayempa changamoto serikalini' sio mpinzani bali 'kijani mwenzako' akimaanisha mtu kutoka chama tawala cha CCM .
'Nisengeshangaa kama ni adui yangu ndiye kapiga kelele..aliniambia mpinzani atakutazama unafanya nini ukimaliza hoja zao hawana maneno lakini shati kijani mwenzio anayetizama mbele mwaka wa 2025…2030 huyu ndiye atakayekusumbua' rais Samia amesema
Rais Samia pia alieleza kilichojiri wakati akichukua madaraka akisema;
"Lakini jengine ni kwamba wakati mmenikabidhi huu mzigo nilianza kusikia lugha zinasema serikali ya mpito, serikali ya mpito, bungeni huko kwa kina Kassim nikarudi katika katiba nikaenda kuangalia serikali ya mpito imeandikwa wapi kwenye katiba, ikitokea nini kunakuwa na serikali ya mpito, sikuona"
Hivi karibuni Spika bunge la nchi hiyo Job Ndugai ndiye aliyekuwa ametoa tamko la kuonekana kupinga hatua ya kuchukua mikopo lakini alianda kikao na waandishi wa habari na kuomba msamaha kwa rais na Watanzania akisema kauli zake zilichukuliwa visivyo na kwamba hampingi rais wala mipango ya maendeleo ya serikali .
"Mtu na akili yake anasimama na anahoji kuhusu mikopo na tozo, sio lolote ni homa ya 2025, kwa mtu ambaye nilimtegemea kushirikiana naye kwenye maendeleo, sikutegemea kama angesimama na kusema maneno hayo.
Kwasababu huwezi kuamini mtu mzima na akili yako unaenda kuhoji tozo na mkopo wa 1.3 trilioni kama ndio kwanza imetokea Tanzania, ni uhuru wake kusema chochote lakini ni mtu mnayemtegemea, mnategemea labda atakuwa na uelewa hasa kwasababu mabajeti yote, mikopo yote taarifa za kiuchumi ni ndani ya nyumba yake ndo zinapita, lakini ni homa ya 2025" alisema rais Samia
Katika hotuba iliyojaa semi nzito kuhusu maazimio yake ya uendeshaji wa serikali na utekelezaji wa miradi ,rais Samia amesema serikali itaendelea kuchukua mikopo kwa lengo la kuleta maendeleo nchini humo
"Sifanyi kwa ajili ya 2025, nafanya ili kulketa maendeleo ya Tanzania na wenzangu msimame hivyo, baadhi yenu hampo hivyo mmeshaingia kwenye makundi hamsemi, na wenyeviti pia mmo" aliongeza rais Samia
Akidokezea uwezekano wa kufanya mageuzi ndani ya serikali rais Samia amesema;
'Nataka niwaambie nitatoa orodha mpya hivi karibuni,kwa wale wote naohisi wanaweza kwenda na mimi kwenye kazi ya maendeleo ya Watanzania nitakwenda nao lakini wale ambao ndoto zao ni kule , nitawapa nafasi wakajitayarishe vizuri huko nje tukutane mbele ya safari".















