Vita vya siku zijazo vitakuwa vya aina gani na dunia imejiandaaje?

Chanzo cha picha, Giancarlo Casem/US Air Force
- Author, Na Frank Gardner
- Nafasi, Mwandishi wa masuala wa Usalama,BBC
Mwaka wa 2021 umeshuhudia mabadiliko ya kimsingi katika sera ya ulinzi na usalama nchini Uingereza. Bajeti ya teknolojia ya kidijitali, intelijensia ya kisasa na mtandao inaongezeka. Lakini bajeti kwa zana za kitamaduni na idadi ya wanajeshi inapungua.
Haya yote yanafanyika wakati majeshi ya Urusi yanakusanyika katika mipaka ya Ukraine, Urusi imekuwa ikitaka Nato kuondoa katika baadhi ya nchi wanachama wake, na China inazidi kupaza sauti kuhusu kuirejesha Taiwan - tena kwa nguvu ikibidi.
Migogoro midogo midogo ya kikanda bado inazuka kote ulimwenguni. Ethiopia inapigana vita vya wenyewe kwa wenyewe, mzozo wa kutaka kujitenga nchini Ukraine umesababisha vifo vya zaidi ya watu 14,000 tangu mwaka wa 2014, waasi nchini Syria wazidi kupamba moto na kundi la Islamic State linaendelea kushambulia sehemu kadhaa za Afrika.
Lakini je, mustakabali wa vita vya nguvu kubwa unaonekanaje na je, nchini za Magharibi ziko tayari kwa changamoto zinazokuja?
Kwanza, "vita vya baadaye" tayari vimefika. Mambo mengi yanayohusu mzozo mkubwa kati ya nchi za Magharibi na labda, Urusi au Uchina, tayari yameandaliwa, kufanyiwa mazoezi na kutumwa.
Mnamo Novemba 16, Urusi ilifanyia jaribio kombora angani, na kuharibu moja ya satelaiti zake. Katika majira ya kiangazi China ilifanya majaribio ya makombora yake ya hali ya juu ya hypersonic, yenye uwezo wa kusafiri mara nyingi kuliko kasi ya sauti. Mashambulizi ya kukera ya mtandao, yawe ya kuvuruga au ya kuharibu, yamekuwa jambo la kawaida la kila siku.

Michele Flournoy alikuwa mkuu wa sera za Pentagon nchini Marekani chini ya Marais Clinton na Obama. Anaamini mwelekeo wa nchi za Magharibi katika Mashariki ya Kati kwa miongo miwili iliyopita umewaruhusu wapinzani wake kufanya mambo mengi ya kijeshi.
"Tuko katika hatua ambapo sisi - Marekani, Uingereza na washirika wetu - tunatoka kwenye miaka 20 ya kulenga kukabiliana na ugaidi, vita vya Iraq na Afghanistan, na tunapoinua macho yetu tunatambua kuwa tuko kwenye mashindano makubwa," anasema.
"Wakati tuliangazia Mashariki ya Kati," anasema, " nchi hizi zilijifunza mbinu za vita za nchi za Magharibi. Na zilianza kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwa teknolojia mpya."

Chanzo cha picha, J.M. Eddins Jr/US Air Force
Mengi ya haya yameelekezwa kwenye shughuli za mtandao - mashambulizi ya kuvuruga muundo wa jamii wa nchi za Magharibi, kuathiri uchaguzi na kuiba data za siri. Hii iko chini ya kizingiti cha vita na mengi yake ni ya kukanushwa.
Lakini itakuwaje ikiwa mvutano wa sasa kati ya nchi za Magharibi na Urusi juu ya Ukraine, au kati ya Marekani na Uchina juu ya Taiwan utegeuka kuwa vita? Je, hilo lingeonekanaje?
"Nafikiri hii inaweza kufanyika katika mazingira ya haraka sana ambayo yanategemea sana mitandao," anasema Meia Nouwens, mtafiti katika Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati (IISS) inayoangazia utumiaji wa data wa Uchina kwa faida za kijeshi. .
"Jeshi la China limeunda kikosi kipya kinachojulikana kama Strategic Support Force ambacho kinashughulika na anga za mbali, vita vya kielektroniki na uwezo wa mtandao."
Hii inamaanisha nini? Ni kwamba mambo ya kwanza ambayo yangetokea katika uhasama wowote itakuwa mashambulizi makubwa ya mtandao na pande zote mbili. Kutakuwa na majaribio ya kumzima mwingine kwa kuvuruga mawasiliano, ikiwa ni pamoja na satelaiti, au hata kukata nyaya muhimu za chini ya bahari ambazo hupitisha data.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hatari kubwa ya kijeshi hapa ni mgogoro wa ghfla. Iwapo setilaiti zako haziwasiliani na wapangaji wako chini ya ardhi wakiwa hawana uhakika wa kinachoendelea, basi inakuwa vigumu kupanga hatua nyingine.
Sababu moja ambayo inaweza kuwa na jukumu kubwa katika vita vya siku zijazo ni intelijensia ya kisasa. Hili linaweza kuharakisha sana wakati wa kufanya maamuzi na majibu ya makamanda, kuwaruhusu kusoma taarifa kwa haraka zaidi.
Hapa, Marekani ina makali ya ubora zaidi ya wapinzani wake na Michele Flournoy anaamini kuwa inaweza kukabiliana na maeneo ambayo Magharibi itazidiwa na idadi kubwa ya Jeshi la China.
"Mojawapo ya njia za kutatiza upangaji wa ulinzi wa wapinzani au upangaji wa mashambulizi ni kuoanisha binadamu na mashine," anasema. "Kwa hivyo ikiwa una mfumo mmoja unaoweza kudhibiti mifumo 100 isiyo na mtu, basi unaanza kuwa na usawa."
Lakini kuna eneo moja ambapo nchi za Magharibi zinajipata kenye hatari nyuma ya Urusi na Uchina. Hayo ni makombora ya hypersonic - makombora yenye nguvu nyingi ambayo yanaweza kuruka popote kati ya mara 5 na 27 ya kasi ya sauti na kubeba kichwa cha kawaida au cha nyuklia.
Urusi imetangaza majaribio ya mafanikio ya kombora lake la Zircon hypersonic, ikitangaza kuwa linaweza kushinda mifumo yoyote ya ulinzi popote duniani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Silaha ya China la Dong Feng 17, ililofichuliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2019, hubeba kombora la kuruka kwa kasi (HGV) ambalo linaweza kuzunguka anga ya mbali kwa njia isiyotabirika, na kufanya iwe vigumu kulizuia.
Majaribio ya hivi majuzi ya mifumo ya Marekani, hayajaenda vizuri. Kuwepo kwa silaha hizi katika maghala ya China sasa kunaifanya Marekani ifikirie mara mbili juu ya kuingia vitani kuilinda Taiwan ikiwa China itaamua kuivamia.

Chanzo cha picha, Giancarlo Casem/US Air Force
Uingereza imechukua uamuzi wa kupunguza nguvu zake za kawaida ili kuwekeza katika teknolojia mpya. Franz-Stefan Gady, mtaalamu wa vita vya siku zijazo, anaamini kuwa hili litazaa matunda katika muda wa miaka 20 lakini kabla ya hapo kutakuwa na pengo la kutia hofu.
"Nadhani tutakuwa na kipindi cha hatari sana ndani ya miaka mitano hadi 10 ijayo ambapo upunguzaji mwingi utatokea. Wakati huo huo, uwezo huu mkubwa wa kiteknolojia hautakuwa imekomaa vya kutosha kuwa na athari za kiutendaji," anasema.
Na hiyo miaka mitano hadi 10 ijayo inaweza yenye changamoto hatari zaidi kwa usalama wa nchi za Magharibi. Kulingana na Michele Flournoy, ambaye alitumia miaka mingi katika katika kitovu cha sera za ulinzi wa Marekani, anaamini kuwa suluhisho ni mambo mawili - mashauriano ya karibu na ushirikiano na washirika na uwekezaji katika maeneo sahihi.
"Ikiwa tutaweka akili zetu pamoja na kuwekeza katika teknolojia sahihi, dhana sahihi, na kuendelea kwa kasi , tutakuwa na uwezo wa kuzuia vita vya nguvu kubwa," anasema. "Tunapaswa kuwa na uwezo wa kufikia malengo yetu na kuweka Indo-Pacific huru na yenye mafanikio katika siku zijazo."















