Aukus: China yalaani Muungano mpya wa kijeshi kati ya Marekani ,Uingereza na Australia

Chanzo cha picha, Getty Images
China imekosoa muungano wa usalama wa kihistoria kati ya Marekani, Uingereza na Australia , ukiutaja 'uliokosa kuwajibika kwa kiasi kikubwa na wenye maono finyu'.
Makubaliano hayo yatazifanya Marekani na Uingereza kuipatia Australia teknolojia ya kujenga manowari zenye uwezo wa kinyuklia kwa mara ya kwanza.
Inaonekana kwa kiasi kikubwa kama juhudi za kuukabili ushawishi wa China katika eneo la kusini mwa China linalozozaniwa.
Eneo hilo limeangaziwa kwa muda mrefu na hali ya wasiwasi bado ipo juu.
Msemaji wa wizara ya masuala ya kigeni nchini China Zhao Lijian alisema kwamba muungano huo unahatarisha kuharibu amani ya eneo hilo na kuongeza kiu cha ubabe wa umiliki wa silaha.
Alikosoa kile alichokitaja ''mawazo ya vita baridi '' na kuonya mataifa hayo mawili kwamba yalikuwa yanaumiza maslahi yake yenyewe.
Vyombo vya habari nchini China viliandika vichwa vya habari kama hivyo vikiukosoa muungano huo, huku kimoja cha Global Times kikisema kwamba Australia sasa imejiweka miongoni mwa wapinzani wa China.
Marekani inagawanya teknolojia yake ya kujenga manowari kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 50 , baada ya kugawana ujuzi huo na Uingereza pekee hapo awali.
Hiyo ina maana Australia sasa itaweza kujenga manowari ze nye uwezo wa kinyuklia ambazo zitakuwa na kasi na vigumu kuzitambua ikilinganishwa na manowari za kawaida.
Zinaweza kusalia ndani ya maji kwa miezi kadhaa na kurusha makombora kwa umbali mkubwa - ijapokuwa Australia inasema kwamba haina nia ya kuweka silaha za kinyuklia ndani yake.
Muungano huo mpya, chini ya jina Aukus, ulitangazwa katika mkutano wa pamoja na vyombo vya habari kati ya rais Joe Biden , waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson na mwenzake wa Australia Scott Morrison siku ya Jumatano jioni na Alhamisi asubuhi.
Na huku China ikitajwa moja kwa moja , viongozi hao watatu walitaja mara kwa mara maeneo ya usalama yanayotiliwa shaka ambapo walisema kwamba hali ya wasiwasi ipo juu.
"Hii ni fursa ya kihistoria kwa mataifa matatu , yalio na washirika sawa ili kulinda mali zao na kuimarisha usalama katika eneo la Indo Pacific ,ilisema taarifa ya pamoja.
Je ni taifa gani lililo na manowari nyingi zinazotumia nguvu za Kinyuklia?













