Sara Jayne: Mtoto mweusi aliyetolewa na mamake mzungu ili kuasiliwa na familia nyengine kutokana na rangi yake

Mwaka 1980 mtoto wa kike alitolewa kwa ajili ya kuasiliwa kwa kuwa alikuwa na rangi ya mwili ambayo ni kosa -alikuwa ni mweusi, wazazi wake walikuwa ni wazungu, na ulikuwa ni wakati wa enzi za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Lakini kuwa alikuwa amelelewa na wenzi wazungu nchini Uingereza kulimfanya atafute nafasi yake katika dunia. Aliipata nafasi yake wakati aliporejea katika nchi alikozaliwa.
Wakati ndege ilipokuwa ikitua mjini Johannesburg, Sara-Jayne King alivuta pumzi. Zaidi ya miaka 25 ilikuwa imepita tangu alipoiona Afrika Kusini kwa mara ya kwanza.
Hakuwa na kumbukumbu ya Afrika Kusini. Aliondoka Johannesburg akiwa mtoto mchanga mwenye wiki saba, ili kupelekwa kwa mama yake mzazi aliyekuwa Uingereza.
Miaka ya katikati haikuwa rahisi. Sara-Jayne hakuwahi kufahamu kuwa alitelekezwa na mama yake aliyemzaa, na alihangaika kuishi kama mtoto mweusi anayeishi katika jamii ya watu wenye kipato cha kati.
Alitoka ndani ya ndege, akatembea kwenye uwanja wa ndege na kuelekea kwenye gari ambalo lingempeleka katika kituo cha kurekebisha tabia.
Hapa , Sara-Jayne alitumai kuondokana na tabia ya kujidhuru na kurekebisha aina fulani ya maisha yake.
Wakati alipokuwa akiendeshwa ndani ya gari njiani, aliona kitu ambacho alikikumbuka . "Nimewahi kuwa hapa kabla," alifikiria. "Nimewahi kuwa hapa kabla, na mimi ni wa hapa."
Alipokuwa akikuwa katika nyumba za kaunti, Sara-Jayne alifahamu kuwa alikuwa na muonekano tofauti na wazazi wake, lakini hakuwahi kudhani "mweusi'' kuwa ndio utambulisho wake, hadi wengine mjini walipomuambia kuwa yeye ni mweusi.
Wanafunzi aliosoma nao mara kwa mara walizigusa nywele zake, wakimwambia zinafanana kama waya wa chuma.
Kwa muda mrefu, Sara-Jayne alikuwa ndiye msichana mweusi pekee aliyemfahamu katika eneo alilokuwa akiishi. Wengine walimwambia kuwa alikuwa tofauti, kwahiyo alihisi ni tofauti na wenzake. "Huwa tunabeba maoni ya watu wengine," anasema.

Kidogo kidogo, Sara-Jayne alianza kuhisi kuna kitu ambacho hakiko sawa kwa kuwa mweusi.
Kuhangaika na asili yake pamoja na kuasiliwa vikawa ni sehemu ya maisha yake, vikawa vinamkumbusha kuwa hana sura ya wazi ya utambulisho wake.
Hii ilimaanisha kuwa mweusi, au raia wa Afrika Kusini au kuasiliwa- yote haya yaliendelea kuzunguka akilini mwa Sara-Jayne. Alijihisi ametengwa na kwamba yuko peke yake.
Maelezo kuhusu kuasiliwa kwake yalikuwa hayaridhishi. Aliambiwa kuwa mama aliyemuasili hakuweza kupata mtoto, na kwamba yeye mwenyewe alikuja kutoka Afrika Kusini. Na hayo ndiyo maelezo pekee aliyopewa.
Alikuwa na kaka mmoja mkubwa ambaye pia aliasiliwa na alikuwa mweusi.
Mahala pekee ambapo alipata taarifa kuhusu watu weusi ilikuwa ni televisheni ya Uingereza miaka ya 1980, ambayo anasema haikutoa taarifa za ukweli ila kuwasifia watu weusi.
Zaidi ya hayo hakuwa na taarifa nyingine za kuhusu watu wenye asili za rangi .
"Nilikuwa ninaamka kila asubuhi na kutazama nje, mbele kulikuwa na uwanja na kutazama kuku na kondoo ," anasema,''kusema kweli nilikuwa nikiishi maisha fulani ya kizungu, ya familia ya kiwango cha kati ."

Katika kijiji cha, Crowhurst, Waafrika walikuwa wakiangaliwa kama masikini. Shule yake ilikuwa ikifanya mchango wa chakula kwa ajili ya msaada wa watoto wenye njaa nchini Ethiopia. Sara-Jayne anakumbuka akiwaona watoto waliokuwa na nzi machoni na barabara za vumbi na kufikiria kuwa hayo ndio mazingira anayopaswa kuishi pia.
Ingawa Sara-Jayne aliamini kwamba kuwa mtu mweusi ni kitu kibaya, alifahamu mapema kuwa weusi na rangi ya kahawia huja kwa viwango tofauti. Huku weusi wake haukuwa unaofaa, wengine ' wanaweza kuvutiwa.
Alipokuwa na umri wa miaka minane, wasichana kutoka Mauritius walihamia mjini. Walikuwa warembo, na nywele laini zenye mawimbi na ngozi nyororo.
Walikuwa na rangi ya mwili ya kahawia inayofaa
Wakati huo huo nywele za Sara-Jayne zilikuwa ngumu kuzitunza. Kila Jumapili asubuhi baba yake alihangaika kuzichana huku Sara-Jayne akilia kwa uchungu.
Ni kitu ambacho alihisi kilimuumiza hadi alipoziwekea kemikali ya nywele ya kulainisha (relaxer) kwa mara ya kwanza alipofikia umri wa kubalehe.
Licha ya nia yao njema, familia yake ilizidisha hisia za kujitenga. Sara-Jayne anakumbuka wakati mmoja alipokuwa akitazama michezo ya Olympiki ya majira ya joto na bibi yake.
Wakati mashindano yalipoanza, alimgeukia Sara-Jayne, akimfahamisha kuwa ataishabikia Uingereza na mjukuu wake anaweza kuishabikia "Afrika".
Akiwa na umri wa miaka 14, Sara-Jayne alifanya uvumbuzi ambao haukutarajiwa.
Wakati alipokuwa akizunguka katika chumba cha mama yake, aligundua barua kutoka kwa mama yake mzazi, iliyoandikwa karibu mwaka mmoja baada ya kuzaliwa kwake.
Barua ilikuwa ameandikiwa yeye
Aliifungua na akaanza kuisoma. Hadithi ya kuasiliwa kwake, maelezo yaliyomshitua, yakafichuliwa kwake.
Alifahamu kuwa mama yake mzazi, mwanamke mzungu Muingereza ambaye alikuwa na mahusiano ya ndoa na mzungu, alikuwa na mahusiano na kimapenzi na mwanaume Mwafrika.
Alipopata ujauzito, hakuwa na uhakika ni mwanaume gani alikuwa ni baba yake. Mtoto alionekana mzungu alipozaliwa na mama yake akamuita mtoto mchanga Karoline.
Lakini siku chache baadaye mama yake aligundua kuwa mtoto kwa kweli hakuwa mzungu. Karoline alikuwa ni mtoto wa mwanaume mweusi -, na kuishi kwake hakukuwa chanzo cha mzazi, bali ni karaha iliyopaswa kushugulikiwa.
Wakati Karoline alipozaliwa, Afrika Kusini ilikuwa na sheria inayozuia mahusiano ya kingono ya watu wa rangi tofauti, na Karoline alikuwa ni ushahidi wa mahusiano yasiyokubalika kisheria.
Kwahiyo mama yake mzazi na mume wake, pamoja na daktari wao, waliandaa mpango. Walidai Karoline alikuwa na ugonjwa nadra sana wa figo na alihitaji matibabu ya haraka na ya kisasa ya ngozi mjini London.
Lakini mara moja walimtoa kwa ajili ya kuasiliwa. Waliporejea Afrika Kusini mikono mitupu, mama yake mzazi na mumewe walimuambia kila mtu nyumbani kwamba Karoline alikuwa amefariki.
Sara-Jayne alihangaika sana kwa kuelewa kwamba mama yake alikuwa amemuacha na kumtoa na hata kudanganya kuwa alikuwa amekufa .
. "Rangi ya mwili wangu ilikuwa ya kuchukiza sana, na kile wazazi wangu halisi walichokifanya kiliwakera sana, kiasi kwamba nililazimika kutolewa kutoka kwenye ardhi ya nyumbani na kukuzwa mahali kwingine," anasema.
"Nilihisi hisia hizi kwamba… ni kwa jinsi gani mtu anaweza kuwa na hofu kiasi kwamba mtu anayefaa kumpenda, kukujali, kukupa maadili kwa vyovyote vile, anaweza kufanya kile mama mzazi alikifanya, ambacho kilikuwa ni kutoa mtoto wake aende mbali naye ."

Hii hasira ya hisisa ya kukataliwa ilianza kujitokeza yenyewe hata kabla Sara-Jayne hajasoma barua. Aliwahi kunywa dozi zaidi za dawa ya Paracetamol alipokuwa na umri wa miaka 13. Baadaye alianza kujikata kata mwenyewe.
Miaka michache baada ya kusoma barua, alipokuwa katika mwaka wa kwanza wa chuo kikuu akisomea masomo ya sheria katika Chuo kikuu cha Greenwich, aliwasiliana na mama yake mzazi kupitia shirika la uasili.
Alijibu, akisema kuwa atajibu maswali ya Sara-Jayne, lakini baadaye hakuwa na shauku ya kuendelea kuwasiliana naye. Hakuelezea kujutia kitendo alichofanya wala kuomba msamaha.
Katika kipindi hiki , Sara-Jayne alianza kushindwa kula vyema na akaanza kujitibu mwenyewe kwa kunywa pombe na kutumia dawa ya kulevya ya codeine. Licha ya hili, alikamilisha masomo yake ya shahada na kupata stashahada ya uandishi wa habari katika Chuo kikuu cha Canterbury. Alipata kazi nzuri sana, akahama kutoka Uingereza akaenda Dubai na kuanza kupata mafanikio ya kitaaamu akiwa mtangazaji wa radio.
Lakini maisha yake ya nyuma yaliendelea kumuwinda kama wingu ambalo hakuweza kuliepuka. Baba yake aliyemuasili hakuwa maishani mwake tena, kaka yake alijiua na mama yake halisi alikuwa amemkataa kwa mara ya pili .
Kutokana na kuendelea kuhangaika na matatizo ya kula vizuri, pombe na kujidhuru mwenyewe alifutwa kazi mjini Dubai. Hatimaye, alifikia wakati ambapo alikuwa hajiwezi.
Ilikuwa ni mwaka 2007 na ilikuwa wakati ambapo Sara-Jayne aliamua apate usaidizi na akagundua kuwa mahali anapaweza kupata usaidizi wa kurekebisha mienendo na hali yake angeupata Afrika Kusini ambako huduma hii ilikuwa ni nafuu.
Kuishi kwake Johannesburg kumemuweka Sara-Jayne katika njia ya kuelekea kujiondoa katika limbo la hisia na matumizi ya dawa ya kulevya , ana matumaini kuwa kurejea kwake kutamponya majeraha hayo .

Miaka miwili iliyopita, Sara-Jayne alitoa kitabu kilichoelezea hali zake za kuasiliwa na masaibu aliyopitia baada ya kuasiliwa.
Alikuwa amemkodisha mchunguzi wa kibinafsi kumsaidia kumpata baba yake halisi aliyemzaa bila mafanikio.
Halafu, wakati alipokuwa akinadi kitabu chake redioni, alitaja jina lake. Hapo ndipo Twitter ilipoingilia kati. Katika kpindi cha saa 36 baada ya kipindi cha redio, alikuwa amepokea simu ya baba yake. Aliipiga, kwa mara ya kwanza, akasikia sauti ya baba yake kwa njia ya simu. Waliongea kwa dakika 30.
Wawili hao walianza kuongea kila siku kwa wiki kabla Sara-Jayne kupanda ndege kuelekea Johannesburg kukutana na baba yake ana kwa ana. Walipanga kukutana katika mgahawa katika duka moja la bidhaa (shopping mall).
Ilikuwa ni siku bora zaidi katika maisha yake . "Sitawahi kumsahau akitembea kuja nilipokuwa, na sote tukaangua kilio, akanikumbatia na kusema, 'Binti yangu, binti yangu,'" anasema. "Ghafla nikasikia msisimko nikajiuliza, mimi ni binti ya mtu fulani. Mimi ni binti wa mtu, ninayetoka kwake ."
Miaka miwili baadaye. Sara-Jayne anafikiria uwezekano wa kubadili tena jina zaidi- kuongeza jina la baba yake la mwisho kwenye majina yake na kuwa Makwala King.
Ingawa anaishi Cape Town, akifanyika kazi kipindi cha Cape Talk radio, huwa anasafiri mara kwa mara kwenda Johannesburg kumuona baba yake na ndugu zake watatu. Bado ana uhusiano wa karibu na mama aliyemuasili nchini Uingereza, lakini anafurahia zaidi kuipata familia yake ya Afrika Kusini.
Na sasa anahisi kuwa mwenye kujiamini na utambulisho wake halisi kama Mwafrika Kusini mweusi. Hajihisi kwa kweli kuwa Muingereza.
Wakati wengine wanapojaribu kumwambia kuwa ni Muingereza , hilo halimbabaishi tena kama ilivyokuwa . "Ninadhani kwa baadhi ya watu bado wanapata ugumu wa kutambua kuwa ukweli ni kwamba hauwezi kuniamulia mimi ni nani na jinsi ninivyojitambua," anasema. "Siwezi kujali ni jinsi gani watu wengine wavyofikiri ninapaswa kujitambua mwenyewe."












