Waridi wa BBC: Apata mapacha akiwa na umri wa miaka 52

Jemima Okutu na mwanawe

Chanzo cha picha, Jemima Okutu

Maelezo ya picha, Jemima Okutu na mwanawe
    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Jemima Okutu, kutoka nchini Kenya, amekuwa na tabasamu mwanana tangu Aprili 14, 2021, baada ya kupata watoto mapacha.

Tabasamu lake sio kwa kupata tu mapacha, ila kwa kupata mapacha akiwa na umri mkubwa wa miaka 52 baada ya kuhangaika kwa miaka mingi.

Wakati wote sasa amekuwa na uso wa tabasamu anapowabeba watoto wake.

Hii ni baada ya kuwapata wanawe wawili ambao ni pacha, Katika umri alionao mwaka huu wa miaka 52.

Ni nadra sana kwa wanawake wa umri wa aina yake kupata mtoto ama watoto, kwa sababu za kibaiolojia.

Jemima ni mzaliwa wa eneo la magharibi mwa Kenya, ambapo akiwa msichana mdogo alitamani kwamba siku mmoja atajaliwa mume, kisha watoto. Ndoto hii yake haijatokea kama alivyopanga akilini mwake ila kwa sasa anashukuru tu kwa kujaaliwa watoto ambao muda huu wana miezi mitatu .

"Kitu ambacho ninaweza kukisema tu , ni 'ahsante kwa mwenyezi Mungu' . Nilikuwa nimefika mwisho wa kutafuta watoto , huu ni muujiza na kamwe sichukulii hali hii kuwa ya kawaida."anasema Jemima

Kutimiza ndoto zake

Mpango wake Jemima ulikuwa kuhakikisha kuwa wazazi wake, kaka na dada zake, pamoja na jamaa wengine wa karibu wako sawa kimaisha. Upeo huu ulitokana na kwamba mwanamke huyu hakuzaliwa kwenye jamii ya utajiri au wastani, alitoka katika jamii ya ufukara.

Mtoto wa Jemima

Chanzo cha picha, Jemima Okutu

Maelezo ya picha, Jemima Okutu

Kwa hiyo yeye alitamani kubadilisha sura ya jamii yake kwa vyovyote vile.

Akiwa binti alihakikisha kuwa shuleni anafaulu masomoni, kuingia chuo kikuu na kufaulu.

Wakati wanawake wenzake walipokuwa wanashika mimba, wengine kuolewa yeye alikuwa anafanya juu chini kuhakikisha kuwa watu katika jamii yake hawakosi elimu au vitu vya msingi maishani.

"Sijui kama nilifanya uamuzi wa busara wa kuchagua kuelimisha kaka na dada zangu pamoja na watu wengine wa karibu na ukoo wangu, kwani hili lilichukua miaka mingi sana, nilijisahau na kuweka mahitaji ya watu wetu kwanza, katika mawazo yangu nilikuwa nawaza kuwa nitakuwa tayari kushughulikia mahitaji yangu baada ya kuhakikisha kuwa kila mtu katika familia yangu amekamilisha masomo yake."anasema Jemima

Chaguo lake hili japo anasema ni jema lakini lilichelewesha sana muda ambao angepata mchumba au mahusiano ya kimapenzi, aghalabu anavyoona kwa wakati huu.

Baada ya Jemima kukamilisha masomo, wazazi wake waliaga dunia. Na alipopata ajira, anasema mshahara wake wakati huo haukuwa mkubwa ukilinganisha na majukumu ambayo alikuwa nayo. Ilibidi awachukue dada na kaka zake na wakaanza kuishi pamoja nyumba moja.

"Nilipoanza kupokea mshahara wangu nilikuwa nawazia nani atachukua pesa ngapi kwa masomo na matumizi, nilisubiri wakamilishe masomo yao kwenye taasisi na vyuo vikuu ,kwanza, "anakumbuka mwanamke huyo

Anasema kutokana na uamuzi huo, ulimfanya kukaa mbali sana na hali ya kuchumbiwa au kushika mimba.

Bilashaka anasema kuwa alikuwa anawaona wenzake wameolewa wamejaaliwa watoto, wengine wameachwa na kuanza kulea watoto pekee yao. Kwa hio hali kama hizo zilimpa hata msukumo zaidi wa kusimama kidete na uamuzi wake.

"Vile vile kuna wakati ambao si kuwa na mawazo ambao chanya kuhusu ndoa na watoto, kutokana na kushuhudia talaka hapa na pale , hapa ninamuona rafiki yangu anateseka kulea pekee yake baada ya ndoa kuvunjika , kwa hio nilikuwa na hoji kuwa mimi sio malaika , huenda nitafanyiwa sawia na wao ikiwa nitaingia kwenye ndoa .Na hilo lilinisukuma nje ya mawazo ya ndoa "anasema Jemima .

Mama huyu wa pacha anasema kuwa wakati kama huo , msimu wanawake wa rika yake walikuwa wanashika mimba na kwa wengine kuingia kwenye mahusiano , shinikizo lilikuweko kutoka kwa shangazi wake . Aidha anasema kuwa siku nyingi baadhi ya shangazi zake walijaribu juu chini kumumtafutia mwenza , ila bado alikuwa na misimamo mikali.

Baada ya kuona kuwa ndoto yake ya kuwasomesha dada na kaka zake kutimia, alianza kuwa na mawazo ya kwamba ni wakati naye aanze mchakato wa ndoa. Lakini sasa changamoto ilikuwa kwamba kutokana na umri kusonga alikuwa hapati mpenzi ambaye alihitaji ndoa. Jemima alikuwa hataki kuwa mke wa pili wala watatu. Hilo lilianza kuwa changamoto kwa asijue la kufanya .

Jemima Okutu

Chanzo cha picha, Jemima Okutu

"Nilipotimiza umri wa miaka 40 nilihisi kwamba nilikuwa tayari kwa ndoa na watoto, tatizo likawa kuwa wanaume wa rika langu walikuwa hawapatikani, wengi walikuwa tayari ni waume za watu, nikaanza kuwa na wasiwasi iwapo nitaweza kushika mimba , kwani umri nao ulikuwa umeenda , sikukata tamaa ya kujaaliwa mtoto , ila nilikata tamaa ya kuolewa"anakumbuka Jemima

Sio kila siku mwanamke atakiri kuwa aliamua kutafuta mtoto kwa kushiriki tendo la ndoa na mwanaume kisha atoroke bila kumjulisha mwenzake kwamba ameshika mimba. Ila kwa Jemima alipofika umri kati ya arobaini hadi arobaini na nne aliamua kuingia kwenye mahusiano kadhaa na wanaume , ila pindi alipoanza kujaribu kushika mimba kwa njia ya kawaida ilionekana kuwa ngumu .

Jemima alishindwa kupata ujauzito alipofikisha umri wa miaka 46.

"Wakati ninajaribu kushika mimba kwa njia ya kawaida , na nikawa sishiki , nilikuwa namuona daktari wangu , na kila alipofanya vipimo ilionekana kila kitu kiko shwari katika sehemu zangu za uzazi . Ila nilizidi kuhofia kuwa nitakuwa mwanamke ambaye hana mtoto maishani mwangu "anasema Jemima.

Akiwa na umri wa miaka 45 na 46 hedhi yake ilifika kikomo na akawa sasa ameingia kipindi ambacho mwanamke husemekana hawezi kujifungua kibiolojia . Jemima alizidi kuwa na hofu.

Mojawapo wa hofu kuu ilitokana na kuwa alihisi upweke , wengi wa watu wa jamii yake na pia kaka na dada aliosaidia kuwasomesha , walikuwa wameanza maisha yao. Alihisi kutengwa na marafiki zake kwa kukosa mume na mtoto.

"Mwaka uliopita nikiwa na umri wa miaka 51 nilipiga moyo konde na kuamua kufuata njia za utafiti wa kisayansi kushika mimba , nilihoji kuwa wakati ninaingia umri wa uzee wangu , ni nani atanisitiri?licha ya umri wangu kwenda nilikuwa na imani ya kujaaliwa mtoto , kwa hiyo niliamua kutafuta usaidizi wa matibabu kama hayo kutoka kwa daktari mmoja nchini Kenya "anasema Jemima

Wakati Jemima anaanza kutafuta matibabu , Daktari mmoja wa afya ya uzazi wa kina mama alimweleza kwamba kuna uwezekano wa yeye kupata mimba ya kisayansi , anasema alianza kutumia dawa za homoni na ya uzazi. Madawa haya yalikuwa yamuwezeshe kurejesha hedhi zake.

Mwezi Juni, 2020 hedhi za mwanamke huyu zilirejea baada ya hapo, mpango wa uzazi wa kisayansi ujulikanao kama IVF (Invitro Fertilization) ulianzishwa - Jemima hakuwa na mwenza wa kutoa mbegu, hivyobasi hospitali ilichanga mbegu za kumwezesha mwanamke huyu kushika mimba .

"Baada ya jaribio la kwanza pekee nilipewa habari njema kuwa utafiti wangu ulifaulu, Vipimo viliashiria kuwa nilikuwa nimeshika mimba ya pacha , nilishikwa na msisimko usioeleweka."anakumbuka Jemima

Miezi ya minne ya kwanza, Jemima hakuambia mtu yeyote kwamba alikuwa mjamzito, ila kuanzia mwezi wa tano uja uzito wake ulianza kuonekana , kazini mwanadada huyu anasema kuwa wengi walishangaa , na hali ya minong'ono ilianza kuhusu hali yeke. Anasema kuwa waliokuwa na ujasiri walimuuliza ili kuelewa, kwa namna gani ameshika ujauzito kutokana na umri wake?

Jemima Okutu,

Chanzo cha picha, Jemima Okutu,

"Wengi walishangaa, watu wengi wanaonifahamu walikuwa wamekataa tamaa kuhusu uwezekano wangu wa kushika mimba au hata kuolewa , ila kwa upande wangu nilijikaza na safari ya maisha yangu huku nikijitayarisha kuwapokea watoto wangu "Jemima anakumbuka.

Tarehe 14 mwezi Aprili mwaka huu ni mojawapo ya siku ambazo Jemima hatasahau maishani mwake , akiwa na ujauzito wa wiki 34 , Daktari wake alifanya uamuzi wa kufanyiwa upasuaji, na akafanikiwa kupata watoto wake mapacha.

Akaanza kuitwa mama, na kuanza safari ya kunyonyesha akiwa na umri wa miaka 52 .

Je daktari wake alisema nini?

Dkt. Kireki Omanwa ni Mshauri wa maswala ya afya ya uzazi kwa wanawake. Alihusika na suala la Jemima, BBC ilipomuuliza alisema kwamba wanaotaka kupata watoto wakiwa na umri mkubwa kwanza wanachopaswa kufanya ni mchakato wa utambuzi ambapo vipimo anuwai hufanywa ili kujua matatizo yao.

Dr Kireki Omanwa

Chanzo cha picha, Dr Kireki Omanwa

Maelezo ya picha, Dr Kireki Omanwa ni Mshauri wa maswala ya afya ya uzazi kwa wanawake

Hapo ndipo mtaalam atawasilisha aina tofauti ya tiba , kulingana na kiwango cha utasa. Tiba hiyo inaweza kuwa IVF (In Vitro Fertilisation- ambapo mayai na mbegu za kiume huchanganywa pamoja kisha kiini tete huhamishiwa ndani ya tumbo la mama.

Kwa wagonjwa ambao hawana hedhi kwa mfano kutokana na umri wao ama uzee, au baada ya matibabu na matumizi ya madawa mengine kama vile kutibu saratani (chemotherapy) au hata wanapozaliwa hivyo, kuna matibabu ya kushawishi hedhi kwa kutumia dawa za homoni .

'Ikiwa tungependa kushawishi hedhi tunaweza kuileta kwa mwanamke yeyote inategemea kwanini ifanyike', alisema.

Daktari huyo anasema pia mchango wa manii au hata msaada wa yai ni jambo ambalo hufanywa katika utalaam maalum. Kuna njia mbili za kupata mfadhili na mtu anaweza kupata mfadhili anayejulikana (dada / kaka, binamu, rafiki au jamaa) au wafadhili wasiojulikana, ambapo mpokeaji na wafadhili hawafahamiani .

Kawaida kuna ukaguzi ambao hufanyika kabla ya chochote - kwa mfano kujua historia ya jumla ya matibabu na upasuaji wa wafadhili au wanaotoa mbegu, magonjwa yoyote au hata ya kurithi katika familia, ikiwa mfadhili ana mtoto au watoto kabla ya matibabu kuanza.

Daktari Kireki anasema "Gharama ya matibabu hutofautiana kulingana na kile kinachofanyika na iwapo kuna mayai na manii na ikiwa tunatumia mayai na manii yaliyotolewa na watu wengine. Iwapo IVF inafanyika basi gharama inatofautiana kutoka mahali popote na hufikia karibu kati ya dola 40 mpaka 75

Je matibabu haya hufaulu kwa kiwango gani?

"Viwango vya mafanikio hutegemea mambo mengi sana mfano kama tumbo lina nyuzi, ikiwa mgonjwa anaugua ugonjwa sugu mfano shinikizo la damu, ugonjwa wa kisukari, ugonjwa wa damu, sababu ya kuvuta sigara / matumizi ya pombe na kadhalika.

Kwa ujumla kote duniani viwango vya mafanikio hutofautiana, lakini vinafikia kati ya 30-50%."