Irani dhidi ya Israeli: Je, kushambuliwa kwa meli iliyotoka Dar es Salaam kuzitumbukiza nchi hizo katika vita vya wazi?

Chanzo cha picha, Reuters
Irani na Israeli ni nchi hasimu kwa miongo kadhaa sasa: kila mmoja akimtazama mwenziwe kama adui mkubwa wa usalama wake na wa ukanda mzima wa Mashariki ya Kati.
Lakini katika miaka ya hivi karibuni uhasama baina ya nchi hizo umegeuka na kuwa kile wachambuzi wa masuala ya usalama wanakiita 'vita ya chini kwa chini.'
Vita hivyo vilianza ardhini kisha angani, lakini katika matukio ya hivi karibuni zaidi uwanja wa mapambano umekuwa ni bahari: meli na boti kadhaa zimeshambuliwa katika Ghuba ya Omani.
Tukio la hivi karibuni zaidi ni kushambuliwa kwa meli ya mafuta ya MV Mercer Street, mnamo Julai 29. Meli hiyo ambayo ilikuwa imetoka kushusha mafuta kutoka bandari ya Dar Es Salaam ilishambuliwa ikiwa njiani kuelekea katika bandari ya Fujairah, iliyopo katika nchi ya Falme za Kiarabu (UAE).
Meli hiyo ambayo ilikuwa ikipeperusha bendera ya Liberia inamilikiwa na kampuni ya Japani lakini inaendeshwa na kampuni ya Israeli inayoitwa Zodiac Maritime.
MV Mercer Street kwa ndege isiyokuwa na rubani ambayo ilikuwa imesheheni vilipuzi.
Watu wawili waliuawa: walinzi wa meli hiyo ambao ni raia wa Romania na Uingereza.
Baada ya kuomba msaada wa dharura, meli hiyo ilisindikizwa mpaka bandarini na manowari mbili za jeshi la Marekani.
Marekani, Uingereza na Israeli zinaishutumu Irani kwa shambulio hilo, wakisema ni kinyume cha seria za kimataifa na halikubaliki.
Irani, imekanusha kuishambulia meli hiyo ikisema shutuma dhidi yake hazina msingi wowote. Hata hivyo, Marekani inasema ina ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa shambulio hilo limetekelezwa na Irani.
Katika tukio lengine liltokea mwezi Aprili, Israeli ilishutumiwa kuwa nyuma ya shambulio la ajabu dhidi ya meli ya jeshi la Iran iitwayo Saviz katika bahari ya Shamu.
Haya ni matukio mawili tu kati ya mengi kwenye miezi ya hivi karibuni yaliyohusisha meli ambazo zinauhusiano na Irani ama Israeli.
"Ni mchezo hatari wa mashambulizi ya kuviziana ikiwemo kuuawa kwa wanasayansi wabobevu wa nyuklia wa Irani ambao wanadaiwa kuuawa na Isreali inayohaha kuizuia nchi hiyo isifanikiwe katika mpango wake wa maendeo ya urutubishwaji wa madini ya urani ambayo hutumika kutengeneza silaha za maangamizi," anaeleza mwandishi wa masuala ya usalama wa BBC, Frank Gardner.
Katika matukio yote hayo, nchi hizo mbili zimeendelea krushiana kidole cha lawama na kwa hali ya mambo ilivyo, kuna uwezekano mkubwa vita hivyo vya chini chini vikachukua sura mbaya zaidi, japo wote Irani na Israeli wamekuwa waangalifu na kujizuia kutumbukia katika vita vya wazi.
Hata hivyo suala la wapi vita hii inaelekea linaweza kuwa na majibu tofauti kwa kuwa nchi hizo mbili hivi karibuni zimepata viongozi wapya na wote wawili wana misimamo mikali. Je, misimamo ya viongozi hao inaweza kuzitumbukiza nchi hizo kwenye vita vya wazi?

Chanzo cha picha, Reuters
Maadui wapya wawili
Matukio ya hivi karibuni, hata hivyo, yanafanyika wakati kuna wahusika wakuu wawili katika vita hivi vya chini kwa chini. (shadow war)
Mmoja ni rais mpya wa Irani, Ebrahim Raisi, mshirika wa karibu wa Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, na anayejulikana kwa upinzani wake dhidi ya Israeli, ambayo ameiita "tishio la hatari."
Wa pili ni waziri mkuu mpya wa Israeli, Naftali Bennett, ambaye tayari ameonesha kuwa msimamo wake ni dhidi ya Irani kama ule wa mtangulizi wake, Benjamin Netanyahu.
Christoph Bluth, Profesa wa Uhusiano wa Kimataifa na Usalama katika Idara ya Mafunzo ya Amani na Maendeleo ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Bradford nchini Uingereza, haamini kwamba uteuzi huu mpya bado umeathiri vita hivi vya chini kwa chini
"Haiwezekani kwamba mabadiliko katika uongozi hadi sasa yameleta mabadiliko makubwa katika sera [za nchi zote mbili]," mtaalam huyo alielezea BBC Mundo.
Badala yake, anasema Profesa Bluth, itaonekana kuwa moja ya sababu kuu zinazoongoza vita hivi vya chini kwa chini ni juhudi za waziri mkuu mpya wa Israeli kumshawishi Rais wa Marekani Joe Biden asifufue mpango wa nyuklia wa Irani.
"Hili linaonekana kuwa jambo muhimu sana la kuhimiza, kwani Israeli imekuwa ikiongeza mashambulizi kwa meli za Irani kama njia ya kuuchochea mzozo, ambao umesababisha mapigano na Irani''.

Chanzo cha picha, EPA
Kwa kweli, matukio yote mapya ya vita vya chini kwa chini kati ya Irani na Israeli vinafanyika wakati mazungumzo yanafanyika Vienna, Austria, kujaribu kufufua makubaliano ya nyuklia na Irani ambayo yatapunguza mpango wa nyuklia wa Irani kwa makubaliano ya kuondolewa kwa vikwazo.
Na kama vile Frank Gardner anaelezea, wote nchini Iran na Israeli, wengi wanapinga kuanza tena kwa makubaliano haya ya nyuklia.
"Kuna watu wengi nchini Irani ambao wanapinga makubaliano ya nyuklia, ambao hawaiamini na hawataki kufanikiwa. Na, kwa kweli, Israel pia hairidhiki na mpango huo.
Lakini Marekani, Uingereza inashinikiza kufufua mkataba huo, "anabainisha mwandishi wa masuala ya usalama wa BBC.
Michael Stephens, mchambuzi wa Mashariki ya Kati katika Taasisi ya Royal United Services (RUSI) ya London, anaamini hatua za Israel dhidi ya Irani ni jaribio la makusudi la kuhujumu mazungumzo ya nyuklia.
"Waisraeli wanajaribu kwa umoja kukwamisha mpango wa nyuklia wa Irani kwa njia hatari," anaiambia BBC.
"Kwanza, kwa sababu juhudi hizi za Israel zinaweza kudhoofisha nafasi ya mazungumzo ya Marekani wakati inapojaribu kufufua makubaliano ya nyuklia na Iran."
"Lakini pili, Wairan wanaweza kuanza kukabiliana na mashambulio dhidi ya maslahi ya Israel kote ulimwenguni. Israel tayari imeonesha kuwa inaweza kuvuruga mpango wa [nyuklia] wa Iran, lakini athari zitakuwa nini?" Michael Stephens.

Chanzo cha picha, EPA
Nchini Iran pia kuna wengi ambao wanapinga makubaliano ya nyuklia, kama vile Frank Gardner anavyodokeza.
"Rais mpya ni mtu wa karibu sana na kiongozi mkuu, Ayatollah Khamenei, na Wanajeshi wa Iran, na kuna watu wengi katika duru hizi ambao hawataki kuwe na uboreshaji wa uhusiano na Magharibi."
Profesa Christoph Bluth wa Chuo Kikuu cha Bradford haamini kwamba uhasama kati ya Israel na Iran utaongezeka kwa njia hatari.
"Sidhani kwamba hiyo itatokea, kwa sababu lengo la Israel la kuzuia matokeo makubwa katika mazungumzo ya nyuklia linaweza kutofaulu na Israel haiwezi kujiruhusu kuweka uhasama mwingi dhidi ya serikali ya Biden," mtaalamu huyo aliambia BBC Mundo.
Lakini ikiwa visa vya baharini vitaendelea, je! Vita hii ya chinichini inaweza kugeuka kuwa makabiliano ya wazi kati ya Israel na Iran na athari mbaya sio tu kwa nchi zote mbili lakini kwa eneo lote?
"Kuna hatari kubwa, lakini pande zote zinajua kuongezeka kwa hatari," anabainisha Profesa Bluth.
"Hakuna upande unaoweza kumudu vita vya kila mahali, na Israel haiwezi kutegemea uongozi wa Biden kuiunga mkono kwa chochote isipokuwa shambulio lisilokuwa na sababu."
"Serikali ya Biden tayari imeanzisha mashambulio dhidi ya wanamgambo wa Iran huko Syria, kwa hivyo katika mzozo wa Syria, Marekani na Israel ziko pamoja.
Lakini katika mzozo huu wa baharini, Israel ina hatari ya kuachwa peke yake," anaongeza mtaalamu huyo.













