Marekani , Israel na nchi za Magharibi zakabiliwa na sintofahamu juu ya shambulio la meli ya mafuta

Chanzo cha picha, Frank Gardner
Malumbano ya hasira yamekuwa yakiendelea, huku mabalozi wakiendelea kuitwa na Wizara za mambo ya nje na vitisho vya ulipizaji kisasi vimetolewa wazi baada ya shambulio la droni dhidi ya meli ya mafuta lililosababisha mauaji wiki iliyopita .
Uingereza, Marekani na Israeli zote zinailaumu Iran kwa kutekeleza shambulio hilo ambayo inakanusha kuhusika, huku ikiapa kujibu kwa chochote kinatakachodhuru maslahi yake. Lakini je ni nini kilichotokea na nini kilicho nyuma ya shambulio hili ?
Siku ya Alhamisi tarehe 29 Julai, MV Mercer Street, meli ya mafuta, ilikuwa ikisafiri bila mzigo wowote kwenye mwambao wa Oman ikitokea katika mji wa Dar es Salaam nchini Tanzania ikielekea katika Milki za kiarabu- UAE iliposimama katika bandari ya Fujairah iliyopo kwenye Ghuba ya Oman kuongeza mafuta.
Meli hiyo inamilikiwa na Liberia na Japan, ilikuwa inafanyia kazi kampuni inayomilikiwa na Israeli, Zodiac Maritime.
Jioni meli hiyo ilishambuliwa kwa vilipuzi vilivyorushwa na droni, ambavyo vililipuka karibu na daraja, na kuharibu majengo ya makazi yaliyokuwa karibu.
Watu wawili waliuawa- Mromania na Muingereza wote walinzi wa usalama-na baada ya kutoa taarifa kwa njia ya radio za mawasiliano, meli hiyo ilisindikizwa hadi kwenye mwambao na manuari mbili za kivita za Marekani.
Kumekuwa na mashambulio kadhaa siku zilizopita dhidi ya meli za Israeli za uchukuzi mwaka huu, na yote Iran ndio inayolaumiwa kuhusika, lakini Tehran imekuwa ikikanusha.
Israeli pia inaaminiwa kuwa nyuma ya mlipuko wa ajabu uliotokea kwenye meli ya kijeshi ya Iran, inayofahamika kama Saviz, shambulio lililofanyika mwezi Arili katika Bahari nyekundu.

Chanzo cha picha, frank Gardner
Hii ni sehemu ya kile ambacho kimeitwa "vita vya chini kwa chini " baina ya Iran na Israeli. Ni mchezo hatari wa piga-nikupige, ambao unajumuisha mauji yanayoshukiwa kutekelezwa na Israeli ya wanasayansi wa Iran na majaribio yake yaliyofanikiwa ya kuizuia Iran kuendelea na mipango yake ya nyuklia.
Hadi sasa, hakuna mtu yeyote aliyeuawa katika mashambulio dhidi ya meli za usafirishaji
Kosa kubwa la kijasusi?
Kama inavyodai Uingereza, Marekani na Israeli, Iran ilihusika na shambulio basi lilikuwa ni kosa kubwa la majasusi wa Iran. Mzozo wake ulikuwa ni kati yake na Israeli kwa hivyo kumuhusisha mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa - Uingereza-kwa kumuua raia wa Uingereza kumeleta mzozo mkubwa wa kidiplomasia.
Boris Johnson amesema kuwa Iran lazima "ikabiliane na athari za matendo yake" na kulitaja shambulio hilo "shambulio lisilokubalika na la ajabu dhidi ya meli ya kibiashara ".
Balozi wa Iran nchini Uingereza, Mohsen Baharvand, aliitwa katika Wizara ya mambo ya kigeni ya Uingereza kuambiwa kuwa nchi yake lazima isitishe vitendo ambavyo vinatishia safari za uchukuzi za meli za kimataifa .
Iran imetoa taarifa ya hasira ya kukana kuhusika na shambulio, ikitaka ioneshwe ushahidi wa madai ya kuhusika na shambulio hilo
Wizara ya mambo ya nje ya Iran imemuita balozi wa Uingereza mjini Tehran, ikizitaja shutuma zilizotolewa na Uingereza, Israeli na Marekani kama "propaganda zisizokuwa na msingi ".
Ujumbe unaoumiza
Nchi hizo tatu zimeapa kujibu na huku zikiendelea kuelezea wazi kuwa na msimamo wa pamoja zina ajenda tofauti.
Uiongereza na Marekani zinataka sana kufufua mkataba wa mwaka 2015 wa nyuklia na Iran, kile kinachoitwa Mpango wa pamoja wa kina wa kimatendo (JCPOA) ambao uliweka hatua kali dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran ili kuishurutisha kuuachampango hui ili iondolewe vikwazo vikali vya kiuchumi.

Chanzo cha picha, Frank Gardner
Mkataba huo ulisitishwa baada ya Rais Donald Trump kuiondoa Marekani kwenye mkataba huo mwaka 2018.
Mazungumzo yamekuwa yakiendelea mjini Vienna lakini Israeli haifurahishwi na mkataba huo, ikiamini kuwa hautasaidia vyovyote katika kudhibiti mpango wa utafiti wa nyuklia wa Iran.
Hiyo ndio maana wakati Israeli inasema "itatuma ujumbe kwa Iran kwamba itaelewa "inaweza pia kuumiza zaidi na kuchokoza zaidi kuliko ile ya Marekani na Uingereza.
Huduma za ujasusi za Israeli Mossad zimekuwa na ufanisi sana katika kuingia ndani ya taasisi za usalama za Iran kwahiyo ni tisho ambalo linaweza kuwachukuliwa kwa uzito sana mjini Tehran.
Mwishowe, kuna sintofahamu inayozikabili serikali hizo za magharibi kuhusu ujasusi unaozingira shambulio hilo, kama upo, kuufanya kuwa wazi.
Iran inasema: kama kuna ushahidi wa uhusika wetu basi uletwe tuuangalie. Lakini taarifa zozote za ujasusi zilizokusanywa zinaweza kutoa alama za siri na kuingilia ujasusi ambao wapelelezi wa Uingereza na Marekani wanapendelea Iran isizifahamu.

Na wakati huo huo kama watashindwa kuweka wazi kile kinachoitwa "bunduki inayotoa moshi" ambacho kitaihusisha Iran, basi wengi watasema, jambo ambalo tayari wanalisema kwenye mitandao ya kijamii , kwamba hizi ni sababu tu zilizotungwa kwa ajili ya kuiadhibu Iran kwa kitu ambacho haikukifanya.












