Je, Tanzania ilisaidiwa na Cuba, Marekani na Israeli kumpiga Idi Amin?

Chanzo cha picha, HULTON ARCHIVE/GETTY IMAGES
Vita vya Uganda-Tanzania, vinavyojulikana nchini Tanzania kama Vita vya Kagera na nchini Uganda kama vita vya Ukombozi vilihusisha Uganda na Tanzania kati ya Oktoba 1978 hadi Juni 1979. Matokeo yake yalikuwa kutimuliwa kwa Idi Amin madarakani na mwezi kama huu wa Juni 1979 ambapo vita viliisha tunakupakulia kumbukumbu za chanzo na matokeo ya vita hivyo . Leo katika sehemu ya tatu ya makala zetu tunaangazia jinsi vikosi vya Tanzania vilivyoingia mi mkuu wa Uganda, Kampala.

Aprili 10, 1979 Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liliingia jijini Kampala ikiwa ni miezi sita kamili toka vikosi vya Idi Amin vilipoivamia Tanzania na kuzusha vita.
Kwa mara ya kwanza katika historia mpya ya Afrika baada ya ukoloni, jeshi la taifa moja huru liliuteka mji mkuu wa nchi nyengine huru. Maelfu ya wakazi wa Kampala walijitokeza kuwalaki wanajeshi wa Tanzania na washirika wao.
Siku hiyo pia ilitamatisha hasa utawala wa Amin, kutoka siku hiyo alikuwa aikimbia na kujificha maeneo mbali mbali ya nchi hiyo mpaka vita ilipoisha rasmi miezi mitatu baadaye.
Hata hivyo, kabla ya kushikiliwa kwa Kampala, mapambano makali yalishuhudiwa kati ya vikosi vya Tanzania na washirika wake raia wa Uganda waliokuwa wakimpinga Amin dhidi ya vikosi vya Libya na Uganda.
Mwanzoni mwa mwezi Aprili, makombora ya Tanzania yalielekezwa katika mji wa Entebbe. Ndege za kivita za Tanzania pia ziliulenga uwanja wa ndege wa Entebbe, lengo likiwa ni kuiharibu njia ya kutua na kupaa ndege ili kuzuia ndege za Libya zisiendelee kupeleka vifaa vya kivita pamoja na wanajeshi Uganda.
Kamanda wa Tanzania aliyekuwa akiongoza mapambano katika uwanja wa vita, Jenerali David Musuguri alijua kwamba endapo wataishika Kampala kabla ya Entebbe basi adui angeendelea kwa na nguvu na angewashambulia kwa nyuma.
Ndege za Tanzania zilifanikiwa kulipua sehemu ya uwanja huo lakini lengo la kuilipua lami ya kutua na kupaa ndege halikufanikiwa.
Idi Amin akimbia
Entebbe pia ndipo Ikulu ya Rais wa Uganda ilipo, na mapambano ya kuuteka mji huo yalipoanza Idi Amin alikuwa yupo Ikulu.
Mashambulio ya makombora ya Tanzania yakiongozwa na Luteni Kanali Ahmed Boma yalidumu kwa siku tatu. Wanajeshi kadhaa wa Uganda waliogopa na kutoroka.
Idi Amin aliutoroka mji huo kwa kutumia helikopta ya jeshi mara baada ya makombora ya Tanzania kutua kwenye uwa wa Ikulu.
Makombora ya Tanzania yaliongezeka usiku wa Aprili 6, asubuhi ya Aprili 7 vikosi vya Tanzania viliingia barabarani kuelekea Entebbe. Saa nne asubuhi ndege kubwa ya Libya ilitua Entebbe kwa lengo la kuwaokoa wanajeshi wake waliokwama eneo hilo.

Chanzo cha picha, Universal History Archive/Getty
Wanajeshi 30 wa Libya waliingia kwenye ndege hiyo haraka, lakini wakati inaanza kupaa kikosi cha kwanza cha Tanzania kilikuwa kimeshaukaribia uwanja huo na kuilipua ndege hiyo. Hakuna hata askari mmoja wa Libya aliyepona. Baada ya shambulio hilo mamia ya wanajeshi wa Libya walichanganyikiwa na kuanza kukimbia kuelekea Kampala. Wengi wao waliuawa.
Baada ya vita ya kuiteka Entebbe kuisha jioni ya Aprili saba, zaidi ya wanajeshi 300 wa Libya waliuawa. Takriban 50 walitekwa na kupelekwa Tanzania ambapo wote waliachiwa bila masharti yoyote miezi tisa baadaye.
Entebbe ndio lilikuwa eneo la mwisho kwa Gaddafi kushiriki katika vita hivyo, baada ya kupokea kipigo kizito alisalimu amri na kurejesha nyumbani askari wake wote waliosalia.
'Shika Kampala'
Kazi ya kuingia katikati ya Kampala ilipewa kikosi kilichokuwa chini ya Luteni Kanali Ben Msuya. Kikosi hiki kilishiriki vita toka awali kabisa, kikiwa cha kwanza kabisa kuingia uwanja wa mapambano kwa kuvuka mto Kagera na mitumbwi baada ya kuvunjwa kwa daraja na vikosi vya Amini.
Hata hivyo, wanajeshi wa Tanzania hawakukutana na upinzani mkali katika operesheni ya kuingia Kampala. Wanajeshi wengi wa Uganda walishaukimbia mji huo wakiongozwa na Amin mwenyewe ambaye alitoroka Kampala siku moja kabla ya wanajeshi wa Tanzania kuingia.
Washirika wa Amin, vikosi vya Libya pia havikuwepo tena. Wanajeshi wachache wa Amin ambao walijaribu kuwashambulia Watanzania waliuawa haraka.

Chanzo cha picha, TANZANIAGOV
Wakati wote wakisonga mbele, wanajeshi wa Tanzania walikuwa wakisema tena kwa furaha na morali kubwa: "Shika Kampala."
Baada ya kuishika Kampala kikamilifu, Rais mteule wa Uganda Yusuf Lule aliapishwa. Lule aliteuliwa kuongoza serikali ya mpito wa makundi ya waganda waliokuwa wanampina Amin katika mkutano uliofanyika Moshi, Tanzania.
kutoka Kampala majeshi ya Tanzania na washirika wao waliendelea kuondoa mabaki ya wapiganaji wa Amin mpaka walipofika kwenye mpaka na Sudan mwanzoni wa mwezi Juni 1979.
Je, Tanzania ilisaidiwa na Cuba, Marekani na Israeli?
Katika hatua mbali mbali za vita hivyo, Idi Amin alisikika akisema kwamba vikosi vya Tanzania vilikuwa vikisaidiwa na wapiganaji kutoka nchi kadhaa zenye nguvu za kijeshi.
Mataifa ambayo aliyataja Amin mara kwa mara yalikuwa ni Cuba, Marekani na Israeli. Hata hivyo madai hayo yalikuwa hayana ukweli wowote.
Lakini je, Amin alipata wapi taarifa hizo?
Baada ya majeshi ya Tanzania kuingia Uganda na kuudhibiti mji wa mpakani wa Mtukula, mipango ilifanyika ili kuingia katika miji ya Masaka na Mbarara.

Chanzo cha picha, Google
Siku moja kabla ya kuanza kwa mapambano ya miji hiyo, makamanda wa vikosi vya Tanzania walikutana kwa mara ya mwisho na kunywa kidogo pamoja. Waliporudi kwenye vikosi vyao usiku wakaanza kupigiana simu ya upepo na kuulizana kwa utani: "Je, Wacuba wapo tayari upande wa kulia?" kamanda mwengine anajibu "ndiyo afande". "Je, Waisraeli wapo tayari upande wa kushoto? Ndiyo afande... Je, Wamarekani wapo tayari hapo kati? Ndiyo afande."
Wakati huo, maafisa wa intelijensia kutoka pande zote mbili walikuwa wanafuatilia mawasiliano ya wenzao, na utani wa Watanzania uliaminiwa na Waganda. Baadhi wa wanajeshi wa Amin waliogopa 'kukabiliana' na majjeshi hayo ya kigeni na kutimua mbio.
Kesho yake, Amin aliongea kwenye redio na kutangaza kuwa nchi yake imevamiwa na madola yenye nguvu za kijeshi. Dunia ilimcheka, lakini haikujjua kuwa chanzo cha taarifa yake kilikuwa ni makamanda wa Tanzania.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, japo Tanzani ilipata michango mbalimbali ya silaha kutoka nchi rafiki kama Algeria, Angola, Zambia na Ethiopia. Nchi pekee iliyopeleka askari wake Uganda kuisaidia Tanzania ni Msumbiji ambayo ilitoa batalioni moja ya wanajeshi 800.
Ikumbukwe kuwa Tanzania ilipeleka wanajeshi wake kusaidiana na wapiganaji wa Frelimo katika vita ya ukombozi ya nchi hiyo dhidi ya wakoloni wa Kireno. Vita hivyo vilitamatika kwa kupatikana Uhuru wa Msumbiji.
Usikose sehemu yamwisho ya makala hizi kesho Julai Mosi kuhusu Vita ya Kagera ama Vita ya Ukombozi ambapo tutaangazia jinsi Idi Amini alivyonusurika kukamatwa au kuuawa na majeshi ya Tanzania na washirika wake na namna alivyotoroka Uganda na kwenda kuishi uhamishoni mpaka umauti ulipomfika.













