Bwawa la Ethiopia: Je Misri inajitayarisha kijeshi dhidi ya Ethiopia?

Chanzo cha picha, Getty Images
Misri inajitahidi kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na kijeshi barani Afrika huku mzozo wake na Ethiopia ukiendelea kutokota juu ya kujengwa kwa bwawa kubwa la umeme katika kijito cha mto Nile.
Shirika la Kijiografia la Misri ambalo lilianzishwa mwaka 1875 linajumuisha baadhi ya hati muhimu ambazo zinaakisi maslahi ya Misri ya muda mrefu katika nchi za Afrika zilizopo kusini mwa eneo la Sahara.
Baadhi ya nyaraka hizo zilizojumuishwa katika shirika hilo ni ramani ya kihistoria ambayo inaonesha kuwa mpaka wa Kusini wa Misri upo katika Ziwa Victoria eneo la Afrika Mashariki.
Shirika hilo lilianzishwa enzi ambayo Misri ilikuwa inadhibiti Sudan na ikawa inataka kuvamia Ethiopia katika kampeni mbaya ya kijeshi kati ya mwaka 1874 na 1876 ambapo Misri iliishia kushindwa vibaya.
Baada ya karibu miaka 70, Misri iliomba msamaha kwa vitendo vyake vya kibeberu ilipokuwa ndiyo nchi yenye viwango vya juu inayopigania uhuru wa Afrika na zaidi wakati wa ukoloni.
Hata hivyo, kujihusisha sana na vita vya Waarabu na Israeli kulichangia kupungua kwa shauku yao katika nchi za eneo la Sahara.
Aidha, miaka ya hivi karibuni Misri imeshuhudiwa ikifanya mazungumzo na nchi kadhaa zinazopakana na mto Nile.
Misri pia imesaini mikataba kadhaa ya kijeshi na kiuchumi na Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na Djibouti miezi ya hivi karibuni.
Misri tayari imehitimisha mikataba mikubwa na Sudan wakati nchi hizo mbili zilipofanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi ambapo ndege za kivita na vikosi maalum vilishiriki.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ethiopia inasema kuwa bwawa hilo litawezesha upatikanaji wa umeme kwa raia wake milioni 65.
Pia, Misri imeunganisha eneo lake la usambazaji umeme na Sudan na mipango inaendelea ya kuunganisha njia za reli pamoja na nia ya kuendesha huduma ya treni kutoka Alexandria hadi mji wa Cape Town Afrika Kusini.
Sababu kubwa iliyochangia kubadilishwa kwa sera yake ya kigeni ni bwawa lililozua utata ambalo linajengwa na Ethiopia katika eneo la mto Nile linalofahamika kama Grand Ethiopia Renaissance Dam.
''Misri siku zote imekuwa ikitegemea diplomasia kutatua mtafaruku kati yake na Ethiopia kuhusu bwawa hilo, lakini inaonekana mazungumzo ni kama yamefikia mwisho au ni kama yanakaribia kufika mwisho,'' amesema Nael Shamma, mtaalamu wa sera ya mambo ya kigeni ya Misri.
Hofu ya kutokea kwa ukame
Tanzania ni mfano mwingine ambapo Misri imewekeza kikamilifu katika bwana la Julius Nyerere mto Rufiji.
Ni wazi kwamba Misri inataka kuangazia mradi huo kama mfano wa utayari wake kusaidia katika maendeleo ya nchi za mto Nile.

Chanzo cha picha, Getty Images
Na huu ndio ujumbe ambao Misri ambayo haina chanzo kingine cha maji ya kunywa na kilimo isipokuwa mto Nile, inajaribu kuupitisha duniani.
Misri haipingi mpango wa ujenzi wa bwawa la Ethiopia lakini ina wasiwasi na athari za mradi huo kuhusiana na kiwango cha maji ya mto Nile wakati ambapo Ethiopia ilikataa kusaini mkataba wa makubaliano wa namna ya kusimamia bwawa lake na hofu ya kwamba utaathiri eneo lake kubwa linalotumika kwa kilimo na kusababisha ukame mkubwa na ukosefu wa ajira huko Misri.
Kwa upande mwingine, Ethiopia inachukulia Bwawa la Renaissance kuwa muhimu katika mahitaji yake ya maendeleo na kutoa umeme kwa wakazi wake.
Uhusiano wa kibiashara na kijeshi
Ni wakati wa Misri kubadilisha mwelekeo na kuangazia zaidi sera yake ya kigeni katika eneo la Jagwa la Sahara Afrika lakini baadhi ya raia wa Misri wanasema hatua hiyo imechelewa sana.
''Kuwa na ushawishi wa kisiasa hii leo sio tu kumiliki silaha,'' amesema Walaa Bakri, mfanyabiashara na mshauri wa kitaaluma chuo kikuu cha Westminister.
Aliandika: '' Makubaliano ya kiusalama na baadhi ya nchi zinazopakana kwenye mto Nile kama vile Burundi, Rwanda na Uganda ni kuzuri lakini hakuwezi kutoa fursa ya ushawishi unaohitajika na Misri''.
Anasema kuwa na uhusiano imara wa kibiashara kunaweza kuchangia kufikiwa kwa mengi zaidi ya ushirikiano wa kijeshi na kuangazia kidogo tu ambayo Misri inaweza kufaidi kutoka kwa nchi zote 9 inazoshirikishana nazo za mto Nile:
''Hakuna ambaye anasema kwamba Misri inastahili kununua kile ambacho haikihitaji kutoka kwa nchi hizi. Hapana, lakini kwa mfano, nchi za mto Nile zinazalisha kiwango kikubwa cha kahawa na Misri inatumia zaidi ya dola milioni 95.5 kwa mwaka kuingiza bidhaa hii nchini mwake, asilimia 95 ikiwa inatoka nje ya Afrika.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati huo huo, kwa mtindo ambao Misri inakabiliana na Ethiopia hali inaendelea kupamba moto.
Hakika, utawala wa Misri na hata rais mwenyewe anapitia shinikizo kubwa la kuendelea kuongeza msisitizo na kuwa imara zaidi katika suala la Ethiopia.
Hata wanaowaunga mkono kama vile Abdel Fattah al-Sisi walianza kuzungumza bila hata kutarajiwa akisema kwamba kushindwa kulinda haki za maji ya Misri kuna maanisha kupoteza haki za kutawala Misri.
Inaonekana kana kwamba Misri ina matumaini ya kuunda washirika wake katika kupata nguvu zaidi ikiwa kukabiliana na Ethiopia katika suala hili litakuwa jambo lisiloweza kuepukika.
Misri na Sudan zote zimepeleka mgogoro juu ya bwawa hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hasa ikizingatiwa kwamba kunatishia amani na uthabiti wa eneo hilo.
Suala hilo lilikuwa katika Baraza la Usalama na likawasilishwa katika Umoja wa Afrika ambayo ilishindwa kuutatua.
Misri na Sudan zinalaumu Ethiopia huku Ethiopia ikishutumu utumiaji wa majadiliano kama njia ya kujithibithishia kuwa wao ndio watumiaji pekee ya maji ya mto Nile ikirejelea mgao wa maji ya mto Nile ambao Misri inapigania.

Chanzo cha picha, Reuters
Sasa ni wazi kwamba mazoezi ya pamoja ya kijeshi yaliyofanyika Sudan yalilenga kutuma onyo sio tu kwa Ethiopia lakini kwa dunia nzima kwamba nchi hizo mbili hazitasita kutumia wanajeshi wake ikiwa kutakuwa na haja ya kufanya hivyo katika suala la kuchagua maisha au kifo kwa nchi hizo mbili kama vile suala la maji.
Inaonekana kana kwamba makubaliano ya kijeshi kati ya Misri, Uganda, Kenya na Burundi kunasisitizia ujumbe huu ingawa ni vigumu kufikiria kwamba nchi hizi huenda zikashinikizwa kuingia katika mgogoro wa vita vya eneo ambao hauna uhusiano na maslahi yao.
Na ikiwa njia ya kutatua mgogoro huu kidiplomasia itashindwa kufua dafu, hakuna uwezekano mkubwa wa raia wa Misri kuunga mkono hatua za kijeshi iwapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.

Chanzo cha picha, Reuters
Wakati huo huo, Sudan hali ni tofauti na Misri. Kuna kiwango fulani cha sintofahamu kwasababu Sudan itanufaika na bwawa hilo kwa kupunguza kiwango cha mafuriko na kuwezesha upatikanaji wa umeme kwa gharama ya chini.
Hata hivyo, kuna makubaliano ya wigo mpana kutoka kwa wanaofuatilia suala hilo, ambao ni kwamba licha ya ustadi na uwezo wa kijeshi na kisiasa kwa Sudan na Misri, mashambulizi ya namna yoyote ile kuzuia kutekelezwa kwa mradi huo kwa miaka mingi hakutatua tatizo hilo.
Na badala yake, kutaendeleza ukosefu wa uaminifu na kufufua tena malalamiko ya zamani na hali ya kulipiziana kisasi.












