Rais Samia Suluhu Hassan aruhusu balozi na taasisi kuingiza chanjo nchini humo

Kamati ya wataalamu iliundwa kwa lengo la kuishauri serikali kuhusu mwelekeo wa kukabiliana na janga la corona

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

Maelezo ya picha, Rais Samia akipokea mapendekezo ya kamati ilioundwa kuishauri serikali kuhusu Corona

Raia wa Tanzania sasa watakuwa na fursa ya kupata chanjo ya corona nchini kufuatia hatua ya rais wa taifa hilo kuruhusu kuingizwa kwa tiba hizo.

Kulingana na taarifa iliotiwa saini na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu Gerison Msigwa, hatua hiyo inajiri baada ya rais Samia Suluhu Hassan kupokea mapendekezo ya kukabiliana na ugonjwa wa corona .

Rais Samia amesema kwamba balosi na taasisi za kimataifa zimeruhusiwa kuingiza chanjo nchini humo ili kuwachanja raia na watumishi wake ili kuendana na taratibu za nchi hizo mbali na kuondoa kadhia wanazopata katika utendaji kazi wao .

Rais Samia amesema kwamba balosi na taasisi za kimataifa zimeruhusiwa kuingiza chanjo

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

Maelezo ya picha, Rais Samia amesema kwamba balosi na taasisi za kimataifa zimeruhusiwa kuingiza chanjo

Hatahivyo Rais Samia amesisitiza kwamba chanjo hizo zitaletwa kwa utaratibu utakaoratibiwa na wizara ya Afya

Kamati ya wataalamu iliundwa kwa lengo la kuishauri serikali kuhusu mwelekeo wa kukabiliana na janga la corona muda mfupi tu baada ya rais Samia kuchukua madaraka kutoka kwa mtangulizi wake hayati John Pombe Mgufuli

Katika mapendekezo hayo kamati imeishauri serikali kuhusu njia mbalimbali itakazotumia kupata fedha ndani ya bajeti ya serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika ya kimataifa kwa ajili ya kugharamiakia vifaa, tiba mafunzo na chanjo.

Rais Samia Suluhu Hassan

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

Kwa upande wake rais Samia ameipongeza kamati hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wake Profesa Said Aboud kwa kazi nzuri na kumuagiza waziri wa Afya bi Dorothy Gwajima kuandaa andiko litakalowasilishwa kwa baraza la mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa kabla ya serikali kufanya maamuzi kuhusu mapendekezo hayo.