Je malipo ya dola milioni 75 ni sawa kwa mtu aliyefungwa jela kwa miaka 31?

Henry McCollum

Chanzo cha picha, Emily Baxter

Maelezo ya picha, Henry McCollum (pichani) pamoja na kaka yake Leon Brown walitumikia kifungo jela kimakosa kwa miaka 31

Malipo ya kihistoria ya dola milioni 75 (pauni milioni 53 ) yametolewa kwa ndugu wawili wakaazi wa jimbo la North Carolina nchini Marekani ambao walifungwa miongo mitatu jela kwa uhalifu ambao hawakuufanya yameibua tena suala la watu weusi kufungwa bila hatia.

Henry McCollum na kaka yake wa kambo Leon Brown walipatikana na hatia mara mbili ya ubakaji na mauaji ya msichana wa miaka 11 mwaka 1983. Hata hivyo mwaka 2014, kulipatikana ushahidi mpya wa vinasaba vya DNA ambao ulithibitisha kuwa hawakua na hatia kisha wakafutiwa mashtaka na kutolewa jela mwaka uliofuatia.

Ijumaa iliyopita, iliamriwa kuwa walipwe dola milioni 31 kama fidia ya maumivu waliyoyapata, ambapo kila mmoja wao atapata dola milioni moja kwa kila mwaka aliokaa gerezani - na kupewa dola milioni 13 kama fidia ya kufungwa kimakosa kwa kukusudia.

Malipo hayo ni malipo makubwa ya pamoja kuwahi kutolewa kwa watu waliofungwa kimakosa katika historia ya Marekani, kulingana na mawakili wa ndugu hao.

"Ninamshukuru Mungu," alisema Bw McCollum, huku akitokwa machozi, alipokuwa akiondoka katika chumba cha mahakama na kaka yake, takriban miaka saba baada ya jaji kuamrisha waachiwe huru.

"Hata leo, kuna watu wengi wasiokuwa na hatia gerezani," ameongeza McCollum. "Na hawastahiki kuwa jela."

Nini kilichotokea katika kesi hii?

Tarehe 24 Septemba mwaka 1983, polisi katika mji mdogo wa Red Springs jimboni North Carolina walipata mwili wa msichana mwenye umri wa miaka 11 katika shamba la soya.

Siku iliyofuatia, kwa kuzingatia tetesi walizozipata kutoka kwa mwanafunzi mwenzake, waliwakamata Bw McCollum na Bw Brown, ambao ni wamarekani weusi wakati huo wakiwa vijana wadogo, wa miaka 19 na 15 mtawalia.

Baada ya saa kadhaa za kufanyiwa mahojiano wakiwa hawana wakili wa kuwawakilisha, maafisa wanasemekana waliwalazimisha wawili hao kusaini waraka wa kukiri kosa hilo uliowahusisha na uhalifu.

Nyaraka za mahakama zinasema kuwa kaka hao wawili walikuwa na matatizo ya utambuzi wa mambo na hawakuweza kusoma vyema, kuandika au hata kuelewa walichokuwa wakisaini.

Wote walihukumiwa kifo. Bw Brown alikuwa mfungwa mwenye umri mdogo zaidi wa North Carolina katika orodha ya wafungwa waliohukumiwa kifo, lakini baadaye akahukumiwa kifungo cha maisha jela. Bw McCollum aliendelea kuwa mfungwa wa muda mrefu wa jimbo aliyetumikia kifungo aliyeko katika orodha ya kifo.

Hakuna uchunguzi au ushahidi wa uchunguzi wa maiti uliowahi kuwahusisha kamwe ndugu hao wawili na uhalifu huo.

Mwaka 2014, matokeo ya vipimo vya vinasaba -DNA yalifichua muhusika halisi wa uhalifu: Roscoe Artis, muuaji aliyepatikana na hatia anayetumikia kifungo cha maisha jela kwa mashitaka tofauti lakini yanayofananana.

Je, suala la utiwaji hatiani wa watu kimakosa Marekani ni la kawaida kwa kiasi gani?

Sajili ya kitaifa kuhusu watu waliotiwa hatiani na kisha kugundulika hawakuwa na makosa imerekodi majina ya watu 2,784 tangu data zilipoanza kukusanywa katika mwaka 1989.

Zaidi ya nusu ya kesi hizi zote zilihusisha baadhi ya aina fulani ya waendesha mashitaka au ukiukaji wa maadili ya kikazi ya watekelezaji wa sheria.

Karibu 50% ya watu ambao waliotiwa hatiani na baadaye kubainika kuwa hawana hatia wamekuwa ni wamarekani weusi.

Sajili hiyo pia ilibaini kuwa watu weusi wana uwezekano wa kutiwa hatiani kimakosa mara saba zaidi kuliko wazungu.

Je, fidia kubwa ni za kawaida?

Wamarekani waliotiwa hatiani kimakosa wanaweza kuwasilisha kesi za madai juu ya kukiukwa kwa haki zao-lakini baadhi ya kesi, walalamikaji huishia kutopata chochote.

Ni vigumu hususan kuwawajibisha maafisa wa usalama kwa ukiukaji wa maadili, kwani vitendo vyao vinalindwa kwa kiasi kikubwa chini ya sheria ya sasa ya Marekani.

Lakini shinikizo la kuwafanya polisi na maafisa wengine wawajibike kwa makosa yao linaendelea kuongezeka na vuguvugu la kupinga ubaguzi wa la hivi karibuni.

Kifo cha George Floyd kilichotokea mwaka 2020 katika jimbo la Minnesota kilipelekea kulipwa kwa fidia ya dola milioni 27 na malipo ya dola milioni 12 yalilipwa kutokana na kifo cha Breonna Taylor kilichotokea kentacky.

Hukumu iliyotolewa Ijumaa katika jimbo la North Carolina ilikuja baada ya maafisa wengine wawili wa usalama kuhusika na suala ambalo tayari lilikuwa limelipiwa fidia na kaka hao wawili, kwa kiasi kidogo.

Jamie Lau, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Duke na mtaalamu wa utiwaji hatiani kimakosa katika jimbo hilo, anasema ni "muhimu " kwamba jopo la mahakama liliagiza ndugu hao walipwe dola milioni 1 kama fidia za uharibifu wa maisha yao, huku ikiongeza uwezekano wa malipo makubwa zaidi ya fidia katika siku zijazo.

Lakini alionya kuwa kiasi kikubwa cha dola kinaweza pia kuwa na athari ya kuwalazimisha washitakiwa kumaliza kesi nje ya mahakama kuliko kupeleka mahakamani kesi ambayo inaweza kuwa na athari kubwa kifedha.