Mzozo wa Israel na Palestina: Wanajeshi wa Israel waendelea kukabiliana na wapiganaji wa Kipalestina

Chanzo cha picha, Reuters
Makabiliano kati ya wanamgambo wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na jeshi la Israeli yameongezeka sana, na umoja wa mataifa umeonya kuhusu uwezekano wa kutokea "vita kamili".
Zaidi ya makombora 1,000 sasa yamerushwa na wanamgambo wa Palestina, Israeli inasema.
Israeli imefanya mamia ya mashambulio ya angani, na kuharibu majengo mawili ya ghorofa Gaza Jumanne na Jumatano.
Angalau Wapalestina 53 na Waisraeli sita wameuawa tangu Jumatatu.
Hiyo ni pamoja na watoto 14 wa Kipalestina waliojipata katika mzozo huo.
Katibu Mkuu wa UN António Guterres alisema alikuwa "na wasiwasi mkubwa" na vurugu zinazoendelea.
Machafuko katika miji ya Israeli iliyo na Wayahudi na Waarabu imesababisha mamia ya watu kukamatwa. Makaazi karibu na Tel Aviv yako chini ya hali ya hatari.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema serikali itatumia nguvu zake zote kulinda Israeli kutoka kwa maadui wa nje na wafanya ghasia ndani.
Ni nini kinachofanyika Gaza?
Wapiganaji huko Gaza walianza kufyatua roketi nchini Israeli Jumatatu usiku, na Israeli imejibu kuzilenga sehemu mbali mbali katika eneo la Gaza.
Siku ya Jumatano Israeli ilisema imewauwa maafisa wakuu wa Hamas huko Gaza, na pia ilikuwa ikilenga maeneo ya kurusha makombora.
Hamas - kikundi cha wapiganaji kinachosimamia Gaza - kilithibitisha kifo cha kamanda wake katika Jiji la Gaza.
Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza inasema kuwa zaidi ya watu 300 wamejeruhiwa huko tangu mzozo uanze, na pia wale 53 ambao wamekufa.
Vikosi vya Ulinzi vya Israeli (IDF) vilisema Jumatano kwamba mashambulizi yake huko Gaza yalikuwa makubwa zaidi tangu mzozo wa 2014.
Hamas ilisema ilikasirishwa na "kulenga kwa maadui kwa majengo ya makazi".
Wakaazi walikuwa wameonywa kuhama majengo kabla ya ndege za kivita kushambulia, hata hivyo maafisa wa afya walisema bado kuna vifo vya raia.
Ni nini kinachofanyika Israel?
Siku ya Jumatano asubuhi askari wa Israeli aliuawa na kombora la kuzuia tanki lililofyatuliwa kutoka Gaza kwenda Israeli, IDF inasema.
Watu wawili, mwanamume na binti yake, waliuawa huko Lod wakati roketi iligonga gari lao. Wote walikuwa Waarabu wa Israeli.
Polisi wa Israeli walisema kwamba kulikuwa na kile kilichoelezea kama ghasia katika maeneo kadhaa ya nchi usiku mmoja, ambapo watu 270 walikamatwa.
Masinagogi na biashara huko Lod yalichomwa moto.
Bwana Netanyahu alielezea ghasia hizo kama "zisizostahimilika" na akasema zinawakumbusha Wayahudi historia yao ya zamani.
Ni nini kimesababisha ghasia?
Mapigano kati ya Israeli na Hamas yalisababishwa na siku kadhaa za kuongezeka kwa mapigano kati ya Wapalestina na polisi wa Israeli kwenye uwanja mtakatifu wa kilima huko Mashariki mwa Yerusalemu.
Eneo hilo linaheshimiwa na Waislamu wote, ambao huiita Haram al-Sharif (Patakatifu Pema), na Wayahudi, ambao inajulikana kama Mlima wa Hekalu.

Chanzo cha picha, EPA
Hamas ilidai Israeli iwaondoe polisi kutoka huko na wilaya iliyo karibu zaidi ya Kiarabu ya Sheikh Jarrah, ambapo familia za Wapalestina zinakabiliwa na tishio la kufukuzwa na walowezi wa Kiyahudi. Hamas ilizindua makombora wakati makataa yake hayakutiliwa maanani.
Hasira ya Wapalestina tayari ilikuwa imesababishwa na wiki kadhaa za mivutano katika Mashariki ya Jerusalem, na kusababisha mapigano kadhaa na polisi tangu kuanza kwa mwezi mtukufu wa Kiislamu wa Ramadhani katikati ya Aprili.














